WAKATI inatarajia kuwakaribisha KMC FC katika mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, tayari Azam imeanza mikakati ya kuhakikisha inapata ushindi dhidi ya Simba.
Wekundu wa Msimbazi atakuwa mwenyeji wa mechi hiyo itakayochezwa Februari 24, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Septemba 26, mwaka jana wenyeji Azam walikubali kichapo cha mabao 2-0.
Akizungumza jijini jana, Kocha Mkuu wa Azam FC, Rachid Taoussi, alisema kwa sasa akili zao ni mchezo wa leo usiku dhidi ya KMC lakini amekiri anaufikiria pia mchezo dhidi ya Simba.
“Hatuwezi kuacha kuufikiria mchezo dhidi ya Simba, ni mchezo mkubwa, tulipoteza katika mchezo wa kwanza, tuna nafasi ya kulipiza kisasi, hatutakubali kuona tunapoteza mchezo wa pili kwa Simba, lakini kwa sasa akili zetu zipo kwenye michezo iliyopo mbele kabla ya mchezo huo,” alisema Taoussi.
Naye kiungo wa timu hiyo, Feisal Salum 'Fei Toto' amesema mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zinazidi kuwa na ushindani kwa sababu wameingia hatua ya lala salama.
Fei Toto, alisema wakati huu kila timu inashuka uwanjani ikiwa na malengo yake na hivyo hakuna mchezo rahisi au mwepesi.
"Hakuna mechi inayotabirika, ni muda wa mapambano kwa kila timu, sisi kwetu wachezaji tumejipanga vizuri kuhakikisha tunashinda kila mechi," alisema kiungo huyo kutoka Zanzibar.
Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu, Yanga watacheza michezo minne kabla ya kukutana na watani zao Simba, wataanza leo dhidi ya KMC, kabla ya Jumapili ijayo kuwakaribisha Pamba Jiji kutoka jijini, Mwanza.
Baada ya hapo Azam watawakaribisha Mashujaa FC ya Kigoma mechi itakayochezwa Februari 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex kabla ya kuifuata Coastal Union siku nne baadaye halafu ikitarajiwa kurejea Dar es Salaam kuisubiri Simba.
Yanga ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara huku vinara wa ligi hiyo ni Simba yenye pointi 43.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED