Waziri aonya fikra Kigoma kichaka ajira

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:10 AM Nov 17 2024
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  Deus Sangu.
Picha:Mpigapicha Wetu
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu.

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu amesema Kigoma si mkoa wa kupatia cheki namba (ajira) na kuhama kwa visingizio vya kuifuata familia au ugonjwa.

Kutokana na hali hiyo , amewataka watumishi kuachana na dhana  kuwa mkoa ni wa pembezoni na hauna fursa za kiuchumi.

Sangu aliyasema hayo jana wakati akizungumza na  watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, ikiwa ni kliniki ya kimkakati ya kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa kero mbalimbali zinazowakabili  watumishi hao.

Alisema kwa kushirikiana na waziri wake, George Simbachawene, wameweka utaratibu wa kufanya klikini hiyo katika mikoa mbalimbali nchini baada ya kuona watumishi wengi wanalazimika kusafiri hadi Dodoma kwa ajili ya changamoto walizo nazo za kiutumishi ambazo zingeweza kutatuliwa papo kwa papo na maofisa utumishi wao. 

Sangu alisema kuna dhana imejengeka kuwa mikoa ya magharibi ikiwemo Katavi, Kigoma na Rukwa kuwa ni  ya adhabu kwa watumishi ambao wamepangiwa kufanya kazi katika maeneo hayo. Alisema jambo hilo si kweli ambalo hasa baada ya    uboreshaji mkubwa  wa miundombinu uliofanywa na serikali.

 â€˜â€™Kumekuwa na wimbi kubwa la watumishi wa umma mara baada ya kupata ajira huja kuripoti mkoani Kigoma  na kuanza taratibu za kuomba uhamisho. Jambo  hili si sawa kwani wananchi wa Kigoma nao wanahitaji huduma bora kama wananchi  wa Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza,’’ alisisitiza. 

Alisema mtumishi wa umma atalazimika kuhama katika mkoa huo endapo atakuwa amekaa miaka mitatu na kuendelea na pia kama atakuwa amepata mtumishi mwenzake wa kubadilishana nae. 

Sangu alisema Kigoma ya sasa ni bora kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka mitatu, ametoa zaidi ya Sh. trilioni 11 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ikiwamo barabara na huduma mbalimbali kama vile afya katika mkoa huo. 

Alisema kutokana na uboreshaji wa miundombinu hiyo,  kwa sasa Kigoma haina tofauti na Dodoma na Arusha kwa kuwa ina kila aina ya fursa pamoja na  miundombinu mizuri.  

Mbunge wa Kigoma Mjini, Kirumbe Ng’enda, alisema Kigoma inahitaji watumishi wachache lakini wenye utayari wa kufanya kazi na si wale walioletwa baada ya kufanya vibaya katika mikoa mingine. 

Awali, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mbwilo Elisante,  alisema mkoa  unakabiliwa na uhaba mkubwa wa watumishi kutokana na wengi kuhamishwa bila  kuletwa mbadala.