JESHI la Polisi mkoani hapa, linamshikilia dereva wa basi la abiria linalofanya safari kati ya Mwanza na Morogoro, kwa tuhuma za mwendo kasi na kukutwa na leseni ya kuendesha pikipiki kinyume cha sheria.
Dereva huyo alibambwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhani Ng’azi katika Kituo cha mabasi Tinde, mkoani Shinyanga, wakati wa ukaguzi wa mabasi yanayofanya safari usiku kutoka jijini Mwanza kuelekea mikoa mingine nchini.
“Huyu sio dereva wa gari la abiria, leseni yake ukomo wake ni kuendesha pikipiki, hatuwezi kumvumilia kuendelea kufanya shughuli hii nyeti bila vigezo," alisema Ng'anzi.
Alisema wanaendelea na operesheni ya ukaguzi wa magari yanayofanya safari usiku kuanzia mkoani Mwanza na Shinyanga.
Katika operesheni hiyo, mabasi 53 yalikaguliwa, kuandikiwa faini 15 na madereva waliobanika kutokidhi vigezo ni wawili.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, madereva wa mabasi ya abiria 105 wamefungiwa leseni, baada ya kubainika kukiuka sheria za usalama barabarani, ikiwa ni ongezeko la madereva 10.
Alisema baadhi ya makosa hayo ni mwendo kasi, kuchezea mifumo ya udhibiti mwendo (VTS) na kuwa katika operesheni hiyo, mabasi mawili yamezuiwa kuendelea na safari kutokana na ubovu.
Ukaguzi huo unafanyika, ili kudhibiti ajali za barabarani zinazotokea hususani katika kipindi cha mwisho wa mwaka.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED