HIVI karibuni, Waziri mwenye dhamana ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, alinikumbusha jambo zuri sana katika historia ya nchi.
Mchengerwa alisema kiini cha kuwa na ofisi hiyo, ni kutokana na wazo la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere la kupeleka madaraka kwa wananchi wa chini, yaani waishio mitaani.
Alikuwa akizungumzia mbilingembilinge iliyoko mitaani sasa hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani.
Akasema Mzee Nyerere, alitaka kuona watu waishio pamoja vijijini, mitaani na vitongojini, wakijichagulia viongozi wao waliowaamini hasa kutokana na kuzoeana, pia na kuishi pamoja kwa muda mrefu.
Mchengerwa akadokeza, kuwa hali hiyo ilijiri hususan kipindi kile akiwapo Mwalimu Nyerere na watu kuchaguana bila matatizo yoyote na kupata viongozi wazuri na rahim.
Hali hiyo ilianza kipindi kile nchi ikitawaliwa na chama kimoja, enzi hizo TANU na baadaye kuzaliwa CCM baada ya muungano wa vyama vya TANU ya Tanganyika na ASP ya Zanzibar mwaka 1977.
Nayo CCM ikaongoza peke yake mpaka ilipotimu mwaka 1992 tuliporejea kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa, waliokuwa hawana vyeo kutokana na kutokuwa wanachama wa CCM nao wakaanza kuvipata.
Wakaibuka wenyeviti, makatibu wakuu na wengineo wakiwakilisha vyama vyao, lakini kipinzani. Na hata uchaguzi nao ukaanza kujigawa kipinzanipinzani hivi, kwamba kama wewe si mwana wa chama fulani, hufai kuongoza.
Gonjwa hilo likaendelea kututafuna mpaka sasa, hata ukifika uchaguzi, ule utanzania wetu unatoweka na kuanza kutazamana kama wenyeji na wakimbizi, ambao mpinzani anakuwa mkimbizi na mwana anachokitaja yeye anabaki kuwa mwenyeji.
Kifupi ikawa kwamba kama wewe si mfuasi au mwumini wa chama asichokitaka, basi hufai hata kulumangia, kwamba hustahili kuwa kiongozi katika nchi hii na siku zote utasimangwa na kusukwasukwa, huenda ikiwa ni pamoja na hata kupata misukosuko.
Mwaka fulani donda letu likaanza kutoka usaha na miaka iliyofuata likatumbuka kabisa na kutuanika Watanzania tulivyooza kisiasa, ukianika kasoro zizisofaa kutambulishana hata kidogo.
Ulipofika uchaguzi ikawa balaa, tunaonana kutoka kundi ligine kisiasa unabaki kuwa kuonekana mbumbumbu usiyestahili, una sifa ya ungumbaru wa kusoma, hadi kuandika, hivyo kushindwa kujaza fomu ya ugombea.
Mtu akabeba sifa hakujua alizaliwa lini na wapi na umri wake kumruhusu kugombea uongozi wa Taifa alimozaliwa, akaenguliwa na kutupwa jalalani kumpisha wa kundi jingine, anayepata urahisi kama wa kupita bila kupingwa.
Mwaka huu sana, yanameonekana tena ya waliokuwa wakishangiliwa kusoma vizuri risala, uchaguzi umefika. Ndio hilo sasa hawajui tena kusoma wala kuandika na hawafai kugombea kuongoza hata mitaa!
Kosa dogo la herufi linatosha kukuengua usigombee. Umekosea tu namba ya mwaka hufai kugombea! Utadhani sijui wanatafutwa viongozi wenye akili mnemba?
Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi naye anashangaa kama mimi! Kawaambia wahusika, akiwamo Mchengerwa, hebu dosari ndogondogo kama hizi tusizipe uzito sana kiasi cha kunyima wengine haki za kuwania uongozi katika Taifa lao, wanaenguliwa huku wananchi wakiwataka na hatimaye kuletewa wasiowataka! Hebu tuendelee kujifunza demokrasia, tutafika!
Tungekuwa na viongozi wengi kama Dk Nchimbi katika nchi hii, naamini makandokando kama haya yasingekuwa yanatuzibia njia ya maendeleo.
Najiuliza, hivi tukiamua kufuta vyama vyote vya siasa nchini ambavyo mimi naona ndivyo vinatugawa, tutakuwa tumepoteza nini?
Hivi mathalan ingekuwa mgonjwa akienda hospitali na kutakiwa kuandika jina lake kwenye kadi ingekuwaje?
Yaani kama sheria ingekuwa inamtaka mgonjwa akikosea jina asitibiwe, hivi hatuoni wengi tungeishia mochari?
Kama sivyo, kwa nini wasimamizi wasituhoji majina tukawambia wakaandika kuliko kututega ili tukosee watuengue? Mbona zamani mambo mengi tulitumia dole gumba na yakaenda?
Wengine wanakuja na oh kazi ya ujasiriamali haifai kukupa sifa ya kuwa mgombea, leo unakataa kutambua ujasiriamali wakati Dk. John Magufuli aliwapa Wamachinga vitambulisho vya Sh 20,000.
Rais Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa CCM Taifa, anawatambua bodaboda na kuwabatiza jina la ‘Maofisa Usafirishaji’, leo wewe nani unasema si kazi rasmi na si ujasiriamali, wanagombea nawaengua?
Acheni hizo!
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED