Nyota wa5 usajili dirisha dogo walioanza kulipa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:40 AM Feb 10 2025
Elie Mpanzu, mmoja wa wachezaji 50, walioingizwa kwenye dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15 mwaka huu, akisajiliwa na klabu ya Simba. Taratibu ameanza kuwa gumzo kwa mashabiki wa soka nchini kutokana na aina yake ya uchezaji wa kasi
Picha: Mtandao
Elie Mpanzu, mmoja wa wachezaji 50, walioingizwa kwenye dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15 mwaka huu, akisajiliwa na klabu ya Simba. Taratibu ameanza kuwa gumzo kwa mashabiki wa soka nchini kutokana na aina yake ya uchezaji wa kasi

MZUNGUKO wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara umeanza, huku jumla ya wachezaji 50 wakiwa wamesajiliwa kipindi cha dirisha dogo la Januari.

Wakati dirisha dogo la usajili likiingiza idadi hiyo ya wachezaji, jumla ya wachezaji 36 wamehamishwa kutoka klabu zao kwenda zingine za hapa nchini.

Vyanzo mbalimbali vya taarifa za uhamisho, vinasema zimetumika kiasi cha Dola milioni 1.98 kwenye usajili wote wa mwezi Januari kwa Ligi Kuu Bara.

Zinasema kiwango cha idadi ya wachezaji wapya waliosajiliwa kipindi hiki kimepungua kwa asilimia 16.7.

Pamoja na changamoto mbalimbali ya vibali vya kuishi, kazi, ili kupata leseni, tayari baadhi ya wachezaji wameshaanza kuzichezea klabu zao mpya walizojiunga nazo.

Baadhi yao kwa muda mfupi tu wameshaanza kuonesha kile kilichowaleta kwenye timu hizo, kwani wameanza kuonesha uwezo ambao klabu hizo zilifanya wawasajili. Hawa ni baadhi ya wachezaji ambao wamesajiliwa dirisha dogo na wameanza kwa moto...

1# Elie Mpanzu - Simba

Ni mchezaji ambaye Simba walimpa mkataba mapema kabla hata ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili.

Awali, ilikuwa asajiliwe mwanzoni mwa msimu, lakini akatimkia nchini Ubelgiji kwenye klabu ya K.R.C. Genk kwa ajili ya majaribio ambayo hayakufaulu. Raia huyo wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo aliyekuwa akiichezea Klabu ya AS Vita ya nchini kwao, aliamua kuingia mkataba na Simba akisubiri dirisha dogo na kukaa kwa muda mrefu nchini.

Alianza kuonekana katika michuano ya kimataifa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, na sasa mechi za Ligi Kuu.

Amekuwa mhimili mkubwa kwenye kikosi hicho, ambapo kwa sasa amejitwalia namba ya kudumu, akicheza kama winga, wakati mwingine namba 10.

Uchezaji wake wa kasi, chenga, na uwezo wa kupasua ngome za timu pinzani, umeonekana kuwarahisishia kazi wenzake licha ya kwamba mwenyewe hajafunga bao lolote.

Thomas Kipese, winga wa zamani wa Simba na Yanga, anasema kwa sasa timu hiyo imepata mtu aliyemwita 'kilainishi', ambapo kwa muda mrefu timu hiyo ilikuwa haijapata mchezaji wa aina hiyo, tangu kuondoka kwa Emmanuel Okwi.

2# Israel Mwenda - Yanga

Yanga ilimsajili Mwenda kutoka Singida Black Stars, ili kumsaidia Kibwana Shomari, ambaye naye alikuwa msaidizi wa Yao Kouassi, aliyefanyiwa upasuaji.

Mwenda, beki wa kulia wa zamani wa Simba, ameingia na mguu mzuri kwenye klabu hiyo, kwani mechi ya kwanza tu dhidi ya Copco FC, alitoa pasi mbili za mabao, akiisaidia timu yake hiyo mpya kushinda mabao 5-0 kwenye mchezo wa Kombe la FA.

Alikuwa kwenye kiwango bora kwenye michezo miwili ya Ligi Kuu, dhidi ya Kagera Sugar, ambapo Yanga ilishinda 4-0, na KenGold, ikishinda 6-1.

Kocha aliyeondoka, Sead Ramovic, alimchezesha kama winga kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar, alipoulizwa akasema alipendezwa mno na kasi yake, hivyo aliona akicheza karibu na lango la timu pinzani atakuwa na msaada mzuri zaidi kwa washambuliaji, hivyo alimpanga wingi ya kulia, na nyuma yake akawa Kibwana.

3# Jonathan Sowah - Singida

Amefunga bao la kwanza kwenye Ligi Kuu, akicheza mechi ya kwanza, akitumia dakika saba tu tangu mchezo kuanza dhidi ya Kagera Sugar, Ijumaa iliyopita.

Katika mchezo huo ambao uliiisha kwa sare ya mabao 2-2, raia huyo wa Ghana, alionesha kuwa kazi ambayo imemleta nchini ni moja tu, kupachika mipira ndani ya wavu.

Alimesajiliwa na Singida Black Stars, akitokea Al Nasr ya Libya, kipindi cha dirisha dogo la usajili.

Straika huyu anakumbukwa kwa kutakiwa na Klabu za Simba na Yanga kwenye usajili wa dirisha kubwa msimu huu, lakini katika hali iliyoshangaza wengi akaibuka akiwa na Singida Black Stars, dakika za mwisho wa usajili wa Januari.

Mashabiki wengi nchini wanamfahamu kwa kumuona kwenye Kombe la Shirikisho, hatua za makundi wakati akiichezea Klabu ya Medeama ya Ghana, iliyokuwa kundi moja na Yanga, ambayo ilifika fainali.

Yanga ilicheza dhidi ya Medema Desemba 2023 mechi mbili za nyumbani na ugenini, straika huyo akionekana kuwa kwenye kiwango bora, hivyo timu kubwa za Tanzania kuanza kumwania.

4# Zouzou Landry - Azam

Alicheza kama beki wa kati, Alhamisi iliyopita wakati Azam FC ikicheza dhidi ya KMC na kushinda mabao 2-0, Uwanja wa Azam Complex.

Zouzou, raia wa Ivory Coast, alisajiliwa kipindi cha dirisha dogo la usajili akitokea AFAD Djekanou ya nchini mwao, na hii ni baada ya Kocha Mkuu, Rachid Taoussi, kuhitaji 'kitasa', ili kuboresha safu ya ulinzi.

Katika mchezo wa kwanza tu aliocheza, alionekana ni mchezaji wa daraja la juu, akisaidiana na Yoro Diaby, kuhakikisha walimaliza mechi hiyo bila kuruhusu bao.

5# John Noble - Fountain Gate

Ukiondoa tukio lake la kupigwa kadi nyekundu katika mchezo kati ya timu yake ya Fountain Gate na Simba, alionesha umahiri mkubwa kwenye mchezo dhidi ya Simba, Alhamisi iliyopita, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara, akichangia kwa kiasi kikubwa sare ya bao 1-1 iliyopatikana.

Aliokoa michomo, na mipira ambayo ilionekana inaelekea kutinga wavuni.

Amesajiliwa na timu hiyo, akitokea Tabora United Januari. Kipa huyo raia wa Nigeria, kabla ya kujiunga na timu hiyo, alizichezea klabu mbalimbali nchini mwao ikiwamo Enyimba FC.