MAELEKEZO HAKI JINAI.... Kitanzi kwa makamanda wa polisi

By Vitus Audax , Nipashe Jumapili
Published at 08:49 AM May 26 2024
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Camillus Wambura.
Picha: Maktaba
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Camillus Wambura.

NI KITANZI kwa makamanda wa polisi mikoa. Maagizo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Camillus Wambura, kwa makamanda wa polisi mikoa yote kuanza mara moja utekelezaji kwa vitendo maelekezo yaliyotolewa kupitia Tume ya Haki Jinai yanadhihirisha hivyo.

Rekodi zinaonyesha kuwa jeshi hilo limekuwa likilalamikiwa kwa mambo mbalimbali ikiwamo baadhi ya maofisa na askari kujihusisha na vitendo vya rushwa, uporaji, kubambikia kesi raia na ukiukwaji wa sheria. Hayo ni baadhi ya mambo yanayolitia doa jeshi hilo lililopewa dhamana ya kulinda rai na mali zao.

 Katika maagizo yake aliyoyatoa juzi wakati wa uvishaji nishani maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, IGP Wambura alisema utekelezaji wa mambo hayo, utaanza kutumika kama kipimo cha utendaji kazi wao. Katika kufanya hivyo, Wambura alisema lengo la serikali ni kuliona jeshi hilo linashika nafasi ya kwanza kwa ubora duniani. 

Alisema, maelekezo ya jeshi hilo pamoja na serikali ni kuacha kufanya kazi kwa mazoea, kubadilika kiutendaji na kifikra ili kuhakikisha maofisa na askari wanafanya kazi kwa weledi na kufuata misingi ya jeshi. 

Katika taarifa na maelekezo kwa haki jinai jeshi hilo limeshindwa kufuata misingi na sheria ya kuundwa kwake, hivyo makamanda wametakiwa kushirikiana kikamilifu na ngazi nyingine kuhakikisha wanafanya mapitio ya mara kwa mara maelekezo ya Tume ya Haki Jinai na kufanyia kazi kwa vitendo. 

"Maelekezo hayo yakachambuliwe vyema na kwa kufuata maelekezo ya serikali kwa kuweka sawa mgawanyo wa kazi na kufanya kazi katika mnyororo mmoja kuanzia ngazi ya taifa hadi kituo cha kata, wote tuongee lugha moja," alisema. 

MAELEKEZO TUME HAKI JINAI

Ndani ya Jeshi la Polisi kumekuwapo malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi kuhusu vitendo vinavyochafua taswira ya chombo hicho.  

Miongoni mwa malalamiko hayo, yaliyoripotiwa katika Tume ya Haki Jinai ni pamoja na jeshi hilo kushindwa kuzuia uhalifu, matumizi ya nguvu kupita kiasi, kubambikia kesi, vitendo vya rushwa , mali za watuhumiwa kupotea vituoni na kuchelewa kufika kwenye maeneo ya  matukio.  

Hali hiyo, inasababisha wananchi kupoteza imani kwa jeshi hilo na kutokutoa ushirikiano unaotakiwa katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani. 

Kutokana na malalamiko hayo, tume ilitoa mapendekezo na maelekezo yakiwamo Jeshi la Polisi kufanyiwa tathmini ya kina itakayowezesha kuwapo maboresho makubwa na kuundwa upya ili kuondoa kasoro za kiutendaji. 

Vilevile, ilipendekezwa jeshi hilo libadilishwe kisheria, kimuundo na kifikra na kuwa Polisi Tanzania (National Police Service) ili kutoa taswira kuwa chombo cha kuwahudumia wananchi, kubadilisha mitaala ya mafunzo na mtazamo wa askari ili kutoka katika dhana ya ujeshi kwenda dhana ya kuhudumia wananchi, 

 Kadhalika, tume ilitaka liboreshe mfumo wa ndani wa kushughulikia malalamiko ya wananchi na liimarishe huduma za intelijensia ya jinai na polisi jamii kwa kuanzisha programu za kuisogeza zaidi kwenye jamii. 

Mambo mengine yaliyopendekezwa ni pamoja na Matumizi ya Amri Kuu za Jeshi la Polisi (PGO) kutokana na kubaini kuwa izmetengenezwa pasipo kuzingatia masharti na wigo wa kisheria uliopo katika kifungu cha 7(2) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi na sheria nyingine. 

Pia ilibainika kuwa miongoni mwa mambo yenye shida kubwa katika PGO ni pamoja na uchunguzi wa vifo vyenye utata, gwaride la utambuzi wa mhalifu, hivyo kutaka PGO yenye GN. Na. 351/2021 inayotumika sasa isitishe matumizi yake na PGO iliyokuwapo awali iendelee kutumika.

