Simba baba lao CAF

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:35 AM Jan 20 2025
   Simba baba lao CAF
Picha: Simba
Simba baba lao CAF

MABAO mawili ya kipindi cha pili, yaliyofungwa na Kibu Denis na Leonel Ateba, jana kwenye Uwanja wa Banjamin Mkapa, Dar es salaam, yaliiwezesha Simba kuondoka na ushindi wa 2-0 dhidi ya CS Constantine ya Algeria na kuongoza Kundi A la Kombe la Shirikisho Afrika.

Ateba raia wa Cameroon, aliweka rekodi ya kufunga bao moja katika mechi mbili mfululizo, kwani katika mchezo uliopita dhidi ya Bravos do Maquis, uliochezwa nchini Angola, Januari 12, mwaka huu, alipachika bao la kusawazisha, lililoiwezesha Simba kutoka sare ya bao 1-1 na kufuzu hatua ya robo fainali.

Ushindi huo umeiwezesha Simba kumaliza mechi zake sita za kundi hilo ikiwa kinara kwa kufikisha pointi 13, ikishinda michezo minne, sare moja, ikipoteza mmoja, ikifunga mabao manane na kufungwa manne.

Kipigo hicho kimeifanya CS Constantine kumaliza nafasi ya pili, ikikusanya pointi 12 nyuma ya Simba, ambapo katika michezo yake sita, imeshinda minne, imepoteza miwili na haijatoa sare yoyote.

Katika mechi ya jana timu zote mbili zilikuwa tayari zimefuzu, badala yake zilikuwa zinatafuta kinara wa kundi.

Iwapo wachezaji wake wangekuwa makini, Simba ingeweza kuondoka na idadi kubwa ya mabao kutokana na kupata nafasi nyingi ambazo walishindwa kuzitumia.

Mechi ilianza taratibu, Simba wakimiliki kwa kiasi kikubwa huku wapinzani wao wakijazana nyuma kwani walihitaji sare tu ili kuweza kuongoza kundi.

Kutokana na hali hiyo, wachezaji wa Simba walikuwa wakipigiana pasi fupi fupi, kati na pembeni kwa lengo la kutaka kuwavuta CS Constantine, lakini walionekana wako makini katika mpango mkakati wao huo.

Kukosekana kwa nafasi kulimfanya Jean Ahoua kuamua kuachia shuti kali la mbali dakika ya 12, lakini mpira ukapaa juu ya lango.

Kiungo mshambuliaji huyo alipata nafasi nzuri dakika nne baadaye kutoka kwa Mpanzu, akiwa anatazamana na kipa, lakini alipiga shuti kali akiwa karibu na lango lililopanguliwa na mlinda mlango Zacharia Bouhalfaya.

Ahoua alishindwa kuitendea haki faulo aliyofanyiwa Kibu Denis dakika ya 21, badala yake akapaisha mpira juu.

CS Constantine ilifanya shambulio kwa mara ya kwanza kwenye lango la Simba dakika ya 25, ambalo lilikuwa la hatari, kwani Brahim Dib, aliwatoroka mabeki na kubaki na kipa, Moussa Camara, lakini wakati ameinua mguu wake wa kushoto kutaka kuukwamisha wavuni, Shomari Kapombe alimuwahi na kuutoa nje, ikawa kona.

Dakika ya 29, nahodha Mohamed Hussein 'Tshabalala' alitaka kufanya kile alichokifanya kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Algeria, Desemba 8, mwaka jana, alipopiga krosi iliyokwenda moja kwa moja hadi wavuni, lakini jana mpira wake uligonga mwamba wa juu na kutoka nje.

Ahoua aliikosesha Simba bao dakika ya 37, baada ya kazi kubwa ya Ateba kuwatoka mabeki wa timu pinzani kwenye wingi ya kulia, kabla ya kupiga krosi ya nyuma, ambayo alipaisha mpira huu akiwa kwenye nafasi nzuri.

Fabrice Ngoma naye aliunganisha vibaya faulo ya Ahoa, dakika moja kabla ya mapumziko, mpira pia ukapaa juu ya lango.

Kipindi cha pili Simba ilizidisha mashambulizi na kufanikiwa kupata bao la kwanza lililowekwa wavuni na Kibu dakika ya 61, kwa shuti kali nje ya eneo la hatari, baada ya wachezaji wa Simba kufanya msako mkali, Elie Mpanzu akamweka mfungaji ambaye alipiga shuti la kushtukiza lililomwacha kipa Bouhalfaya akiruka bila mafanikio.

Wenyeji walizidisha mashambulizi na kufanikiwa kupachika bao la pili lililotiwa ndani ya kamba na Ateba.

Kipa Camara aliuanzisha kwa Fondoh Che Malone, ambaye aliukokota kwa umbali mrefu kwenye wingi ya kulia, kabla ya kumpa Kapombe aliyekuwa ameingia ndani kidogo, ambaye alipiga nusu krosi, iliyomkuta mfungaji akiwa katikati ya mabeki wawili na kipa wao. Aliwazidi nguvu na ujanja kabla ya kuujaza wavuni.

Kwa matokeo hayo, Simba ambayo inasubiri droo ya michuano hiyo ili kujua itacheza na nani, itaanzisha ugenini na kumalizia nyumbani kitu ambacho wanachama, mashabiki, viongozi na Kocha Mkuu, Fadlu Davids walikuwa wanakihitaji.