Vijue viwanja 10 vya Euro

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:58 AM Jun 17 2024
Olympia stadium.
Picha: Mtandao
Olympia stadium.

UJERUMANI i ni mwenyeji wa Kombe la Mataifa ya Ulaya 2024 (Euro 2024), ikiwa ni miaka 18 imepita tangu kuandaa Kombe la Dunia, ambalo Italia iliibuka mabingwa.

Fainali za Kombe la Mataifa ya Ulaya zitafanyika msimu wa majira ya joto kati ya Juni 14 na Julai 14 katika viwanja 10 katika miji 10 ya Ujerumani. 

Viwanja tisa kati ya 19 vilitumika katika Kombe la Dunia la 2006, isipokuwa Dusseldorf Arena.

Ni muhimu kukumbuka kuwa jiji la Munich ni mwenyeji kwa mara ya pili mfululizo, baada ya kuwa miongoni mwa majiji 11 kuwa mwenyeji wa mashindano hayo katika msimu wa joto wa 2021.

Olympia stadium, watazamaji 71,000

Ni uwanja ambao mechi za timu ya Hertha Berlin (ambayo kwa sasa inashiriki ligi ya daraja la pili), ulikuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya 1936, fainali ya Kombe la Dunia ya 2006 na fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2015, na umekuwa mwenyeji wa fainali ya Kombe la Ujerumani kila mwaka tangu 1985.

Ni uwanja wenye uwezo wa kubeba watazamaji 71,000 katika jiji la Berlin, utakuwa mwenyeji wa fainali ya Kombe la mataifa ya Ulaya 2024 mnamo Julai 14.

Ulifunguliwa Agosti 1936 wakati wa utawala wa Wanazi na ukakarabatiwa 2000 na 2004 ambao kwa sasa ndio mji mkuu wa Ujerumani baada ya kuunganishwa 1990, ni moja ya miji inayovutia.

Jiji hilo linalovutia watalii, limejaa historia na utamaduni, kama vile lango la Brandenburg na mnara wa televisheni wenye urefu wa mita 368.

Allianz Arena, watazamaji 66,000

Uwanja huo ulijengwa na Bayern Munich na timu ya Munich 1860, ulifunguliwa mwaka 2005, kabla ya Bayern kuchukua umiliki kamili.

Ulikuwa mwenyeji wa ufunguzi wa Kombe la Dunia la 2006 na fainali ya Ligi ya Mabingwa ya 2012, wakati Chelsea ilipowafunga wenyeji Bayern Munich kwa mikwaju ya penalti. 

Pia mechi za Kombe la Ulaya la 2020 katika msimu wa joto wa 2021 zilichezwa.

Ndio uwanja wa mechi ya ufunguzi kati ya Ujerumani na Scotland Juni 14 na moja ya mechi mbili za nusu fainali.

Munich ni nyumbani kwa watu milioni 1.6. Ni jiji la tatu kwa ukubwa nchini Ujerumani, eneo lililojaa historia, majumba, bustani na kitovu cha unywaji bia.

Signal Iduna Park, watazamaji 62,000

Uwanja wa timu ya Borussia Dortmund ni mojawapo ya viwanja maarufu duniani kutokana na ukuta wa njano wa mashabiki. Ulifunguliwa mwaka 1974 na ukafanyiwa ukarabati 2003.

Umetumika kwenye mechi muhimu, ikiwa ni pamoja na Fainali ya Kombe la UEFA ya 2001 kati ya Liverpool na Alaves ya Hispania.

Utatumika kucheza moja ya mechi mbili za nusu fainali katika Kombe la Ulaya la 2024.

Dortmund ni kitovu cha utamaduni wa eneo la Ruhr. Eneo hilo lilikuwa maarufu miaka 50 iliyopita kwa makaa ya mawe, chuma na bia, lakini kwa sasa ni maarufu kwa teknolojia.

MHP Arena, watazamaji 51,000

Uwanja huo umekarabatiwa na kuwa wa kisasa zaidi tangu kujengwa kwake 1933. Ulitumika katika Kombe la Dunia la 1974 na 2006, Kombe la Ulaya la 1988 na fainali ya Kombe la Ligi ya Mabingwa 1959 na 1988, pamoja na Riadha ya Dunia ya 1993.