KAULI ZA SAMIA 

Tangu alipoingia madarakani machi 19, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan amefanya vikao na maofisa wakuu na makamanda wa polisi huku akihimiza jeshui hilo kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.  

Katika kikao cha tathmini  ya utendaji kazi kwa mwaka 2020/21, kilichofanyika Agosti 25, 2021 Oysterbay, Dar es Salaam,  Rais Samia alilitaka Jeshi la Polisi kutimiza majukumu yake ipasavyo kwa kutenda haki kwa jamii na kuepuka kutumia nguvu  kuwakandakiza wananchi.

Aidha, Februari 4, 2022 Rais Samia alikemea matukio ya mauaji ambayo yalikuwa yakiripotiwa, ambayo yalidaiwa kufanywa na baadhi ya askari polisi na kuagiza kuundwa kamati maaulum kuchunguza chanzo cha mauaji hayo.

Katika kipindi hicho, kulikuwa na taarifa za mauaji katika mikoa ya Mtwara, Mbeya, Mwanza, Moshi na Dodoma huku baadhi ya maofisa na askari wa jeshi hilo wakitajwa kuhusika. 

"Nimemwelekeza Waziri Mkuu aunde kamati nyingine iende ikafanye uchunguzi wa mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi alafu watuletee taarifaa. Lakini  wakati huo huo, nataka jeshi lijitafakari waone kinachotokea ni kinyume cha misingi ya jeshi la polisi,” alisema. 

Rais Rais Samia pia aliwataka maofisa wa polisi kuwaacha huru watu ambao wanahisi upelelezi wao hautakamilika katika kesi zao ili wakafaidi uhuru wao wakiwa nje na kama kesi haina mwelekeo, watu hao waachiwe huru lakini kwa zile kesi ambazo wana uhakika upelelezi utatimia, ziharakishwe ili watu wasisote mahabusu.

Sambamba na hilo, aliahidi mbele ya maofisa hao, wakati huo jeshi likiongozwa na IGP Simon Sirro kwamba atafanya mabadiliko. Muda mfupi baadaye, alitekeleza hilo kwa kumteua Wambura kushika nafasi hiyo huku Sirro akipelekwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe. Kabla ya uteuzi huo, Wambura alikuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).  

NISHANI ASKARI 

IGP Wambura wiki hii, amekuwa akiwavalisha nishani maofisa na askari wav yeo mbalimbali katika kanda mbalimbali huku akibainisha kuwa serikali imeendelea kutambua mchango wa jeshi hilo kwa kuboresha maslahi ya watumishi, kuongeza ajira pamoja na miundombinu. 

“Kwa hatua hii ya nishani tunazozitoa pamoja na mambo mengine, Rais Samia Suluhu Hassan ameweka alama isiyofutika katika mioyo ya askari wetu kwa ishara ya kutambua michango na kazi nzuri zinazofanywa na jeshi hili nchini, hivyo tunashukuru saana,” alisema.  

Wambura pia alisema jeshi hilo lilikuwa na ombwe kubwa la upandishwaji vyeo kwa muda mrefu lakini kwa kipindi hiki Askari wamepandishwa vyeo katika ngazi mbalimbali sambamba na utolewaji wa ajira ambazo zimekuwa zikitolewa kila mara lengo likiwa ni kuongeza nguvu kazi katika jeshi hilo. 

Vilevile, alisema maboresho makubwa ya miundombinu mbinu ya jeshi yakiwamo majengo pamoja na ununuzi wa vitendea kazi yakiwemo magari yameendelea kufanyika hivyo kutufanya sisi kama jeshi kuwa na deni kubwa kwa serikali. 

Aidha alisema jeshi hilo limedhamilia kuhakikisha linazidi kiimarisha amani na kuwa suala la uvunjifu wa amani haina nafasi katika taifa, hivyo kuahidi kufnya kazi kwa moyo na ushirikiano kutokana na kupatiwa rasilimali za kutosha. 

Akizungumza kwa niaba ya askari waliopokea nishani, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna (DCP) Wilibroad Mutafungwa, alisema nishani hizo zitawaongezea morali, nidhamu na uwajibikaji katika utendaji kazi na kuahidi kuendelea kusimamia na kutekeleza majukumu kwa weledi na misingi ya jeshi hilo. 

"Tunaomba hatua hii iwe endelevu kwa kuendelea kutoa nishani hizi kutambua michango, majukumu na uwezo wa askari, hali inayoongeza chachu katika utumishi," alisema DCP Mutafungwa.