CHIMBUKO SHERIA WATOTO NJITI...Waanzilishi wanaharakati; TUGHE, TUCTA zikapokea kijiti

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 09:41 AM Feb 07 2025
MADAKTARI wa watoto waliozaliwa njiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), katika picha ya pamoja na wazazi wao, katika Maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Watoto Njiti
Picha: Mtandao
MADAKTARI wa watoto waliozaliwa njiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), katika picha ya pamoja na wazazi wao, katika Maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Watoto Njiti

IJUMAA siku ya mwisho mwezi uliopita, Januari 31, gazeti la Nipashe lilichapisha makala inayosomeka "Kinamama kwenye ajira wenye watoto njiti, namna wanavyoteseka kazini wakiwa na vichanga’..."

Makala hiyo ilieleza madhila wanayokutana nayo wafanyakazi wanaojifungua watoto njiti, kwa kukosa likizo na muda wa kutosha kuwahudumia watoto wao.
 
Siku moja baada ya kuchapishwa gazeti hili, serikali nayo kupitia Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, liliridhia hoja ya kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa wanawake wanaojifungua watoto njiti.

Hiyo imekuwa ikipigiwa chapuo kwa muda mrefu na wadau mbalimbali wa haki za wafanyakazi. Kulingana na uamuzi huo, likizo ya uzazi itaongezwa kufikia wiki 40 za ujauzito, huku baba wa mtoto njiti akipewa siku saba za mapumziko.
 
Ni hatua muhimu na juhudi za wadau ikiwamo taasisi ya Doris Mollel, ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakipigania haki hiyo, kwa lengo la kulinda ustawi na afya za watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.

Watoto hao wanahitaji uangalizi wa karibu kutoka kwa wazazi wao ili kuhakikisha ukuaji wao unakua kwa afya njema.
 
SAFARI YA HAKI

Majadiliano kuhusu hoja hiyo, yalianza rasmi mwaka 2017 na mwaka 2018, suala hilo lilipelekwa bungeni kwa mara ya kwanza. 

Mnamo Januari 31, 2025, muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi Namba 13 wa Mwaka 2024 uliwasilishwa bungeni na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Awali, akiwasilisha muswada huo uliopendekeza likizo hiyo iende hadi wiki 36, lakini baada ya majadiliano na kamati husika, serikali ilikubaliana kuongeza muda huo hadi kufikia wiki 40. Ni ujumbe wa tabasamu wa ‘kuupiga mwingi!’

Kadhalika, likizo ya baba kwa mtoto njiti imeongezwa kutoka siku tatu hadi saba, ili kutoa fursa inayomsaidia mama na mtoto.
 
MAREKEBISHO SHERIA AJIRA 

Mbali na suala la likizo ya uzazi, muswada huo umependekeza mabadiliko mengine kadhaa katika Sheria za Ajira nchini. Kifungu kipya cha 34 A kimependekezwa ili kumruhusu mwajiri kumpatia mwajiriwa likizo bila ya malipo isiyozidi siku 30 kwa dharura au majanga yanayoweza kutokea. 

Pia, Kifungu cha 14 kinabainisha aina mpya za mikataba ya ajira, ikiwamo ajira ya muda maalum kwa wale wanaojifunza kazi au katika mazingira maalum kama vile misimu ya kilimo au utalii.
 
Vilevile, Kifungu cha 37 kinazuia mwajiri kuanzisha au kuendelea na shauri la nidhamu dhidi ya mwajiriwa endapo mgogoro huo upo mbele ya Tume ya Usuluhishi na Mahakama ya Kazi. 

Lengo la hatua hii ni kuzuia uingiliaji wa mchakato wa kushughulikia migogoro ya ajira.
 
LIKIZO WAZAZI WA NJITI

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatuma Toufiq, alipendekeza serikali kuboresha sheria hiyo zaidi kwa kuzingatia pia haki za akina mama wanaojifungua watoto wenye mahitaji maalum kama vile watoto wenye usonji, vichwa vikubwa, mgongo wazi, mdomo sungura, matundu kwenye moyo, na seli mundu. 

Mapendekezo hayo yanalenga kuhakikisha watoto hao wanapata uangalizi wa karibu kutoka kwa wazazi wao kwa muda wa kutosha.
 
Mbunge wa Mchinga, Salma Kikwete, akawataka wanaume wanaopewa likizo ya wiki moja, kutumia muda huo kuwahudumia wake zao na watoto wao, badala ya kushiriki shughuli zisizohusiana na familia.
 
AJIRA ZA WAGENI

Muswada huo pia umeweka masharti mapya kwa wageni wenye vibali vya kazi nchini Tanzania. 

Mwekezaji wa kigeni mwenye kibali cha kazi, hatalazimika kupata kibali kingine endapo atakuwa anamiliki hisa katika kampuni tofauti. 

Aidha, wakimbizi wenye hadhi stahiki wataendelea kufanya kazi bila kubanwa na ukomo wa muda wa kibali cha kazi.

Pia, kuna kifungu cha muswada huo, kimeweka masharti ya kuzuia urejeshwaji ada ya maombi ya kibali cha kazi, huku Kifungu cha 12, kikirekebishwa kuruhusu maombi ya kuhuisha kibali cha kazi kuwasilishwa angalau miezi miwili, kabla ya kuisha kwa muda wa kibali kilichopo.
 
WANAOWAPIGANIA NJITI

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation, Doris Mollel, baada ya bunge na serikali kupitisha mabadiliko ya sheria hiyo, ana ufafanuzi wa sababu za kuanzisha vuguvugu la mabadiliko ya Sheria ya Mwaka 2024 kwa wazazi wanaopata watoto njiti.

Anasema ni kutokana na changamoto nyingi wanazokutana nazo wafanyakazi wanawake wanaojifungua watoto njiti, ikiwamo tatizo la kiafya, msongo wa mawazo na kufutwa kazi kunakotokana na kutumia muda mrefu hospitalini.

Dorice anasema kuwa, tangu mwaka 2017 wamekuwa na shughuli, vikao na harakati mbalimbali za kupambania mabadiliko hayo, wazo likianza mwanzoni mwa mwaka 2017 wakati alipotembelea wodi ya watoto njiti kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, alipoenda kuchangia vifaa tiba hospitalini hapo.
 
Doris anabainisha, miongoni mwa shughuli zilizofanyika mwanzoni mwa vuguvugu hilo, ni pamoja na vikao zaidi ya 50 vikihusisha wahusika  mbalimbali,wakiwamo Umoja wa Wake wa Viongozi Nchini (Millenium Group), Umoja wa Wabunge Wanawake (TWPG).

Pia, kuna wanasheria wa wizara mbalimbali, ,awaziri, Wabunge wanawake, wafanyakazi wanawake, Chama cha Madaktari wa Watoto Wachanga, pamoja na Kamati za kudumu za bunge na maofisa wa wizara mbalimbali serikalini.
 
Mwaka 2021, Taasisi ya Doris Mollel Foundation ilianzisha Ajenda ya "Mtoto Njiti" na baadae mwaka 2023, Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) na Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), nao waliunga mkono jitihada hizo za Doris Mollel Foundation.

Ni suala lililofikisha mwaka jana wakati wa sherehe za siku ya wafanyakazi duniani, Rais Samia Suluhu Hassan akatoa kauli yake ya kwanza hadharani, kupitia kwa Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, akitangaza ujio wa marekebisho ya sheria hiyo ya kazi.
 
Akimshukuru Rais Dk. Samia, aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Waziri Angellah Kairuki, Doris Mollel anasema kupitia marekebisho hayo ya sheria, Tanzania sasa inakuwa katika nchi chache barani Afrika, zinazounda mazingira jumuishi na bora kwenye kazi, yakizingatia afya ya wazazi wanaopata watoto njiti nchini kote.

CHAMA CHA WAFANYAKAZI 
 
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), nao wametoa pongezi zao kwa serikali, kupitia bunge kuridhia na kupitisha sheria hiyo.
 
Makamu Mwenyekiti wa TUGHE, Dk. Jane Madete, anasema ni hatua itakayosaidia kulinda ustawi wa watumishi wanaojifungua watoto njiti nchini, kwani imekua changamoto kwa na ya muda mrefu kwa wafanyakazi wanawake wanaojifungua watoto njiti.
 
Anaeleza, wamekuwa wakipitia changamoto zikiwamo za kiafya, hivyo wanahitaji kupata muda wa mwingi wa kupumzika na kumhudumia mtoto, kutoka ngazi ya uangalizi hadi wanaporuhusiwa kutoka hospitalini.
 
" Pia, wamekuwa kwenye wasiwasi mkubwa wa kupoteza ajira zao, jambo ambalo linaweza kupelekea msongo wa mawazo na hata kuathiri kwa kiasi kikubwa malezi ya mtoto aliyezaliwa" anahitimisha.