Wanasoka mashabiki wa mpira wa kikapu na wakali wa mavazi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:04 PM Dec 09 2024
Wanasoka mashabiki wa mpira   wa kikapu na wakali wa mavazi
Picha:Mtandao
Wanasoka mashabiki wa mpira wa kikapu na wakali wa mavazi

WAKATI michezo miwili mikubwa zaidi duniani inapogongana; soka na mpira wa kikapu, kuna kuwa na mitindo ya kuvutia ya mavazi yakioneshwa, iwe nje ya uwanja au ndani.

Nyota wa Manchester United, Marcus Rashford alizua tafrani kwenye mitandao ya kijamii Novemba aliposafiri kwa ndege binafsi hadi Maddison Square Garden nchini Marekani kuishangilia timu ya New York Knicks ikicheza na Brooklyn Nets kwenye Ligi ya NBA.

Aliwasili akiwa amevalia koti la kifahari la Louis Vuitton kabla ya kukaa kwenye viti ili kuishuhudia timu ya Knicks ikitawala kwa ushindi dhidi ya wapinzani wao.

Ingawa wengine hawakukubaliana na chaguo la Rashford la mapumziko ya mechi za kimataifa, mapenzi yake ya wazi ya mpira wa kikapu yanamfanya ajiunge na orodha ndefu ya wachezaji wa mpira wa miguu ambao ni mashabiki wakubwa wa mchezo huo.

Vinicius Junior, Jude Bellingham na Neymar ni miongoni mwa baadhi ya mashabiki wanaovaa kimaridadi zaidi wakiwa uwanjani kushangilia mpira wa kikapu. 

5. Jude Bellingham

Jude Bellingham kwa sasa amefikia kwenye ubora wake na ukamwezesha kujiunga na Real Madrid msimu wa majira ya joto wa 2023.

Ukiachana na kujiunga kwake kule 'Los Blancos', lakini Bellingham sasa amejiimarisha kama shabiki wa mpira wa kikapu. 

Na bila shaka, fursa ya kuhudhuria mojawapo ya michezo hii pia inampa mchezaji huyo wa Kimataifa wa England nafasi ya kuonesha baadhi ya mavazi yake bora na kuvutia.

Alionekana akiwa amevalia sweta la bluu la hoodie na jinsi nyeusi Oktoba akiwa uwanjani Marekani.

Kwa kifupi Bellingham anajua jinsi ya kuvaa na anakwenda sambamba na fasheni. 

4. Aurelien Tchouameni

Kiungo wa kati wa Real Madrid, Aurelien Tchouameni ni mmoja wa wanamitindo bora kabisa sawa na wachezaji wenzake wachache.

Nyota huyo wa Ufaransa mara kwa mara amekuwa kwenye kurasa za mitindo akiwa nje ya soka. Hata kule Real Madrid anajulikana kwa ustadi wa kutupia mavazi ya kisasa.

Tchouameni anajulikana kwa mtindo wake wa mavazi ya mitaani, na vazi linalojumuisha shati la Migos na suruali ya tracksuit aina ya Essentials inaonesha ustadi wake binafsi.

Mpira wa kikapu ndio furaha yake kuu kushabikia kuliko hata wa miguu. 

3. Marcus Rashford

Nyota huyu wa Man Utd alikuwa tayari amepata nafasi yake miongoni mwa wachezaji wanaovalia vizuri zaidi kwenye soka, lakini kwa hakika amejiimarisha baada ya kusogea hadi Maddison Square Garden akiwa amevalia vazi la mbunifu Louis Vuitton.

Chini ya nguo zake za kifahari, Rashford alivalia koti, akiunganisha cheni za rangi ya fedha. Pete za Chrome Hearts zilimalizia mtindo huu bora wa kuvutia macho ya mashabiki kila mahali.

Baadaye alifanikiwa kuchukua jezi ya Knicks kutoka kwa mchezaji wa kikapu, Jalen Brunson. 

2. Vincius Junior

Iwe Ligi ya Ulaya au NBA, Vinicius Junior karibu kila wakati utamkuta amekaa siti za mbele kwenye baadhi ya mechi za kusisimua zaidi za mpira wa kikapu.

Vinicius, ambaye inajulikana kuwa ni shabiki mkubwa wa LeBron James, hata alibadilishana jezi na nguli huyo wa Los Angeles Lakers Krismasi iliyopita. 

Kwa kawaida, nyota huyo wa Real Madrid kila mara hujitokeza kwa mavazi ya mtindo wa aina yake.

Chapa za hadhi ya juu, cheni kubwa ni miongoni mwa staili anazozipenda Vinicius.

Kwa hakika Vinicius angekuwa nyota wa NBA katika maisha mengine kama si mpira wa miguu. 

1. Neymar

Neymar si tu shabiki mkubwa wa mpira wa kikapu, lakini pia ni mzuri katika kucheza, kwa mujibu wa nyota wa NBA All-Star mara sita, Jimmy Butler.

Unaweza kuchukua neno lake kwa hilo, lakini kilichodhahiri ni mtindo wazi wa mavazi kwa Mbrazili huyo ambao mara nyingi huoneshwa akiwa jukwaani.

Nyota huyo wa zamani wa NBA All-Star amehudhuria mechi nyingi zaidi za NBA kwa timu ya Los Angeles Lakers.

Na hata timu hiyo humtaja Neymar kama mmoja wa mashabiki wake muhimu.

Mavazi yake daima ni pamoja na cheni nyingi shingoni na mikononi na pete nyembamba vidoleni.