Upo katika mji wa Stuttgart, ni mojawapo ya miji muhimu ya viwanda na makao makuu ya watengenezaji magari Mercedes na Porsche.

Volkspark stadium, watazamaji 49,000

Uwanja huo ulifunguliwa kwa mara ya kwanza mwaka1953, ukafanyiwa ukarabati mwaka 2000, na kuandaa mechi za Kombe la Ulaya la 1988 na Kombe la Dunia la 1974 na 2006.

Volksparkstadion upo katika mji wa Hamburg, mji wenye bandari kubwa ya kimataifa, historia tajiri ya kitamaduni, usanifu mzuri majengo na maisha ya usiku ambayo huwa kivutio kwa watalii wengi.

Mercur Spiel Arena, watazamaji 47,000

Unamilikiwa na timu ya Fortuna Düsseldorf, ambayo ilishiriki mara ya mwisho ligi kuu katika msimu wa 2019/2020.

Uwanja huo, ambao zamani ulijulikana kama Reheinstaedon, ulikuwa mwenyeji wa mechi za hatua ya makundi za Kombe la Ulaya la 1988.

Dusseldorf, mji mkuu wa jimbo la Rhine-Westphalia Kaskazini, mji huo una wakazi 650,000. Rhine-Westphalia ni jimbo lenye watu wengi zaidi nchini Ujerumani.

Rhein Energie Stadium, watazamaji 43,000

Uwanja wa klabu ya Cologne, ilishuka daraja hadi daraja la pili, ulikarabatiwa kwa ajili ya maandalizi ya Kombe la Dunia 2006, baada ya kufunguliwa mwaka 1923 na kufanyiwa ukarabati wa awamu ya kwanza mwaka 1975.

Ulikuwa mwenyeji wa mechi za Kombe la Ulaya 1988, Kombe la Shirikisho 2005 na Kombe la Dunia la 2006.

Tangu 2010, hutumika kwa fainali ya Kombe la Wanawake la Ujerumani, pamoja na mechi za mpira wa magongo na matamasha.

Cologne nyumbani kwa zaidi ya watu milioni moja. Ni nyumbani kwa maeneo muhimu zaidi ya watalii nchini Ujerumani kama Kanisa Kuu la St. Peter, urithi wa dunia wa UNESCO.

Deutsche Bank Park, watazamaji 47,000

Uwanja wa timu ya Eintracht Frankfurt ulifunguliwa Mei 1925. Ulikuwa mwenyeji wa mechi za Kombe la Dunia la 1974, ikijumuisha ufunguzi, Kombe la Ulaya la 1988, Kombe la Shirikisho la 2005 na Kombe la Dunia la 2006.

Frankfurt ni eneo la kimataifa la fedha na biashara, mji huo uko kwenye kingo za mto Main. Ni jiji la tano kwa ukubwa nchini Ujerumani na maghorofa yake ya kipekee limepewa jina la utani "Manhattan.”

Red Bull, watazamaji 40,000

Ni uwanja wa kisasa wenye paa la kisasa ambalo lilifunguliwa mwaka 2004. Ni uwanja pekee utakao chezewa kombe la Ulaya katika eneo la iliyokuwa Ujerumani Mashariki.

Ulitumika katika mechi za Kombe la Dunia la 2006. Ni uwanja wa klabu mpya ya RB Leipzig tangu 2010.

Mji wa Leipzig umejaa historia na ndipo alipoishi mwanamuziki Johann Bach siku za nyuma. Mji huo ulishuhudia maandamano ya amani mwaka 1989 huku Ujerumani ikijiandaa kuunganisha sehemu hizo mbili.

Veltins, watazamaji 50,000

Uwanja huo ulifunguliwa mwaka 2001 na ni nyumbani kwa timu ya Schalke FC, bingwa mara saba wa Ujerumani na kwa sasa inashiriki ligi ya daraja la pili.

Una paa linaloweza kufunguliwa na kufungwa. Uwanja huo uliandaa fainali ya Ligi ya Mabingwa ya 2004 na robo fainali ya Kombe la Dunia la 2006.

Upo katika jiji la Gelsenkirchen, lililokuwa maarufu kwa makaa ya mawe na chuma, lakini siku hizi ni kijani kibichi, sinema, safari za boti, na viwanda vya kale.