Fadlu: CS Sfaxien hawachomoki leo

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 12:58 PM Jan 05 2025
Kocha Mkuu Simba SC, Fadlu Davids
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu Simba SC, Fadlu Davids

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, Simba, leo itakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi, nchini Tunisia kucheza mchezo wa raundi ya nne hatua ya makundi dhidi ya, CS Sfaxien, huku Kocha Mkuu, Fadlu Davids akisema kutokana na mazoezi, mbinu na maelekezo aliyoyatoa kwa wachezaji wake, anaamini watapata ushindi kwenye mchezo huo.

Akizungumza akiwa mjini Tunis, Fadlu, alisema baada ya kuwaangalia wapinzani wake jinsi wanavyocheza, amewapa wachezaji wake mbinu za kucheza nao, akiwaelekeza wachezaji jinsi gani wanatakiwa kucheza wakati wakiwa na mpira na vipi wazuie wakati wakiwa hawana mpira miguuni.

Fadlu alisema amewakumbusha wachezaji wake kuwa makini na makosa madogo madogo ambayo yalifanyika kwenye mchezo dhidi ya CS Constantine nchini Algeria na kusababisha kupoteza kwa mabao 2-1.

"Maandalizi ya mechi yamekamilika, kilichobaki ni kwenda kutimiza kile nilichowaambia wachezaji uwanjani, kila mmoja anatakiwa atimize majukumu yake. Tumeiangalia timu hii udhaifu wake na nguvu zake, nimewapa wachezaji wangu mbinu za kuwakabili, nadhani hawatoniangusha.

Nimewaambia wasirudie tena makosa yaliyofanyika kwenye mchezo dhidi ya CS Constantine, kwani makosa binafsi yaliathiri mchezo mzima tukajikuta tunapoteza katika mechi ambayo ilibidi tuondoke na pointi tatu au moja," alisema kocha huyo.

Mchezaji mwandamizi wa timu hiyo, Shomari Kapombe, amesema yeye na baadhi ya wachezaji wenzake hawana wasiwasi kwani wameshacheza sana na timu za Afrika Kaskazini maarufu kama timu za 'Waarabu', hivyo wanajua jinsi gani ya kuwakabili.

"Sisi kama wachezaji tumeshacheza sana na Waarabu, kuna aina fulani ya uchezaji wao wakiwa nyumbani, huwa wanafanya mashambulizi makali mwanzoni ili kupata mabao ya mapema, lakini nina imani kwa mbinu anazotupa mwalimu na anazoendelea kuelekeza hadi tutakapoingia uwanjani, tutajua jinsi gani ya kuwadhibiti," alisema  Kapombe.

Nahodha wa timu hiyo, Mohamed Hussein 'Tshabalala', amesema kitu ambacho wanaingia kupigania katika mchezo wa leo ni ushindi ili kurahisisha kazi ya kutinga hatua ya robo fainali kwani kwa misimu yote wamekuwa wakifika hatua hiyo baada ya michezo ya mwisho.

"Safari hii wachezaji tumeambizana tufuzu robo fainali mapema tofauti na misimu iliyopita na ili iwe hivyo ni lazima tushinde mchezo huu," alisema.

Simba ambayo ipo kwenye Kundi A, inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi sita, iwapo itashinda leo itafikisha pointi tisa huku ikiwa imebakisha michezo miwili dhidi ya Bravo do Maquis ya Angola ugenini na CS Constantine nyumbani.

Wenyeji wa mchezo huo, CS Sfaxien wanakwenda kucheza mechi ya nne ikiwa haina pointi yoyote katika michezo mitatu iliyocheza mpaka sasa.