Rais Samia Suluhu Hassan amezungumzia mambo muhimu yaliyojadiliwa na viongozi wa nchi tajiri zaidi duniani uliofanyika Rio De janeiro Brazili siku ya Jumatatu na Jumanne.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Rais Samia amesema lengo la viongozi wa Afrika ni kwamba ifikapo mwaka 2030 watu milioni 300 Afrika wawe wameshapata umeme.
Amesema hivi sasa Afrika watu milioni 700 hawana umeme kabisa hivyo angalau ikifika mwaka 2030 watu milioni 300 wawe wameshapata umeme.
“Sasa 2030 tukijaliwa na mambo yakaenda vizuri namimi nitakuwa nimemaliza dhamana hii nitajidai kuwa nimewezesha watu hao kupata umeme,” alisema
Alisema kando ya mkutano wa G20 alipata nafasi ya kukutana na viongozi wa nchi mbalimbali na wakuu wa taasisi za kimataifa ambapo walijadili ushirikiano uliopo, miradi na maeneo mapya ya uwekezaji.
Alitaja baadhi ya viongozi aliokutana nao kuwa ni Waziri Mkuu wa Norway ambaye walijadili kuhusu ajenda ya nishati safi ya kupikia, Rais wa Misri ambaye walijadili mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere JNHPP na Waziri Mkuu wa Vietnam waliyejadiliana naye kuhusu ushirikiano katika sekta ya mawasiliano.
Pia alisema alikutana na Rais wa Indonesia, ambaye walijadiliana kuhusu ushirikiano uliopo kwenye sekta ya mafuta na gesina marais wa benki ya dunia na benki ya maendeleo Afrika.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED