Wahitimu Kibaha watakiwa kuunda vikundi vya uzalishaji mali

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 07:30 PM Nov 22 2024
Wahitimu Kibaha watakiwa  kuunda vikundi vya  uzalishaji mali
Picha:Julieth Mkireri
Wahitimu Kibaha watakiwa kuunda vikundi vya uzalishaji mali

MKURUGENZI wa Elimu Ofisi ya Rais Tamisemi Dk. Emmanuel Shindika amewataka wahitimu katika chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali ambavyo vitakuwa njia ya mafanikio itakayopapatia fursa ya kuunganisha ujuzi na kutumia rasilimali zitakazopatikana kwenye maeneo yao.

Shindika ameyasema hayo alipokuwa akihutubia wananchi kutoka maeneo mbalimbali pamoja na wahitimu 147 wa fani za ufundi bomba, ufundi wa magari, umeme, uungaji na uundaji wa vyuma, ushonaji, kilimo na mifugo  kwenye mahafali ya  chuo hicho ambacho kiko chini ya Shirika la Elimu Kibaha.

 Amesema serikali imejipambanua katika kuimarisha uchumi kwakua na sera nzuri  za kibenki, ukopeshaji na ushirika wa akiba na mikopo na hivyo vijana wanaohitimu wanatakiwa kutumia fursa hizo kwa kujiunga kwenye vikundi na kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri.

Kadhalika amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI imejipanga kuhakikisha Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha kinazidi kupata fursa za kimafunzo na kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.

1

Amesema Serikali itaendelea kupeleka fedha za ukarabati wa mabweni ya wanachuo  na miundombinu mingine, huku changamoto nyingine zilizopo Serikali itaangalia namna ya kuzitatua .

Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha Robert Shilingi ameiomba Serikali kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya chuo hicho ili vijana wanaojiunga katika chuo hicho kusoma katika mazingira mazuri.

Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha Joseph Nchimbi aliiomba Serikali kusaidia fedha za ruzuku kwa ajili ya chakula na uendeshaji kama ilivyo katika vyuo vingine vya FDC vilivyo chini ya Wizara ya Elimu.

Nchimbi pia ameomba chuo hicho kiweze kusaidiwa gari kwa ajili ya usafiri  sambamba na fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati na kuongeza majengo.