Tundu Lissu aibuka kisera zaidi

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 12:23 PM Nov 22 2024
Tundu Lissu aibuka kisera zaidi

MAKAMU Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ameibuka na hoja mpya, safari hii akijikita kisera zaidi akiwataka wanachama na watanzania kutokuwa wanyonge kutokana na wagombea wao walioenguliwa katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Amesema wana nafasi ya kuwakataa katika sanduku la kura kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi huo kisha kurudiwa uchaguzi kwa kuwekwa wagombea wengine.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akihutubia wananchi wa Nyamongo, huko Tarime Vijijini, mkoani Mara wakati wa ufunguzi wa kampeni za uchaguzi zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Lissu alisema chama hicho kina wagombea 2,612 nchi nzima na kuwa idadi hiyo siyo haba, hivyo kuwataka wananchi na wanachama wao kuhakikisha wagombea hao wanashinda, ikiwa ni sehemu ya kupunguza alichokiita "maumivu ya wale walioondolewa katika uchaguzi huo".

Alisema katika eneo la Nyangoto, kama ilivyo kwa maeneo mengine, mgombea wao wa nafasi ya mwenyekiti ameenguliwa katika kinyang’anyiro, hivyo kuwapatia kazi mbili wananchi wa maeneo yenye tatizo la namna hiyo ili kuhakikisha wanapata viongozi wanaowapenda baada ya walioteuliwa kuenguliwa.

"Kwanza, ni kuhakikisha wale wote waliobaki katika kinyang’anyiro wanashinda nafasi wanazozigombea. Mfano, katika eneo hili mkihakikisha tuna wawakilishi hawa 25 katika Halmashauri ya Kijiji, sisi ndiyo wenye uamuzi bila kujali kiongozi ni yupi," alisema Lissu.

Alitaja mbinu nyingine ya kuwakataa wagombea aliodai "wamewekwa bila idhini ya wananchi", ni kuwapigia kura ya 'HAPANA' na kuwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi, ili mgombea ashinde nafasi hiyo ni lazima awe na kura za ndio zaidi ya asilimia 50.

"Hii ni tofauti na kanuni za mwaka 2019, tukishapiga kura za 'HAPANA' kwa namna yoyote, lazima mwezi ujao turudie uchaguzi na sisi tutaweka wagombea wetu, na ninajua mtafanya mnachokifanya miaka yote, hamtakubali kuibiwa kura, atakayejaribu kutuchezea kwenye kura, mnajua cha kumfanya, hivyo ninajua tutashinda kwa kishindo," alisema Lissu.

Akiwa Lamadi, mkoani Simiyu, Lissu alisema nchi haitakombolewa kwa kupiga magoti na kufanya maombi, bali kwa kufanya mabadiliko ya msingi kwenye mfumo ya kuiendesha.

"Kwenye uchaguzi huu, si mnafahamu ambavyo wameharibu? Wameharibu sana, si tu kwa sababu ni wabaya bali pi kwa sababu hatukufanya mabadiliko ya msingi kwenye mfumo wetu wa kuendesha nchi.

"Wanaotengeneza kanuni za uchaguzi ni wao wenyewe, wanaozisimamia, wanaoamua mchezo uchezweje, marefarii na  wachezaji ni wao wenyewe, unategemea nini? Unategemea tutendewe haki? Kama tusipopambana katika huu mwaka uliobaki, tukabadilisha sheria za uchaguzi, tukabadilisha na tume, mwaka ujao yatakuwa yaleyale.

"Nani anayeamini kwamba hawa wanaweza wakafanya tofauti na walivyofanya mwaka 2019 na mwaka 2020? Kwa hiyo, kwa huu mwaka mmoja uliobaki, tuache mchezo, tuache kuwachekea watatumaliza.

"Mwaka ujao yatakuwa ni yaleyale na yakitokea yaleyale, wajinga watakuwa ni sisi kwa sababu hakuna asiyeyajua wanayoyafanya, tukiruhusu wafanye tena, wajinga watakuwa sisi na hakuna visingizio.

"Nchi haikombolewi kwa maombi, haikombolewi kwa kupiga magoti na kumwomba Mungu, inakombolewa kwa mapambano, fanyeni kampeni, mkafanye uchaguzi, wagombea wawekeni kwenye nafasi tuanze kujijenga upya," alisema Lissu.

Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi, aliwaomba wananchi kuchagua wagombea wanaotokana na chama hicho, kwa kuwa kina wagombea makini ambao wana maslahi na maisha ya wananchi.

"CHADEMA tumesimama imara kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake. Tunasimamia sera ambazo zitahakikisha huduma bora kwa wananchi wetu, bila kubagua mtu yeyote. Tutahakikisha miundombinu ya afya, barabara, elimu na huduma za jamii zinaboreshwa," alisema Ntobi.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA Taifa, Yahaya Alawi kutoka Zanzibar, akizindua kampeni mkoani Geita, aliwataka wananchi kufanya mabadiliko katika uchaguzi huo ili yawasaidie kunufaika na rasilimali za madini walizonazo mkoani humo.

Alisema madini ya dhahabu popote duniani ni hazina lakini wakazi wa eneo husika, yaani mkoa wa Geita, licha ya kujaliwa kuwa na utajiri wa rasilimali hiyo, wanakabiliwa na umasikini.

"Tufanye mabadiliko kwa kutumia haki ya kikatiba kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaotokana na CHADEMA, jitokezeni kwa wingi Novemba 27, 2024 kutekeleza haki yenu hii ya msingi," alisema Yahaya.

*Imeandaliwa na Elizabeth Zaya (DAR), Vitus Audax, Marco Maduhu (SHINYANGA), Alphonce Kabilondo (GEITA).