KLABU ya Tabora United imesema kwa sasa hakuna mazungumzo na klabu yoyote yanayoendelea juu ya uhamisho wa winga wao, Offen Chikola kwa ajili ya kumsajili kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, huku ikiweka bayana kuwa haendi kokote.
Na Adam Fungamwango
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Christina Mwagala amesema jana kuwa hakuna dili lolote kutoka klabu yoyote, linalomhusisha mchezaji wao huyo ambaye kwa sasa yupo kwenye majukumu na kikosi cha timu ya Tanzania Bara kinachoshiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, Zanzibar.
Mwagala alisema hayo kufuatia baadhi ya vyombo vya habari kuripoti kuanzia juzi juu ya mchezaji huyo aliyeipa mafanikio makubwa Tabora United kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kutakiwa na klabu ya KMC kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi chao.
"Kumekuwa na taarifa au tetesi za mchezaji wetu Chikola kuwa ana mazungumzo na moja ya klabu inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Uongozi wetu unapenda kuwafahamisha mashabiki wa soka kuwa hakuna mazungumzo yoyote ambayo yamefanyika kati yetu na hiyo klabu kwa sababu Chikola bado ana mkataba na klabu sisi na ataendelea kuitumikia timu yetu. Kwa maana hiyo timu yoyote ambayo ingekuwa inamhitaji ingekuja kwanza kwetu, lakini pia hatuwezi kumuacha kwa sasa kwani ni mchezaji muhimu kwetu," alisema Mwagala.
Chikola amekuwa na mwanzo mzuri msimu huu akiwa na kikosi cha Tabora United ambacho kimekuwa tishio kwenye Ligi Kuu hadi kutamatika kwa mzunguko wa kwanza, ikimaliza kwenye nafasi ya tano kwenye msimamo baada ya kucheza michezo 15 na kushinda michezo saba, sare nne na kupoteza michezo minne ikiwa na pointi 25.
Wakati huo huo, klabu hiyo imesema imewapa mapumziko mafupi wachezaji wake kabla ya kurejea tena kuanza mazoezi kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuanza mwezi Machi.
Mwagala amesema mapumziko hayo yametokana na kusimama kwa ligi, lakini pamoja na hayo wameamua kutoa ya muda mfupi ili kutowafanya wachezaji wasiwe na utimamu wa mwili.
"Tumewapa mapumziko ya muda mfupi tu, nadhani mpaka mwishoni mwa mwezi huu tutarejea tena kambini kujiandaa na ligi," alisema Ofisa Habari huyo.
===
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED