WAKATI uongozi wa Simba ukithibitisha nyota saba wa kigeni wako nchini kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kujiunda na Wekundu wa Msimbazi, straika wa Rivers United, Augustine Okejepha, amekamilisha mazungumzo ya kuitumikia klabu hiyo katika msimu ujao wa mashindano, imefahamika.
Taarifa za ndani kutoka Simba zinasema nyota huyo raia wa Ghana amesaini mkataba wa miaka mitatu na anatarajiwa kuwasili nchini mapema wiki ijayo.
Chanzo hicho kimesema Okejepha ameichagua Simba kutokana na rekodi walizonazo na kukataa dau la Dola za Marekani 220,000 zilizowekwa na mabosi wa Orlando Pirates inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
"Tunashukuru mchakato wetu wa usajili unakaribia kufika mwisho, idadi kubwa ya wachezaji tuliowalenga wameshapatikana, tunataka kwenda kuanza kambi tukiwa na kikosi kamili," kimesema chanzo chetu.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ameliambia gazeti hili wachezaji hao wametua kwa nyakati tofauti kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo na hatimaye kusaini mikataba na kuanza kuitumikia Simba.
Ahmed amesema uongozi wa klabu hiyo umejipanga kufanya usajili mkubwa kwa sababu wanataka kurudisha heshima na hadhi ya klabu.
"Tuna wachezaji wapya saba wa kigeni wapo hapa hapa Tanzania kwa ajili ya usajili, bahati nzuri si watu wengi wanaowafahamu, lakini pia wapo chini ya ulinzi mkali, napenda kuwaambia wanachama na mashabiki wa Simba wasione kimya wakadhani hakuna kinachofanyika.
Wakati haya majembe saba yapo Dar, baadhi ya viongozi wetu wamegawana majukumu, kuna mmoja yuko Zambia, yupo aliyekwenda Ivory Coast, kuna anayesafiri kwenda DRC (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), mmoja Maylasia, kote huko wanakwenda kumalizana na wachezaji," amesema Ahmed.
Ameongeza kwa mara ya kwanza baada ya misimu mingi Simba itakuwa na wachezaji wengi wapya katika kikosi chake na hii inafanyika kwa malengo ya kutengeneza timu mpya itakayorudisha heshima ya klabu.
"Tunafanya ukarabati mkubwa, timu hii lazima tuijenge upya, watu wamechoka, wanataka furaha, wanataka makombe, hawataki kuendelea kuyaona ya zamani, wanataka kuyaona mapya, huwezi kuyapata kama hujatengeneza timu bora," meneja huyo amesema.
Ingawa hakuwa tayari kutaja majina ya wachezaji waliokuja nchini kujiunga na Simba, chanzo chetu kimebaini yuko kiungo mshambuliaji, Jean Ohoua (22), kutoka Stella Adjame ya Ivory Coast, kiungo mkabaji mwenye asili ya Angola, Debora Fernandes Mavambo (Mutondo Stars - Zambia), na beki wa kushoto, Valentin Nouma ambaye ni raia wa Burkina Faso na msimu uliopita alikuwa akiichezea Rahimo FC.
Pia yupo winga mchachari, Jushua Mutale, kutoka Power Dynamos ya Zambia.
Kuhusu kuchelewa kutoa 'thank you' kwa wachezaji wengine, Ahmed amesema kinachokwamisha mchakato huo ni baadhi yao bado wana mikataba na kinachofanyika ni mazungumzo ya kuvunja mikataba hiyo.
"Tuko katika mazungumzo ili tuachane nao kwa amani, hatutaki kuwa wadaiwa sugu wa FIFA, tukishamalizana tutamalizia kutangaza tunaowaacha, huku tukisubiri usajili wote ukamilike ndiyo tuanze kutangaza, hatutaki tutangaze leo halafu kesho tukae kimya," ameongeza.
Tayari Simba imeshatangaza itasafiri kwenda katika jiji la Ismailia, Misri ili kuweka kambi kwa lengo la kujiandaa na msimu mpya wa mashindano huku Tamasha la Simba Day likipangwa kufanyika Agosti 3, mwaka huu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED