MATOKEO LA NNE, KIDATO CHA PILI; Udanganyifu bado tatizo

By Waandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 12:24 PM Jan 05 2025
Mtahiniwa
Picha: Mtandao
Mtahiniwa

BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne na Kidato cha Pili Mwaka 2024, likieleza kuwa changamoto ya udanganyifu bado ipo katika baadhi ya vituo.

Kutokana na dosari hiyo, NECTA imekifungia kituo S2527 cha Shule ya Sekondari GoodWill mkoani Arusha kuwa Kituo cha Upimaji wa Mitihani ya Taifa kutokana na ilichoeleza kuwa "Mkuu wa Shule na baadhi ya walimu kudhibitisha kufanya udanganyifu kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi wao".

Katibu Mtendaji NECTA, Dk. Said Mohamed, aliyasema hayo jana mkoani Dar es Salaam wakati akitangaza matokeo ya upimaji huo uliofanyika mwezi Oktoba na Novemba mwaka jana.

Alisema kituo hicho kinafungiwa kwa mujibu wa Kifungu 4(8) cha Kanuni za Mitihani za Mwaka 2016 hadi hapo baraza litakapojiridhisha kuwa ni salama kwa uendeshaji Upimaji wa Mitihani ya Taifa.

"Kituo hiki kilijaribu kuwarubuni wasimamizi na askari polisi Oktoba 28, 2024, ikashindikana. Mkuu wa Shule hiyo akajaribu tena kuwarubuni wasimamizi wetu Oktoba 29, 2024, ikashindikana tena. 

"Hivyo, wakaamua kutumia mbinu mbadala ya kuandaa majibu kwa kuhusisha walimu wa shule hiyo wakati mtihani unaendelea na kuwapanga wanafunzi kupata majibu... (alitaja neno lenye maana ya msalani).

Dk. Mohamed alisema pamoja na kituo hicho kufungiwa, baraza litawasilisha pendekezo rasmi kwa Kamishna wa Elimu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kufutiwa usajili wake moja kwa moja.

"Kituo hiki si tu kinakosa sifa ya kuwa kituo cha mtihani, bali kinakosa sifa ya kuendelea kuwa shule. Bila shaka mzazi anapopeleka mtoto shuleni, anatarajia pamoja na elimu, apate malezi bora na maadili na si kufundishwa udanganyifu," alisema.

Katibu Mtendaji alisema bila juhudi za ziada kudhibiti jaribio hilo, wangetangaza kufuta matokeo yote ya wanafunzi wa Kidato cha Pili shuleni huko.

"Kufutiwa kituo hicho maana yake baraza halitopeleka mtihani hapo kuanzia mwaka 2025. Wito kwa wazazi, wafikirie endapo hapo ni mahali salama kwa watoto wao kuendelea kupata elimu ya sekondari," alisema.

Kuhusu hatua kwa walimu waliowezesha utoro kwa wanafunzi na kisha kufanyiwa mtihani katika mikoa ya Mwanza na Songwe, Dk. Mohamed alisema wamefungiwa kushiriki kazi zote za Baraza la Mitihani katika kipindi chote.

Alisema pamoja na hatua zilizochukuliwa na Kamati za Mikoa,  baraza litawasilisha hoja kwa mamlaka zao za ajira ili kuchukuliwa hatua za kinidhamu za utumishi wa umma, ikiwamo kutenguliwa madaraka ya ukuu wa shule, kufutwa kazi serikalini na kufunguliwa mashtaka ya jinai ya kuhujumu mitihani ya taifa.

Hata hivyo, Dk. Mohamed alisema takwimu za udanganyifu zinaonesha kupungua mfululizo kwa miaka ya karibuni.

Alisema baraza haliwezi kuwavumilia wale wanaopanga kuhujumu elimu kwa kuwa hatua kali dhidi yao zitachukuliwa.

MATOKEO YALIYOFUTWA

Katibu Mtendaji alisema katika Mtihani wa Upimaji wa Taifa wa Darasa la Nne, baraza limefuta matokeo yote ya wanafunzi 100 waliofanya udanganyifu na watano walioandika matusi kwenye skripti zao.

"Wapo wanafunzi wawili walifanya udanganyifu kwa kusaidiana ndani ya chumba cha mtihani. Wanafunzi 98 ni watoro wa muda mrefu shuleni, hivyo walimu wakuu waliwapanga wanafunzi wenzao wa darasa la tano na sita kufanya mtihani kwa maslahi yao binafsi," alisema.

Pia alisema wamefuta matokeo yote ya wanafunzi 41 waliofanya udanganyifu na watano walioandika matusi kwenye skripti zao katika Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili.

