Coastal Union yapania kupindua meza kibabe

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 06:37 AM Aug 25 2024
KOCHA msaidizi wa klabu ya Coastal Union, Ngawina Ngawina.
Picha: Mtandao
KOCHA msaidizi wa klabu ya Coastal Union, Ngawina Ngawina.

KOCHA msaidizi wa klabu ya Coastal Union, Ngawina Ngawina, amesema wana kila sababu ya kupindua meza kwenye mchezo wao wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravo do Maquiz ya Angola kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa wiki iliyopita uwanja wa Nacional da Tundwa, Angola, Coastal walikubali kipigo cha mabao 3-0 hivyo ili isonge mbele inahitaji ushindi wa angalau wa mabao 4-0.

"Matokeo yaliyopita yamepita, kwa sasa tunajipanga kwa ajili ya mchezo wetu ujao tukiwa na lengo la kupindua matokeo tuliyoyapata ugenini," alisema Ngawina. 

Alisema baada ya kurudi nchini aliwapa mapumziko mafupi wachezaji wake na baadae kuanza kufanyia kazi makosa waliyoyafanya kwenye mchezo uliopita ili yasijirudie katika mchezo wa leo. 

Alisema anatarajia kufanya mabadiliko kidogo kwenye kikosi kilichoanza kwenye mchezo uliopita.

"Nashukuru mpaka sasa hakuna mchezaji majeruhi, tumefanyia kazi makosa tuliyoyaona kwenye mchezo uliopita, tutapambana kuanzia dakika ya kwanza mpaka ya mwisho kuhakikisha tunapata matokeo mazuri," alisema Ngawina.

Aidha, aliwataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi katika mchezo huo ili kuwatia moyo wachezaji wao.

 Kwa upande wake mchezaji wa timu hiyo, Jackson Shiga ambaye alizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, alisema malengo yao ni kupindua matokeo waliyoyapata Angola. 

"Tumejipanga vizuri kuhakikisha tunabadilisha matokeo ambayo tuliyapata kwenye mchezo wa awali licha ya Kocha wetu Mkuu kutokuwepo, sisi haijatuathiri kwa sababu tumebaki na benchi la ufundi ambalo linafanya kazi na sisi kwa ushirikiano mkubwa, alisema Shiga. 

Wakati huo huo, Msemaji wa timu hiyo Abbas El Sabri, alitoa sababu ambazo zimeufanya Uongozi wa Klabu hiyo kumuondoa aliyekuwa Kocha Mkuu, David Ouma.

Sabri, alisema sababu ambazo zimeufanya uongozi huo kumuondoa Kocha huyo ni kutoridhishwa na matokeo ambayo waliyapata kwenye mchezo wao wa awali na kwa sasa benchi la ufundi litakuwa chini ya Kocha Msaidizi Ngawina Ngawina atakayesaidiana na Joseph Lazaro. 

"Uongozi umefanya maamuzi hayo baada ya kutoridhishwa na kile ambacho kilitokea tulipokuwa Angola, leo (jana),  Kocha Ouma ameripoti ofisini ili wajadiliane na viongozi kwa ajili ya kupewa majukumu mengine baada ya muda mfupi tutawatangazia kile kinachoendelea juu yake," alisema El Sabri.