INAPOTAJWA suala la Virusi Vinavyosababisha Ukimwi (VVU), huwa vinaendana na kuwapo taarifa za aina mbalimbali, zikiwamo za mafanikio, sherehe, ugonjwa au msiba, zote zina njia zinazojulikana na zinapaswa kuzingatiwa kuhakikisha zinafika kwa wakati sahihi.
Ndipo kunatajwa kuwapo njia nyingi za kufikishaji taarifa za ugonjwa na mwongozo maalum wa taifa unaosimamiwa na Wizara ya Afya.
Pia serikali kwa kutambua umuhimu huo kwa mtoto walioambukizwa VVU, namna ya kumfanya atambue hali yake kutatua changamoto alizo nazo, zimekuwa zikiwakumba wazazi au walezi, sasa kumetolewa kutoa mwongozo maalum wa namna ya kufikisha taarifa kwa njia sahihi.
Dk. Lilian Mwakyosi, anayejihusisha na kuelimisha jamii kuhusu Ukimwi na HIV, anasema kuna umuhimu mtoto kupewa taarifa kama amepata maambukizi ya VVU, lakini unapaswa kuzingatia mwongozo wa nchi unaoelekeza namna nzuri ya kufikisha hizo taarifa taratibu, kulingana na umri wake.
“Mtoto asipoambiwa kuna athari zinazoweza kujitokeza, hawezi kuwa makini katika kunywa dawa kwa usahihi kwa kuwa hajui anakunywa kwa sababu gani.
“Pia, alikuwa anaweza kusababisha maambukizi bila ya kujijua baada ya kwenye uhusiano,” anasema Dk. Lilian, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya DARE.
Katika mwongozo wa Wizara ya Afya,
unaeleza mtoto anapofikisha umri miaka minne hadi sita, anatakiwa aanze kupewa taarifa kwa hatua kuhusu maambukizi yake.
Inafafanuliwa pale mtoto anapofikisha kati ya miaka nane hadi 10 na anaonekana ana uwezo wa kuelewa masuala ya maisha na anamudu masomo darasani, mtoto huyo atakuwa na uwezo kuelewa masuala ya afya yake na kinga inavyofanya kazi mwilini.
Inatarajiwa katika umri huo, atapewa taarifa kamili kuhusu hali yake ya maambukizi ya VVU. Pia, inabainisha umuhimu wa mzazi au mlezi, kwa kushirikiana na mtoa huduma, wakaandaa mpango kumweleza mtoto hali yake, kabla hajataarifiwa na vyanzo vingine.
“Kusikia habari kuhusu hali yake ya maambukizi kutoka kwa mtu mwingine, kunaweza kumfanya mtoto ajisikie vibaya na atingwe na msongo wa mawazo na hata kupeleka kuchukua maamuzi yasiyofaa kama vile kujiua, kuacha shule, kuacha dawa hata kutokuwa na imani na wazazi wake,” inaelezwa.
Katika taarifa hiyo, inaelezwa mtoa huduma anatakiwa kuzingatia mambo kadhaa kabla ya kumweleza mtoto mwenye VVU hali yake.
Hapo kunatajwa hitaji la kutathmini uwezo wa mtoto kukabiliana na taarifa za kushtua, pia uwapo uhusiano mzuri kati ya mlezi au mzazi, mtoto, pia mtoa huduma.
VVU VINAVYOMPATA MTOTO
Kuna ufafanuzi wa wataalamu wa afya, kwamba anaweza kuambukizwa VVU kwa kuchangia mswaki na vitu vyenye ncha kali kama vile sindano na nyembe, kisha akaongezwa damu yenye VVU.
Kuna sehemu kwenye utumiaji dawa za kulevya kwa njia ya sindano unafanyika, watoto pia wanakuwa hatarini kupata maambukizi ya VVU, kwa kuchangia sindano husika.
Pia, inatajwa maambukizi kwa njia ya ngono hutokea kwa watoto wanaoanza wakiwa katika umri mdogo, kukiwapo maelezo:
“Baadhi ya sehemu kuna dhana potofu kwamba VVU inapona na kuisha kabisa pale unapofanya ngono na mtoto mdogo au mtoto ambaye hajawahi kufanya ngono. Hivyo kufanya watu wanaoishi na VVU kuwabaka watoto na kuwaambukiza VVU,” inaelezwa.
Usafirishaji haramu watoto kwa visingizio vya kuwapatia elimu au kazi bora, nako kunatatajwa kuwaweka watoto hatarini kupata maambukizi ya VVU, kwa kulazimishwa kufanya biashara ya ngono na hata kubakwa.
HATUA ZINAVYOCHUKULIWA
Hapo kisaikolojia kunatajwa utayari wa mlezi au mzazi kumweleza mtoto wake mwenye VVU hali yake ya maambukizi, wajibu akiubeba mtoa huduma akishirikiana na mlezi au mzazi.
Ni hatua inayoanza na kuandaa mpango wa kumweleza mtoto hali yake ya maambukizi utakaokidhi mahitaji ya mtoto na familia husika, ikisisitizwa umuhimu wa kuwapo mawasiliano endelevu kuhusu afya ya mtoto, kwa kuwa mtoto anapozidi kukua,uelewa wake pia unapanuka.
