Yanga kumng'oa kiungo wa Singida BS usajili dirisha dogo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 01:42 PM Dec 09 2024
Kelvin Nashon.
Picha: Mtandao
Kelvin Nashon.

WAKATI zimebaki siku sita tu kabla ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa, Klabu ya Yanga ipo kwenye hatua za mwisho kupata saini ya kiungo mkabaji matata wa Singida Black Stars, Kelvin Nashon.

Habari kutoka ndani ya Yanga, zinasema kuwa mchezaji huyo ana asilimia kubwa ya kujiunga na Yanga kwa mkataba wa mkopo wa miezi sita kutibu eneo hilo ambalo kwa sasa linaonekana kulegalega.

Mtoa taarifa huyo amesema Nashon, anakwenda kusaidiana na Khalid Aucho ambaye kwa sasa amekuwa akiandamwa na majeraha ya mara kwa mara, akicheza pia mechi nyingi ambazo zimeonekana kuathiri kiwango chake.

"Nadhani Nashon anaweza kutusaidia kwa sasa, tutamchukua kwa mkataba wa muda mfupi wa miezi sita, kama akifanya vizuri, basi mwishoni mwa msimu tutakaa na Singida Black Stars kwa ajili ya kufanya biashara nyingine, kwani tutamsajili kwa miaka miwili.

"Angalia hivi sasa kocha wetu, Sead Ramovic, ameamua kumchezesha Duke Abuya namba sita, wakati ni winga na kiungo mshambuliaji, kwa sababu tuna mapungufu kidogo kwenye eneo hilo, tunachohitaji ni ubora na Nashon timu zote alizoenda ameonekana yupo imara na kiwango chake hakishuki," alisema mtoa taarifa huyo.

Mbali na Aucho, raia huyo wa Kenya, Abuya, Yanga ina kiungo mkabaji mwingine, Aziz Andambwile, aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu akitokea Fountain Gate, lakini amekuwa hapati nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho.

Viungo wengine wawili, Mudathir Yahaya na Salum Aboubakar, wanaonekana kutumiwa zaidi kama namba nane, wakipanda kwenda kusaidia mashambulizi na kurudi kusaidia viungo wakabaji.

Habari zinasema huenda Yanga ikasajili wachezaji kadhaa na kuwaondoa wengi kipindi hiki cha dirisha dogo kutokana na mapungufu yaliyoonekana tangu mwanzo mwa msimu.

Viongozi wengi wa Yanga kwa sasa wapo nchini Algeria ambapo juzi timu yao ilicheza mechi ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kundi A dhidi ya MC Alger, na kuchapwa mabao 2-0.