KATIKA ya miaka ya 1980, kuna mwanaume mmoja, alitunukiwa shahada ya uvumilivu wa mapenzi.
Waliomtunuku mwanaume huyo ni wanamuziki na mashabiki wa bendi ya DDC Mlimani Park Orchestra.
Wakati wa kumtunukia huko, wakamtungia na wimbo waliouita, 'Shahada ya Uvumilivu.'
Ilikuwa kama 'sapraizi' tu, wakati anaingia ukumbini tu, muziki waliokuwa unapigwa ukakatishwa, na kupigwa wimbo mpya ambao ulikuwa haujawahi kusikika.
Maudhui ya wimbo ule, uliwafanya wengine walie machozi, lakini mwenyewe alipousikia alishangaa na kufurahi kwa wakati mmoja.
Wimbo huo ambao ndiyo ilikuwa ni shahada tosha kwake, ulimfanya kufarijika na kupunguza kabisa maumivu aliyoyapata awali kama si kuyaondoa kabisa.
Alikuwa ni shabiki mkubwa wa bendi hiyo na alikuwa hakosi kwenye maonyesho yao, alifurahi kupita maelezo, miezi michache baadaye, Sikinde wakaenda kuurekodi wimbo huyo kwenye studio za Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) enzi hizo, sasa TBC.
Labda utajiuliza ni kitu gani kilichomtokea jamaa huyo hadi kufikia hatua ya Sikinde kumtungia wimbo?
Miaka hiyo jamaa alikuwa mfanyabiashara wa kununua korosho mikoa ya Kusini kwa wakulima na baadaye yeye kuuza kwenye miji mikubwa na hata nje ya nchi.
Msimu mmoja wa korosho akaamua kwenda na mkewe ili aone ni jinsi gani anavyofanya biashara hiyo.
Walipofika kwenye hoteli moja kubwa kwenye moja ya mikoa ya Kusini, kesho yake jamaa akamuacha mkewe ili kuwafuata wakulima vijijini kununua korosho zao, na akishakamilisha zoezi hilo arejee hotelini alikomuacha mkewe. Aliporudi hakumkuta. Tafuta huku na huku, wapi! Jamaa alichanganyikiwa.
Uliza huku na kule. Ndipo kuna watu hapo hapo hotelini walipomtonya kuwa aliondoka na mtu mwingine na walionekana kuwa na tahadhari sana.
Baadaye ikagundulika kuwa alirubuniwa na mwanaume mwingine ambaye alifika hapo, alipomuona anampenda, akamtongoza na kumpa maneno mengi matamu kama asali na laini kama sufi.
Ubuyu wote sasa ukawa mikononi mwake. Akaondoka na shehena yake ya korosho kwa ajili ya biashara, lakini hakurejea na mke. Hili lilimtesa kiasi cha kuhadithia rafiki zake wa karibu, akiwemo mtunzi wa wimbo huo, Benovilla Antony.
Msimamo wa jamaa ni kumuachia Mungu. Akaapa hatolipiza kisasi chochote, na anaendelea na maisha mengine ingawa roho ilimuuma sana.
Kisa hicho Benovilla alikichukua na kukitengenezea wimbo ambao baada ya kukamilika ulipigwa kwa mara ya kwanza akiwa anaingia ukumbini na kumshangaza sana.
Mkasa mzima wa tukio unasimuliwa na wimbo huu uliotwa 'Shahada ya Uvumilivu.'
"Habari zako tumezisikia, ewe jirani yetu Moyogani eee, tulijua toka zamani kwamba, mama Hadija ni malkia katika nyumba yako.
Hakuna kilichokuwa chini ya uwezo wako akakikosa Moyogani eee, kwa hakika mkataa pema pabaya panamwita, ooh jirani, kweli huna lawama."
Hapa Benovilla amejinasibisha kama jirani wa Moyogani, akiwa anafahamu matunzo yote ambayo jamaa anampatia mkewe, lakini ikawaje?
"Akatokea hasidi mvurugaji wa mambo, kamshawishi mkeo mama Hadija, akufanyie vituko kusudi umwache arudi kwao, baadaye aende kwa hasidi Nachingwea. Huko akaolewe kwa mkataba wa kujengewa nyumba aaa, eee uchungu wa jambo hili ni mkubwa, lakini ulivumilia."
Ni kawaida wa wanamuziki, wakipata kisa cha kweli, watapunguza baadhi ya vitu, wataongeza vingine ili mradi kuongeza ladha ya maudhui yanayokubalika kwa jamii.
"Nia yetu ni kukuasa, uendelee na uvumilivu jirani yetu, tena sote twakusubiri, Sikinde Ngoma ya Ukae, tukutunukie shahada wa uvumilivu.
Wala wewe ulipize kisasi kwa hasidi aliyemrubuni mkeo, mwache acheze na pesa, dunia itamchapa, itamchapa viboko, Moyogani eee.
Tunajua ulipatwa na uchungu kwa pande zote mbili, lakini uliheri kulala juu ya paa, kuliko ndani ya nyumba, iliyokanganyika, Moyogani ee." Huyo ndiye mwanaume pekee aliyewahi kutunukiwa shahada wa uvumilivu wa mapenzi.
Tuma meseji 0716 350534
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED