MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, Mutallah Mbillu,ametoa msaada wa dawa za kuogeshea mifugo lita 12,ikiwa ni mpango mkakati wa serikali kudhibiti na kukabiliana na magonjwa yanayoathiri mifugo ukiwamo wa ndigana baridi.
Amesema hayo,wakati akiongoza zoezi la kuogesha mifugo katika eneo la Lata Kata ya Oloipiri, kwa ajili ya kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa ndigana baridi unaowaathiri mifugo mbalimbali wakiwemo ng'ombe.
Alisema shughuli ya uogeshaji wa mifugo imefanyika ikiwa ni mpango mkakati wa kuimarisha ufugaji na itawawezesha wananchi kuogesha mifugo yao bure .
Akizungumza wakati zoezi hilo,amewasisitiza wafugaji kuogesha mifugo yao kila baada ya siku saba badala ya desturi ya kuogesha kila mwisho wa mwezi, ili kuhakikisha kinga madhubuti dhidi ya ndigana baridi.
Hata hivyo,amesema afya bora ya mifugo ni muhimu kwa ustawi wa kiuchumi wa halmashauri hiyo, kwa kuwa wafugaji ni nguzo kuu ya mapato ya halmashauri.
Naye Ofisa Kilimo,Mifugo, na Uvuvi wa halmashauri hiyo,Chobby Chubwa,amesema katika kuhimiza wafugaji kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo,alibainisha kuwa ugonjwa wa ndigana baridi unaweza kudhibitiwa kwa njia ya kuogesha mara kwa mara.
Aidha amesema asilimia 70 ya magonjwa ya mifugo hutokana na kupe, hivyo kuogesha mifugo ni hatua muhimu katika kuboresha afya ya mifugo.
Akizungumza kwa niaba ya wafugaji katika eneo hilo,Ramatho Saringe,mkazi wa Kijiji cha Oloipiri,ameishukuru serikali na halmashauri kwa kuanzisha na kusimamia zoezi hilo kwani hatua hiyo itasaidia kudhibiti ugonjwa wa ndigana baridi ambao umekuwa changamoto kubwa kwa mifugo yao.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED