MKUTANO WA DHARURA DAR Wakuu SADC, EAC: Njia sahihi

By Jenifer Gilla , Nipashe Jumapili
Published at 11:43 AM Feb 09 2025
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza katika mkutano huo
Picha: Mtandao
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza katika mkutano huo

VIONGOZI wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamesema njia sahihi ya kumaliza mgogoro mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ni kukaa meza moja na kuzungumza na si visasi.

Wamesisitiza mazungumzo, ushirikiano na ulinzi wa maisha ya raia, viwe msingi wa hatua zote zitakazochukuliwa katika kuleta amani katika nchi hiyo.

Wakuu hao wamekutana kwa dharura jijini Dar es Salaam baada ya kundi la waasi wa M23 kuanzisha mapigano mapya mashariki mwa DRC.

Kundi hilo limeuteka Mji wa Nyabibwe ulioko katika ukingo wa Ziwa Kivu, Jimbo la Kivu Kusini nchini DRC kwa madai ya kujihami na mashambulizi ya Jeshi la Serikali ya DRC.

Akizungumza katika mkutano wa dharura jana jijini Dar es Salaam uliolenga kujadili mgogoro huo wa DRC ili  kutafuta suluhisho la kudumu na kurudisha amani katika nchi hiyo, Rais wa Kenya, William Rutto ambaye pia ni Mwenyekiti wa EAC, alisema:

"Ili kupatikana suluhu ya haraka na kudumu katika mgogoro unaoendelea mashariki kwa DRC, ni muhimu pande zinazopigana kusitisha mapigano na kuzungumza."

Alisema ili hilo litokee ni muhimu mapigano nchini Kongo yasitishwe ili kuunda mazingira yatakayowezesha mazungumzo ya kujenga na utekelezaji makubaliano ya kina ya amani.

Hivyo, Rais Ruto aliyahimiza makundi yote yenye silaha nchini DRC, wakiwamo M23, kusitisha mashambulizi kwa jeshi la DRC ili kuepuka hatua za kulipiza kisasi zitakazokwamisha juhudi kusitisha mapigano kwa haraka

 "Ni lazima tuwahimize wadau wote waachane na tofauti zao na kushiriki katika mazungumzo yenye tija kwa lengo la kupata suluhisho la kudumu kwa kushughulikia mizizi ya mgogoro huu," alisema Ruto.

Alisisitiza kujifunza kutoka kwa mchakato wa amani wa Rwanda na Nairobi na kuhimiza mtazamo wa pamoja wa kikanda katika kushughulikia mgogoro huo.

Alitoa wito kwa nchi wanachama kuongeza juhudi zao kuhakikisha kunapatikana suluhisho litakalohakikisha nchi hiyo inakuwa na amani na utulivu wa kudumu.

"Hii ni fursa ya kihistoria kwetu, kama majirani wa DRC, kuhamasisha nia yetu ya pamoja kuwa mpango mmoja wenye mshikamano, mbinu ya kugawanyika itaathiri maendeleo yetu," aliongeza.

Rais Ruto alimshukuru Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kupongeza juhudi za EAC na SADC kwa kuonesha uharaka katika kushughulikia hali mbaya ya usalama na kibinadamu nchini DRC.

Rais wa Zimbabwe na Mwenyekiti wa SADC, Emmerson Mnangagwa, alitoa wito kuwapo mpango madhubuti wa kutatua mgogoro huo, akiwasisitiza viongozi wa kikanda hatowaangusha wananchi wao.

Alisema SADC itaendelea kushiriki kikamilifu kuhakikisha suluhu inapatikana kwa njia ya amani mashariki mwa Kongo.

"Hatupaswi kuwaangusha watu wa kanda zetu. Wanatuamini sisi. SADC itaendelea kushiriki kikamilifu kuhakikisha amani inapatikana," alisema Mnangagwa.

Aliongeza kuwa hali ya machafuko mashariki mwa DRC ina athari kubwa kwa bara zima, hivyo mataifa ya Afrika yanapaswa kushikamana kama walivyofanya wakati wa harakati za ukombozi.

"Hatua zetu lazima ziwe za pamoja na ziimarishwe ili kuhakikisha tunafanikisha lengo letu kuu: amani ya kudumu kwa watu wa DRC," alisema.

Mnangagwa pia alitoa pole kwa familia za wanajeshi na walinda amani waliopoteza maisha yao katika mgogoro huo na kuwa anatambua mateso makubwa wanayopitia raia wema nchi hiyo.

Rais Samia alisisitiza Tanzania imedhamiria kusaidia juhudi za kuimarisha amani na usalama katika eneo hilo.
 "Tuna jukumu la pamoja la kushughulikia changamoto za usalama ambazo zimeathiri vibaya maisha ya raia wasio na hatia.

"Mkutano huu ni fursa ya kujitathmini na kujipanga upya katika kuhakikisha tunaleta amani na uthabiti wa kudumu," alisema.

Alitoa wito kwa pande zote zinazohusika katika mgogoro wa DRC kushiriki mazungumzo kwa nia njema na kuweka mbele maslahi ya wananchi wa Kongo.

"Lazima tushirikiane kwa dhati kutafuta suluhisho jumuishi na la kudumu ambalo litahakikisha watu wa DRC wanapata amani waliyokuwa wakiitamani kwa miongo kadhaa," alihitimisha.

Mkutano huo uliangazia haja ya jamii ya kimataifa kuunga mkono juhudi za kikanda kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji makubaliano ya amani.