Wakili Minde umenena afya ya akili ni pasua kichwa

By Godfrey Mushi , Nipashe Jumapili
Published at 02:58 PM Apr 28 2024
Afya ya akili ni pasua kichwa kwenye jamii.
PICHA: MAKTABA
Afya ya akili ni pasua kichwa kwenye jamii.

WANAHARAKATI ni sauti ya watu wasio na sauti. Wanaharakati hao wanaweza kuchochea mabadiliko makubwa ya mageuzi ya fikra, uchumi na mwenendo wa siasa za eneo fulani kama wanaona linalegalega na linahitaji ufumbuzi wa haraka.

Wana nafasi kubwa sana ya kuondoa mipaka kati ya rika, rangi, itikadi, jinsia na hali zote za kiuchumi.

Kwa nini naandika haya? Siku mbili zilizopita, nilimsikia mwanaharakati wa haki za binadamu na Wakili mkongwe nchini, Elizabeth Minde, akieleza kwa uchungu namna watoa huduma za kijamii hivi sasa wanavyoathirika kwa matatizo ya afya ya akili na trauma (kiwewe).

Mwanaharakati huyo anapigania watoa huduma wanaofanya kazi zinazofanana kama mashirika ya kiraia kusaidi wenye matatizo hayo, kupewa ujuzi wa kukabiliana na changamoto ya afya ya akili wakiwa katika mazingira ya kazi au nyumbani, ili kuhakikisha kupungua kwa matatizo hayo kwenye jamii, ambako inaonekana tatizo hilo limekithiri.

Anamaanisha kwamba matokeo ya matatizo ya afya ya akili na trauma hivi sasa, yanawaathiri wao na wateja wao.

Akashauri ifike mahali, serikali na wadau wake waje na mafunzo maalum, kwa sababu sasa yanaathiri na watoa huduma wanaoshughulika kila siku kupokea wateja mbalimbali kwenye masuala ya kisheria.

Minde anaamini kwamba kuwajengea uwezo kutasaidia kuangalia wanaharakati na afya zao za akili, na yale wanayokumbana nayo katika harakati, kuanzia familia zao, wanakutana na kesi ngapi na lipi suluhisho la afya zao za akili.

Nanukuuu: “Impact (matokeo) ya hivi vitu ni nini jamani, hata kwetu, inatuathiri sisi na wewe. Kwa hiyo lazima tujue namna ya kuhimili huo mlolongo inakuwaje, kwa sababu si tu tunazungumza trauma ya mteja, tunazungumzia trauma ya watoa huduma pia.

“Unapozungumzia afya ya akili, wanakusimulia kama vile wewe ni kichaa, lakini ni kitu ambacho kinatokana na mwingiliano wa matatizo, inakuathiri wewe na inamuathiri na yule aliyekuja kwako, naye ameathirika vilevile.

Anakwenda mbali zaidi kwa kusema: "Mtu mwenye tatizo la afya ya akili, kwa mtu ambaye si mtaalamu anatakiwa amuonyeshe sehemu ya kwenda au kumpatia ushauri wa awali, na kwa mtu ambaye ni mtaalamu, anatakiwa kumshauri na kumfanyia rufaa kwa wataalamu wengine,maana changamoto hii ina athiri wakati mwingine hadi mwili."

Niliposikia maneno hayo ya Wakili Minde, nilimtafuta haraka haraka, rafiki yangu, Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili wa Hospitali ya Rufani ya Kanda ya KCMC, Editruda Gamassa, nikamshirikisha kuhusu hayo yanayozungumzwa na wanaharakati.

Alinijibu kwa kifupi tu kwamba magonjwa ya afya ya akili ni matatizo ya ubongo ambayo humfanya mtu kuwa na hisia, fikra na matendo tofauti na yale yanayotarajiwa na jamii. Pasina shaka kwamba ni kawaida kuwa na hisia kali, kutokana na tukio la kufadhaisha au la kuogofya.

Dk. Gamassa akaniambie tena, kwamba ni kawaida kuwa na miitikio mikali ya kihisia au kimwili. Kwamba, watu wanaweza kupata aina mbalimbali za athari za kimwili, kiakili, kihisia na kitabia.

Kitaalam anasema tukio la kiwewe ni tukio lolote maishani ambalo husababisha tishio kwa usalama wetu na kuwezekana kuweka maisha yetu au ya wengine hatarini.

Kwa hiyo, mtu hupata viwango vya juu vya dhiki ya kihisia, kisaikolojia, na kimwili ambayo huvuruga kwa muda uwezo wake wa kufanya shughuli kwa kawaida katika maisha ya kila siku.

Mifano ya matukio yanayoweza kuhuzunisha ni pamoja na misiba ya asili, kama vile mafuriko, kupata ajali mbaya ya gari, kuwa ndani ya ndege ambayo inalazimika kutua kwa dharura, au kushambuliwa kimwili.

Licha ya kuwapo mambo mengi unayoweza kuyafanya ili kukabiliana nayo na kupona kiwewe, baada ya kupata msaada wa kitaalamu ili kuanza kurudi katika hali ya kawaida.

Walakini mara nyingi, athari hizi hupungua kama sehemu ya mchakato wa uponyaji wa asili wa mwili na kuzoea.

Godfrey Mushi, ni Mwandishi Mwandamizi wa Nipashe, Kanda ya Kaskazini. Anapatikana kwa barua pepe: [email protected] Simu ya mkononi: +255 715 545 490