UBOMOAJI wa jengo lililoporomoka Jumamosi Kariakoo, jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu 20 na makumi wengine kujeruhi umeanza, huku Waziri Mkuu akizindua kamati ya uchunguzi wa tukio hilo na usalama wa majengo katika eneo hilo la kibiashara.
Juzi Rais Samia Suluhu Hassan alitembelea eneo hilo muda mfupi baada ya kuwasili nchini akitokea Brazil na kuagiza maduka yaliyoko mbali na eneo la tukio kuanzia jana yafunguliwe huku shughuli ya kulibomoa jengo na kuhifadhi mizigo ya wafanyabiashara ikiendelea.
Shughuli hiyo inafanywa na vyombo vya dola ambao hadi jana saa 11 jioni ilikuwa inaendelea huku mitambo mbali ikionekana ikitumika kunasua mizigo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alizungumza na Nipashe, akifafanua kuwa hatua inayofuata ni kuhifadhi mizigo iliyonasuliwa ili baadaye itambuliwe na wenye mali.
Alipoulizwa iwapo kuna watu wengine wameokolewa, Chalamila alisema hakuna miili wala majeruhi wengine waliopatikana katika hatua hiyo.
"Wenye maduka wameunda kundi la WhatsApp, wanawasiliana kwa ajili ya kupeana taarifa kuhusu mizigo yao ambayo tutaihifadhi mahali salama kisha baadaye watakuja kuichukua.
"Unajua mizigo ikiangukiwa na jengo haiwezi kuwa sawa, kama ambavyo namna ghorofa hilo lilivyoporomoka, lakini zoezi la uhamishaji mizigo kupitia vyombo vya dola linaendelea na linakwenda vizuri," alisema Chalamila.
KAMATI YAZINDULIWA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana alizindua Kamati ya Wataalamu ya Uchunguzi wa Jengo hilo na kuitaka ihakikishe kuwa inafanya uchunguzi kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia viwango vya kitaaluma.
Alizindua kamati hiyo kwenye ukumbi wa mikutano ulioko Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni, jijini Dar es Salaam, akiagiza itekeleze majukumu yake kwa kufuata sheria, kanuni na maadili ya kazi.
Amesema mbali na kuchunguza jengo hilo lililoporomoka, kamati hiyo pia imeundwa ili kuchunguza majengo mengine yanayoendelea kutumika katika eneo la Kariakoo, kuchunguza uimara wa majengo yanayojengwa, kuchunguza endapo taratibu zinafuatwa wakati wa ujenzi, ikiwamo vibali, makandarasi wenye sifa na usimamizi wa mamlaka husika wakati wa ujenzi.
Waziri Mkuu alisema madhumuni mengine ya kuundwa kwa kamati hiyo ni pamoja na kuchunguza endapo uboreshaji majengo unaofanywa Kariakoo unazingatia sheria, kanuni na taratibu pamoja na kubainisha majengo yote yaliyo katika hatari ya kuanguka na kupendekeza hatua za kuchukua.
Tarehe 16 Novemba mwaka huu, saa tatu asubuhi, ilitokea ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa tatu katika Mtaa wa Agrey, kata ya Kariakoo, jijini Dar es Salaam na kusababisha athari kubwa kwa watu na mali katika eneo hilo. Baada ya ajali hiyo, Rais Samia alimwelekeza Waziri Mkuu kuunda kamati hiyo ya uchunguzi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED