Elimu kuhusu VVU/Ukimwi kwa wasichana ipewe kipaumbele

By Maria Seme ,, Halfani Chusi , Nipashe
Published at 10:51 AM Jun 26 2024
Wasichana wapewe kipaumbele elimu ya UKIMWI.
Picha: Maktaba
Wasichana wapewe kipaumbele elimu ya UKIMWI.

TAKWIMU za Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) zinaonesha wasichana wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 24 ndiyo kundi hatarishi zaidi kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Kulinda kundi hilo, Ofisa Miradi wa Shirika la Msichana Initiatives, Rosemary Richard ameshauri serikali na wadau kuongeza wigo wa kuelimisha jamii hususani kwa wasichana wadogo ili wajilinde dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo.

Mkoani Dar es Salaam, Rosemary ametoa rai hiyo alipowakutanisha wanaharakati na wasichana viongozi kutoka mikoa minne kutafakari maendeleo ya harakati za kifeminia Afrika na duniani kwa ujumla.

Rosemary amesema kupitia mradi wao wa 'Sauti Yetu Nguvu Yetu', unaokutanisha wasichana mbalimbali kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja katika kupambana na ukatili wa kijinsia na kupeana elimu ya kujikinga na VVU, wamebaini wengi hawana elimu ya kutosha kujikinga na maradhi hayo.

Amesema mradi huo unatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Dodoma (Kongwa) na Tabora, ukilenga kupata wafadhili watakaowezesha kuifikia mikoa mingine kutengeneza wasichana watakaobeba ajenda ya kuzuia ukatili wa kijinsia, kutetea usawa na kupinga mifumo dume.

“Siku chache zilizopita tulisikia wasichana wadogo ndio wanaongoza kwa maambukizi ya VVU. Katika kupambana na hili, pia tumeamua kuwapa elimu wasichana viongozi watakaoweza kuelimisha na wengine katika kujilinda na madhila hayo," amesema.

Amesema imani potofu kwa baadhi wanaowafikia - kuamini wanataka kubadilisha mila na desturi zao, ni miongoni mwa vikwazo vinavyowakabili katika kutekeleza mradi huo.

"Tunapowafikia mtaani, wengine tunaonekana kama tunapotosha jamii na wengine wanaamini tunaharibu mila na desturi zao, wakati lengo letu ni kupambania haki na usawa katika jamii," amesema.

Msichana Kiongozi ambaye ni mnufaika wa mradi huo kutoka Bagamoyo, mkoani Pwani, Mariam Rajabu, amesema elimu aliyopata kupitia mradi huo imemwezesha kusimamia na kuwatetea wasichana wengine kuhusiana na mila potofu na ukatili wa kijinsia.

Amesema kuwa wakati anaingia katika mradi huo, alikuwa hajui hatua za kuchukua kuokoa wasichana wengine, lakini hivi sasa ameshaokoa zaidi ya wanne.

Amepongeza uamuzi wa shirika kuwakutanisha na wanaharakati nguli katika semina hiyo. Anaamini itawasaidia kupata uzoefu katika kuendeleza jukumu lao la kutetea usawa wa kijinsia.

Msichana Kiongozi kutoka Tabora aliyenufaika na mradi huo, Joyce Agustino amesema mradi huo umemfanya awe imara na kuwa ufahamu mkubwa kuhusu vitu mbalimbali, ikiwamo uchechemuzi, ufeminia na kupingana na mifumo dume.

Amesema wanachofanya katika jamii ni pamoja na kuunganisha wasichana kutoka maeneo mbalimbali na kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili.

Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), mmoja wa mwanaharakati, amesema amefurahi kushiriki semina hiyo, akiamini ni fursa kwake kurithisha wasichana hao uzoefu wake.

"Semina hii itazaa matunda. Kwa mfano, mimi katika shirika langu tunapinga rushwa ya ngono. Hivyo, ninapojengea uwezo wasichana, wakaelewa namna bora ya kupambana na rushwa ya ngono, watakuwa na uelewa na baadaye tutapata viongozi wasichana wasio na doa." amesema Janeth.

Kwa mujibu wa TACAIDS, maambukizi mpya kwa watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 15 yamepungua kwa asilimia 16.7 kutoka 72,000 (THIS 2016/17) hadi 60,000 (THIS 2022/23). 

Hata hivyo, maambukizi mapya ya VVU yameongezeka maradufu katika kipindi tajwa kwa wasichana wenye umri wa miaka 15-24.