Kuhusu wanafunzi waliofeli darasa la nne na kidato cha pili, Dk. Mohamed alisema wanapata fursa ya kukariri darasa mpaka watakapopata umahiri huo.

Katika Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne, alisema jumla ya wanafunzi 1,633,279 walisajiliwa kuufanya wakiwamo wasichana 839,515 sawa na asilimia 51.40 na wavulana 793,764 sawa na asilimia 48.60.

Alisema kati ya wanafunzi waliosajiliwa, 1,530,911 walifanya upimaji, wakiwamo wasichana 797,691, sawa na asilimia 95.02 na wavulana 733,220 sawa na asilimia 92.37. Wanafunzi 102,368, sawa na asilimia 6.27 hawakufanya upimaji.

Dk. Mohamed alisema Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili, jumla ya wanafunzi 879,352 walisajiliwa kufanya upimaji huo wakiwamo wasichana 476,244 sawa na asilimia 54.16 na wavulana 403, 108 sawa na asilimia 45.84.

Alisema kati yao, 879,352 waliosajiliwa, watahiniwa wa shule walikuwa 869,743 na wa kujitegemea ni 9,609.

Alisema kati ya wanafunzi 869,743 wa shule waliosajiliwa, 797,564 sawa na asilimia 91.70 walifanya upimaji ambapo wasichana ni 437,833 sawa na asilimia 93.09 na wavulana ni 359,731 sawa na asilimia 90.07. Wanafunzi 72,179 sawa na asilimia 8.30 hawakufanya upimaji.

Alisema kati ya wanafunzi 9,609 wa kujitegemea waliosajiliwa, wanafunzi 7,527 sawa na asilimia 78.33 walifanya upimaji na 2,082 sawa na asilimia 21.67 hawakufanya upimaji.

UFAULU WA JUMLA

Dk. Mohamed alisema jumla ya wanafunzi 1,320,227 kati ya 1,530,805 wenye matokeo sawa na asilimia 86.24 wamefaulu kuendelea na Darasa la Tano mwaka 2025 kwa kupata daraja A, B, C na D.

Alisema mwaka 2023, wanafunzi waliofaulu walikuwa 1,287,934 sawa na asilimia 83.34. Hivyo kumekuwa na ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.90 kwa wanafunzi waliopata fursa ya kuendelea Darasa la Tano kulinganishwa na 2023.

Alisema kuwa kati ya wanafunzi waliofaulu kuendelea, wasichana ni 699,901 sawa na asilimia 87.75 na wavulana ni 620,326 sawa na asilimia 84.61. Takwimu zinaonesha wasichana wamefaulu zaidi kulinganishwa na wavulana.

UBORA WA UFAULU

Dk. Mohamed alisema wanafunzi wa shule waliopata Madaraja ya A-C ambayo ni ya ubora wa ufaulu ni 931,468 sawa na asimia 60.85. Mwaka 2023 walikuwa 809,379 sawa na asilimia 52.38. Hivyo ubora wa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 8.47 kulinganishwa na mwaka 2023.

“Kuna uwiano mzuri wa ubora wa ufaulu kati ya wasichana na wavulana. Wavulana waliopata madaraja A-C ni 445,673, sawa na asimia 60.79 na wasichana ni 485,795 sawa na asilimia 60.90,” alisema.

Alisema idadi ya shule katika makundi ya umahiri inaonesha kuwa kati ya shule zote 20,036, shule 12,865 sawa na asilimia 64.20 zimepata wastani wa daraja A-C, ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.75 kulinganishwa na mwaka 2023.

Alisema shule 19,839 sawa na asilimia 99.01 zimepata wastani wa daraja A-C.

Dk. Mohamed alisema ufaulu wa somo la Kiswahili ni asilimia 84.52 na English Language ni asilimia 68.86 ambapo katika somo la Kiswahili umepanda kwa asilimia 0.37 na English Language umeshuka kwa asilimia 3.68 kulinganishwa na mwaka 2023.

"Ufaulu masomo ya Sayansi ya Jamii ni mzuri, masomo ya Sayansi na Hisabati ufaulu wa somo la Sayansi na Teknolojia ni asilimia 87.87 na somo la Hisabati ni asilimia 71 ambapo  katika somo la Sayansi na Teknolojia  umeongezeka kwa asilimia 1.01 na somo la Hisabati umeongezeka kwa asilimia 17.40 kulinganishwa na 2023.

"Wasichana wamefaulu vizuri zaidi katika somo la Sayansi na Teknolojia, lakini wavulana wamekuwa bora katika somo la Hisabati," alisema.

Kwa upande wa upimaji Kitaifa Kidato cha Pili, Dk. Mohamed alisema jumla ya wanafunzi wa shule 680,574 kati ya 796,825 wenye matokeo ambao ni sawa na asilimia 85.41 wamefaulu kuendelea Kidato cha Tatu ambapo wamepata madaraja I, II, III na IV. 

"Mwaka 2023, wanafunzi waliofaulu walikuwa 592,741 sawa na asilimia 85.31. Hivyo, ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.10," alisema.

Alifafanua kuwa kati ya wanafunzi 680,574 walifaulu kuendelea na Kidato cha Tatu, wasichana ni 367,457 sawa na asilimia 83.99 na wavulana ni 313,117 sawa na asilimia 87.13. Hivyo, wavulana wamekuwa na ufaulu bora kuliko wasichana.

Alisema wanafunzi wa kujitegemea waliofaulu na kupata sifa ya kufanya mtihani Kidato cha Nne ni 4,205 sawa na asilimia 55.94.

UBORA WA UFAULU

Dk. Mohamed alisema ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata wanafunzi wa shule unaonesha waliopata madaraja I- III  ni 239,707 sawa na asilimia 30.08 mwaka 2023 walikuwa 192,633 sawa na asilimia 27.73. Hivyo ubora wa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 2.35.

Katibu Mtendaji alisema ufaulu wa somo la Historia na Geografia ni wa wastani ambapo Historia ni asilimia 56.37 na Geografia ni asilimia 58.51.

“Katika somo la Civics ufaulu umeshuka kutoka asilimia 48.27 mwaka 2023 hadi asilimia 33.24 mwaka  2024. Somo la Kiswahili na Chinese Language ni mzuri sana ambapo katika somo la Kiswahili ni asilimia 91.74 na somo la Chinese Language ni asilimia 90.82.

"Masomo ya Arabic Language na French Language yana ufaulu wa wastani ambapo ufaulu wa masomo hayo ni kati ya asilimia 51.06 hadi 69.07.

"Katika somo la English Language ufaulu umeongezeka kutoka Asilimia 68.27 mwaka 2023 hadi asilimia 74.58 mwaka 2024.

"Masomo ya Sayansi Asili, Hisabati na Teknolojia, ufaulu wa masomo ya Engineering Science, Information & Computer Studies na Home Economics ni wa wastani ambao ni kati ya asilimia 51.46 hadi asilimia 62.97," alisema.

Dk. Mohamed alisema masomo ya Biology yana ufaulu ulio chini ya wastani ambao ni kati ya asilimia 18.85 hadi 47.00.

Alisema takwimu zinaonesha kuwa, ufaulu wa masomo ya Home Economics, Physics, Chemistry na Additional Mathematics unazidi kuimarika ambapo kwa mwaka 2024 ufaulu umeongezeka kati ya asilimia 3.18 hadi 14.65 kulinganishwa na mwaka 2023.

Alisema katika somo la Biology ufaulu umeshuka kutoka asilimia 55.74 mwaka 2023 hadi asilimia 47.00 mwaka 2024.

Alisema ufaulu wa somo la Book-Keeping umeendelea kubaki kuwa wa wastani kwa asilimia 51.51 na ufaulu wa somo la Commerce umeshuka kutoka asilimia 50.28 mwaka 2023 hadi asilimia 43.77 mwaka 2024.

“Ufaulu waa somo la Fine Art, Theatre Arts na Music ni mzuri ambapo katika somo la Fine Art ni asilimia 84.16, Theatre Arts ni asilimia 71.35 na somo la Music ni asilimia 80.91 . Somo la Physical Education lina ufaulu wa chini ya wastani ambapo ni asilimia 25.24," alisema.

Dk. Mohamed alisema masomo yote ya ufundi yana ufaulu wa juu ya wastani ambapo somo lenye ufaulu wa juu ni Building Construction lenye ufaulu wa asilimia 84.79 likifuatiwa na somo la Electrical Engineering lenye ufaulu wa asilimia 83.66.

Alisema somo lenye ufaulu wa chini kabisa ni Woodword and Painting Engineering lenye ufaulu wa asilimia 59.20.

Alisema masomo ya dini yameonesha mabadiliko makubwa ya ufaulu, somo la Bible Knowledge limeongezeka ufaulu kutoka asimia 84.01 mwaka 2023 hadi asilimia 94.14 mwaka 2024 na somo la Elimu ya Dini ya Kiislamu limeongezeka ufaulu kutoka asilimia 68.32 mwaka 2023 hadi asilimia 71.41 mwaka 2024.