Hivyo, inatajwa kuwa mtoa huduma anapaswa kuzungumza na mzazi au mlezi, faida na hasara za kumweleza mtoto mwenye VVU hali yake, wachukue kwa busara uamuzi wa pamoja.
“Kumbuka kumweleza mtoto mwenye VVU hali yake ya maambukizi hakuhitaji haraka. Pata muda wa kutosha wa kushauriana na mtoa huduma namna ya kutoa taarifa hiyo kwa mtoto wako,” unaeleza kipeperushi cha mwongozo wa Wizara ya Afya.
Monika Jorum (siyo lake halisi), anaishi na VVU, akiwa na maelezo ya masikitiko kuwa alifiwa na mwanawe mwaka 2007 akiwa na umri wa miaka saba, lakini baada ya kifo ndiyo ikajulikana tayari naye alikuwa na VVU.
Anasema, alijifungua mwanawe akiwa na afya njema na hakufahamu wao kuwa na VVU. Baada ya miaka kadhaa, mwanawe alianza kuugua kifua, akatibiwa pasipo hali ya kutengemaa.
“Naamini ningekuwa nimejua mapema pengine ningemsaidia naye aweze kupata dawa. Pia, ningemweleza kwa kuwa ndugu zake nimeshawaeleza, japo wao hawana maambukizi ya VVU, lakini naamini kuwa taarifa ni muhimu kwao na kwangu pia,” anasema Monika.
KUTOKA TACAIDS
Kaimu Meneja wa Mipango na Bajeti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Renatus Mukasa, ana maelezo kwenye mafunzo maalum yaotawyo ‘Science Cafe’ yanayosimamiwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA).
Anasema, kuna haja ya elimu ya kuzuia maambukizi ya HIV kuendelea kutolewa kwa msisitizo, ili ama kukumbusha au kuongeza umakini wa mapambano.
Mukasa anadokeza kwa kutumia Utafiti wa Kitaifa wa Athari za VVU Tanzania 2022-2023 uliofanywa majumbani, uligundua kulikuwapo takriban mikasi mipya 60,000 za maambukizi ya VVU miongoni mwa watu wazima nchini.
Mukasa ambaye ni Mchumi Mwandamizi, anaeleza utafiti umebaini kuwapo tofauti kubwa katika kiwango cha maambukizi ya VVU kulingana na umri, jinsia na kanda zilizopo.
“Kiwango cha juu cha maambukizi kilikuwa miongoni mwa wanawake na katika baadhi ya mikoa ya Tanzania Bara. Kiwango cha maambukizi ya VVU kilikuwa chini ya asilimia moja katika mikoa yote ya Zanzibar,” anasema.
Mukasa anaongeza kuwa, suala la kusonga mbele katika lengo la Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Ukimwi (UNAIDS) la mwaka 2030 la kumaliza Ukimwi, kunahitaji umakini wa ufuatiliaji unaoendelea kugundua maambukizi mapya yalivyo.
Pia anataja tiba kutolewa kwa wakati na huduma za kinga mchanganyiko za kuzuia maambukizi zaidi zikipatikana.
Katika utafiti huo, pia ulitoa taarifa muhimu kuhusu maendeleo ya kitaifa na kikanda kuelekea kudhibiti janga la VVU ikiwamo maendeleo kuelekea kufikia malengo ya 95-95-95 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Kudhibiti Ukimwi (UNAIDS).
Tanzania hadi sasa, inatajwa imeshafika lengo la pili kati ya malengo matatu ya UNAIDS 95-95-95 kabla ya mwaka 2025, ikionyesha upatikanaji wa programu za matibabu madhubuti kwa wale wanaojua hali yao ya VVU.
Ni utafiti uliofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) na msaada wa kiufundi kutoka Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) vya Marekani na ICAP katika Chuo Kikuu cha Columbia.
Hapo kuna washirika wa ndani, ipo Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR)na taasisi nyingine kadhaa.
Katika uzinduzi wa Muungano wa Kimataifa Kutokomeza Ukimwi kwa Watoto Afrika, unaokutanisha mawaziri wa afya na wawakilishi kutoka nchi 12 za Kiafrika, pia wadau kimataifa uliofanyika mjini Dar es Salaam, Februari Mosi mwaka jana.
Hapo walikubaliana kuweka mipango ya kutokomeza Ukimwi miongoni mwa watoto, ifikapo mwaka 2030, chini ya usimamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Kutokomeza VVU na Ukimwi (UNAIDS).
Ni muungano utakaofanya kazi kwa miaka minane, ikibainishwa kuwa wakati robo tatu ya watu wazima wanaishi na virusi vya Ukimwi, asilimia 76 wako katika matibabu.
Watoto nao ambao ni sawa na asilimia 52, ndio wanaopata matibabu ya dawa za kurefusha maisha na kupunguza makali ya VVU.
Takwimu za mwaka 2021 za UNAIDS, zinabainisha watoto 160,000 walipata maambukizi mapya ya VVU, kati yao asilimia 15 ya vifo vyote vitokanavyo na Ukimwi, vinaangukia kwa watoto, licha ya kwamba wao ni asilimia nne pekee ya kundi hilo linaloishi na VVU.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED