Ushauri bila matusi inawezekana

By Magabilo Masambu , Nipashe Jumapili
Published at 01:22 PM Apr 21 2024
Kutoa Ushauri bila matusi inawezekana.
PICHA: MAKTABA
Kutoa Ushauri bila matusi inawezekana.

SIFA kubwa tuliyokuwa nayo kama nchi ilikuwa juu ya umoja wetu. Majirani na dunia nzima walijua hivyo ndiyo maana wenye shida na nchi zao sisi tulikuwa washauri na wasaidizi wao. Inawezekana bado tu washauri wao lakini nafikiri sasa wanaweza kuwa wanatutazama tofauti.

Tunajenga nchi kwa wanufaa yetu sote na vizazi vyetu ya nini tugombanie fito? Pengine wakati mwingine kutotambua wapi fito na miti iliyojenga nyumba yetu ilikotoka, hilo linaweza kuwa tatizo. Kuna wakati kutofahamu sawasawa historia ya mafanikio yetu, kunaweza kuzaa laana ambayo inaweza kuwa inatufarakanisha bila kujijua. Lakini bado naamini tunaweza kusemezana kwa lugha tulizofundishwa kutumia majumbani.

Kuna umuhimu wa kuwa na mawazo jumuishi kwa maana ya kusikiliza kila mtu anasema nini kuhusu sisi au nchi. Nikubaliane na kauli ya Rais Samia Suluhu aliyowahi kuitoa wakati wa mkutano wake na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kwamba katika nchi hii hakuna mwenye hatimiliki na kwamba tuishi kwa kuheshimiana.

Ukweli huo unapaswa kuheshimiwa na kila mmoja wetu kwa sababu sheria hazipaswi vilevile kusimamiwa kwa kubaguliwa maana tunaambiwa sheria ni msumeno na kwamba unakata pande zote japo mingi ninayoifahamu ina makali upande mmoja na upande mwingine ni butu. Kwa hiyo inaweza kutumika kukata upande mmoja na kuacha upande mwingine!

Mivutano inaweza kutumika kama mifupa anayorushiwa mbwa anayemfukuza mwizi na  mwisho wa siku, mwizi hatakamatwa na badala yake mbwa ataendelea kuzubaa akila mifupa hiyo ambayo pia ataishia kuilambalamba tu kwa sababu hana uwezo wa kuitafuna.

Maana yangu ni kwamba leo tuna zaidi ya miaka 60 ya uhuru na maendeleo tulio nayo leo hatuwezi kujivuna sana japo nakubali kwamba yako mambo yamefanyika katika ujenzi wa miundombinu, elimu, afya na maeneo mengine lakini kusema kweli pengine tusingekuwa na hii mivutano na malumbano ya huyu kamtukana yule na kadhalika, tungalikuwa tumepiga hatua zaidi.

Siku tutakayotambua kwamba kila mmoja katika nchi hii ana mchango katika maendeleo  bila kutazama dini, kabila, chama cha siasa anachotoka na kwamba mawazo na jitihada zake zinatumika na kuheshimika, basi tungalikuwa mbali zaidi ya hapa.

Inawezekana tunayo matatizo katika maeneo ya kisheria basi yatazamwe. Kama ni ya kimaadili yazungumzwe ili mradi turudi pamoja kama taifa moja lenye nia moja ya kujenga nchi. Bahati mbaya tuliyo nayo ni kwamba nia njema zinazungumzwa lakini hazitekelezwi. Yasiyozungumzwa ndiyo hutekelezwa, yasiyotekelezwa ndiyo yanahitajika, wanaoyahitaji hawayazungumzi.

Inawezekana hajapatikana refa anayetakiwa kupuliza kipenga wakati timu mbili zinapokuwa uwanjani. Kama watu wawili wamekosana au hawaelewani, ni vyema lazima apatikane mtu wa tatu nje ya mahakama za kisheria badala ya ndani ya mahakama za majadiliano ili kusikiliza hoja za pande mbili na kuwaunganisha wawili hawa.

Zamani migogoro mingi katika jamii ilitatuliwa na wazee. Bado naamini wazee hao hawajaisha bado wapo. Iwe migogoro ya kimila, kisiasa au kiserikali wanaweza kusimama kwenye nafasi zao wakashauri kwa sababu kuishi kwingi ni kufahamu mengi. Inawezekana  makosa mengine yanatokana na kutoijua historia.

Kauli na vitendo ni mambo mbalimbali. Zinaweza  kutoka kauli nzuri sana kwa viongozi wetu juu ya umoja wetu lakini vitendo vikakinzana na kiukweli hili ni tatizo moja tulilo nalo Afrika. Tatatizo hili linatokana na utamaduni wa kufundishwa uongo tukiwa wadogo. Mara nyingi tu inatokea kutoa maelekezo kwa watoto kwamba mtu fulani akija mwambieni sipo nimetoka, wakati umelala ndani. Kwa hiyo mtoto tayari anafundishwa kusema asichoamini hata mwenyewe maana anafahamu fika upo.

Naamini kwamba siku tutakapoamua kuzitendea haki hotuba zetu na matamko mbalimbali tukayatekeleza kama tunavyoyasema kwenye majukwaa, basi tunaweza kuwa tumetengeneza jambo jema sana ambalo litabaki kwenye histoaria ya maisha yetu.

Bado tunayo nafasi ya kuwa wamoja pamoja na tofauti za kimtazamo na katika hili si lazima tufikiri sawasawa, kutofautiana ndiyo uhai wetu lakini usitumike kudhalilisha pia utamaduni wetu kama Watanzania. Kila mmoja anatakiwa kujiona kuwa anayo nafasi sawa ya kujiletea maendeleo yake binafsi na ya nchi kwa ujumla.

Haipaswi kuonekana kwamba wako wanaotakiwa kujenga nchi na wengine wabaki watazamaji. Hilo halitakuwa tofauti na ubaguzi wa aina yoyote ile kama wa rangi na kadhalika na mambo yote haya bado yanaweza kufanyika bila kutukanana na kudhalilishana japo tunayo haki ya kushauri.

0689157789

[email protected]