Rais Samia aieleza dunia Tanzania itakavyolisha Afrika

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:17 PM Nov 22 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: Mtandao
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema katika mkutano wa nchi zenye uchumi mkubwa duniani G20 alipata nafasi ya kueleza mikakati ya Tanzania ya kujitosheleza kwa chakula na kulisha nchi zingine Afrika.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari  mara baada ya mkutano huo wa G20 kuhusu mambo yaliyojadiliwa katika mkutano Rio De janeiro Brazil siku ya Jumatatu na Jumanne.

Alisema kama Tanzania haitakumbwa na madhara makubwa ya mabadiliko ya tabia nchi  basi itakuwa na uwezo wa kujitosheleza kwa chakula chake na kulisha majirani.

Alisema pamoja na hayo bado kuna maeneo ambayo iwapo yataongezewa nguvu hali ya uzalishaji wa chakula itakuwa bora zaidi na kutaja mambo hayo kuwa ni tafiti mbalimbali, matumizi ya mashine na mbolea.

Alisema bado dunia inakabiliwa na tatizo la njaa nan chi nyingi zimeweka mikakati ya nini cha kufanya kupunguza njaa na nchi zilizoendelea zimeahidi kutoa msaada wa kifedha kuondoa njaa.

“Tulipopewa nafasi sisi Tanzania tulisema kama hatutapata shida ya mabadiliko ya tabia nchi tutakuwa na uwezo wa kuzalisha ziada na kuauzia wenzetu wa mataifa mengine jirani,” alisema

“Tuna vikwazo ambavyo tukisaidiwa tutakwedna kasiz aidi kama kilimo, masuala ya kutumia mashine katika kilimo, mashine za kuvunia, kumwagilia na ardhi tuliyonayo tutaweza kwenda kwa kasi kubwa sana,” alisema

Alisema tatizo lingine ni uhaba wa mbolea hali ambayo inasababisha kuagiza nje ya nchi na kwamba kazi kubwa iliyopo ni kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya mbolea ili kujitosheleza na kuachana na utegemezi.

“Tukiweza kutumia mbolea sahihi na tukawa na mbolea inayojitosheleza tutalisha wenzetu wa Afrika kwasababu kama leo hii tunauza baadhi ya bidhaa hadi China inamaana tukijipanga vizuri tunaweza kabisa kufanya vziuri,” alisema