Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Mohamed Mtulyakwaku, amewataka wananchi waliofikiwa na miradi ya umeme vijijini kuhakikisha wanaunganisha nyumba zao na umeme kwa lengo la kujiletea maendeleo.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mabama, wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora, Mtulyakwaku alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imewekeza gharama kubwa kufikisha miundombinu ya umeme vijijini.
“Nitoe rai kwa wale wote ambao miundombinu imefika karibu na nyumba zenu, mhakikishe mnaunganisha umeme ili kufanikisha maendeleo yenu,” alisema.
Aidha, aliwataka wananchi kulinda miundombinu hiyo na kuepuka tabia ya kuchoma moto nguzo za umeme wakati wa maandalizi ya mashamba. Pia aliwahimiza kutumia umeme kwa maendeleo ya kiuchumi kupitia biashara kama saluni, sehemu za kuonyesha mipira, na kuuza vinywaji baridi.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Miradi ya REA Mkoa wa Tabora, Mha. Oscar Migani, alieleza kuwa miradi yote inayotekelezwa na REA itakamilika kwa ubora na wakati uliokusudiwa. Aliongeza kuwa vijiji vyote 156 vya Wilaya ya Uyui vimefikishiwa umeme, huku vitongoji 468 kati ya 706 vikifaidika na huduma hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED