Kwa nini shetani anashambulia ndoa?

By Flora Wingia , Nipashe Jumapili
Published at 02:52 PM Apr 28 2024
Ndoa.
PICHA: MAKTABA
Ndoa.

KARIBU tena msomaji wangu tuendelee na vituko katika duru la ndoa. Huko nyuma nilichambua maoni na madai ya baadhi ya kinababa wakilalamikia wake zao kuwakimbia, kisa mdororo wa kiuchumi.

Yaani maisha yalipokuwa mazuri walitulia, lakini uchumi wa mwanaume ulipoyumba, baadhi ya wanawake wakabwaga manyanga.

Je, ni utashi wao? Tokea mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, Mungu alikuwa amekusudia taasisi hii ya ndoa iwe yenye ushindi na mafanikio. Inahuzunisha leo kuwa watu wengi hawaoni ushindi huo.

Maandiko ya Mungu yanasema baada ya shetani kuingilia ratiba iliyokuwa imepangwa na Mungu, historia yote ya mwanadamu ilibadilika.

“Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu. Akamwambia mwanamke, ati, hivi ndivyo alivyosema Mungu, msile matunda ya miti yote ya bustani?”

Hapa tunaona kwamba shetani hakumshambulia mwanaume moja kwa moja. Alikwenda moja kwa moja kwa mwanamke kwa sababu aligundua kuwa mwanamke alikuwa amepewa ngao ya kumlinda mwanaume. Alijua kuwa kama ngao ingetolewa mara moja, ingekuwa rahisi sana kumkamata Adamu.

Maandiko yanaonyesha kuwa baada ya mazungumzo kati ya mwanamke (Hawa) na nyoka akimsisitiza kuwa akila matunda ya mti uliokayazwa hatakufa, ndipo akaingia kwenye mtego wa shetani.

Hawa hakuishia hapo, alikwenda kumshawishi na mumewe kula lile tunda. Na hicho kikawa chanzo cha mateso makubwa ya mwanadamu. Kilichotokea wakati ule ni zaidi ya anguko la Adamu na Hawa. Na kwa tukio hilo, ndicho chanzo cha vita kali kati ya mwanadamu na shetani.

Laiti kama yule mwanamke asingekuwa mjinga kumsikiliza shetani, katu shetani asingepata nafasi ya kutushambulia hivi leo.

Shetani na mawakala zake wamekuwa wakishambulia ndoa nyingi kwani leo hii ndoa hazina amani, furaha na upendo vimetoweka kwenye familia nyingi; mafarakano na chuki vimepandwa kwenye ndoa nyingi.

Swali la kujiuliza; kwa nini shetani amepata nafasi ya kushambulia ndoa leo? Ni ulweli usiopingika kuwa yule mwovu shetani amepata nafasi ya kushambulia ndoa nyingi na kusababisha ajali mbaya kwenye ndoa kwa sababu ya mambo mbalimbali. Hapa nitaje machache.

UJINGA: Ujinga si tusi. Ujinga ni ile hali ya kutokwa na uwezo wa kufahamu jambo fulani,

Ni ile hali ya kukosa maarifa kuhusu jambo.

Mungu katika moja ya maandiko yake akasema, “Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao wanaona kiu sana.” (Isaya 5:13).

Msomaji wangu, leo ndoa nyingi zinashambuliwa kwa kukosa maarifa. Ni maarifa tu ndiyo yanaweza kukutoa kwenye mateso ya ndoa unayopitia. Na ujinga ni moja ya silaha zenye nguvu anazotumia shetani. Ukitaka shetani aendelee kukutesa na kukuharibia maisha endelea kuwa mjinga.

Leo ndoa za Wakristo wengi zinashambuliwa kwa kukosa maarifa. Hivi unajua unaweza kuwa umeokoka kabisa na ni mwombaji mzuri lakini ndoa yako ikaangamizwa na shetani?

Hebu jiulize maswali yafuatayo;-

Je, una maarifa yapi kuhusu ndoa? Je, unapokutana na changamoto kwenye ndoa unapaswa ufanye nini? Je, wakati mumeo/mkeo amebadilika ghafla na kuwa mtu mwingine unatakiwa ufanyeje?

Pale unapogundua kuwa mumeo/mkeo ameanza kuwa na mahusiano na wanawake/wanaume wengine unatakiwa ufanyeje? Je, umesoma vitabu vingapi vya kiroho vinavyohusu ndoa? Ni maarifa tu yanayoweza kukusaidia kumshinda shetani na mawakala wake.

Sababu nyingine shetani kusambulia ndoa ni watu wengi kupuuzia kanuni na misingi ya ndoa.

Ni muhimu kuzingatia kwamba kupata tu maarifa kuhusu ndoa haitoshi kumfanya shetani asikushambulie, bali kusimamia na kutendea kazi maarifa uliyo nayo.

Ukitaka uwe na ndoa yenye mafanikio na upenyo ni lazima utendee kazi kanuni na maelekezo yote yanayohusu ndoa. Kwa bahati mbaya watu wengi walioko kwenye ndoa hupuuza na kutupilia mbali kanuni na maelekezo waliyopewa siku wanafunga ndoa.

Pale unapopuuzia kusoma vitabu vilivyoandikwa na watumishi wa Mungu kuhusu ndoa na jinsi ya kufanikisha ndoa yako, utajikuta unampa shetani nafasi ya kukushambulia.

Msomaji wangu naamini umejifunza kitu. Bado tunaedelea na uchambuzi huu na wiki ijayo tutaangalia zaidi chanzo cha matatizo ya ndoa. Je, una maoni au kisa? Ujumbe mfupi

0715268581.