RIPOTI MAALUM: Utumikishaji watoto majumbani mfupa mgumu

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:25 AM Nov 17 2024
Pamoja na juhudi mbalimbali za serikali za kuhakikisha kila mtoto anapata elimu ya msingi, bado kuna baadhi ya watoto wenye umri chini ya miaka 14 walioajiriwa kwenye kazi za nyumbani, zinazowafanya kukosa haki ya kupata elimu
Picha: Mtandao
Pamoja na juhudi mbalimbali za serikali za kuhakikisha kila mtoto anapata elimu ya msingi, bado kuna baadhi ya watoto wenye umri chini ya miaka 14 walioajiriwa kwenye kazi za nyumbani, zinazowafanya kukosa haki ya kupata elimu

MSAIDIZI wa ndani ni hitaji la kila mwanamke ambaye yuko katika shughuli za kiuchumi. Pamoja na umuhimu huo, kuna utumikishaji mkubwa wa watoto chini ya miaka 18, umri ambao ni wa mtoto kuwapo katika mfumo wa elimu.

Licha ya serikali kuweka mazingira wezeshi kwa mtoto kusoma bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita, lakini uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwapo kwa changamoto hiyo katika miji na majiji.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi, anasema watoto saba hadi 10 walio chini ya miaka 14, husafirishwa kila mwezi kutoka wilayani Ngara kupelekwa jijini Mwanza kwa ajili ya kufanya kazi za ndani.

Anasema hali si nzuri hivyo kuwataka wadau pamoja na jamii kwa ujumla kushirikiana kwa karibu kuhakikisha hali hiyo inadhibitiwa, ili watoto hao wapate fursa ya elimu.

Mtoto mwenye umri wa miaka 12 (jina limehifadhiwa) mkazi wa Ngara mkoani Kagera, anasimulia namna ambavyo hakubahatika kwenda shule licha ya kuwa na matamanio hayo.

Anasema miaka miwili nyuma akiwa na miaka 10, alimwuliza baba yake sababu za kutokwenda shule kama watoto wengine anaocheza nao kila siku.

Tofauti na matarajio yake, majibu aliyopewa ni kwamba hakuna ambaye ataweza kumtafutia mahitaji ya shuleni wakati  chakula ndani ya familia yao upatikanaji wake ni shida.

“Niliambiwa nisubiri atakuja mtu kunipeleka mjini kufanya kazi za ndani. Baada ya siku tatu alikuja mgeni nyumbani kwetu, aliongeza na baba nikaambiwa nijiandae nakwenda mjini kufanya kazi za ulezi wa watoto na shughuli za ndani,” anasimulia mtoto huyo.

Binti huyo ambaye ni mwenyeji wa kijiji cha Kumnazi, kata ya Kanazi, anasema alipandishwa gari la kwenda Bukoba mjini na aliambiwa atapokewa na mwanamke ambaye ataishi naye huko. 

Naye binti wa miaka 14 kutoka Ukerewe mkoani Mwanza, mwenye simulizi tofauti na mwenzake, anasema alipomaliza shule ya msingi, wazazi wake walimwambia anakwenda mjini kufanya kazi ili awatumie fedha kijijini kwa sababu maisha yao ni duni.

“Changamoto ninayopata hapa ni muda wa kupumzika ambapo huwa ni usiku tu tofauti na nilivyokuwa nyumbani. Kazi zangu ni kufua nguo za familia nzima, kufanya usafi na kupika chakula,” anasema.

Binti wa miaka 15 ambaye mwaka huu alipaswa kuwa kidato cha pili, anasema aliacha shule akiwa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Lubugu, wilayani Magu na kukimbilia kuuza baa akiamini maisha yake yatakuwa bora.

“Wakati ninasoma mwalimu wangu alinipenda kutokana na bidii na utiifu, ghafla nikabadilika na  kutoroka nyumbani kutafuta kazi na ndipo nilipoangukia kazi ya uuzaji wa baa katika eneo la Ihayabuyaga, Magu,” anasimulia.

Binti huyo anasema changamoto anazokutana nazo kazini ni utumikishwaji kingono, kufukuzwa na wamiliki wa baa na wakati mwingine kukosa makazi, hivyo kulazimika kuzunguka mtaani na inapofika jioni kuomba hifadhi na nyakati nyingine hukosa chakula.

“Nyumbani hawajui changamoto ninazopitia. Wanajua  nimefanikiwa kupata kazi nzuri. Wakati mwingine baba uniomba fedha. Ninapitia wakati mgumu sana, ninatamani kurudi nyumbani, lakini ninaogopa mitaonekanaje” anasema.

Sara John (17) ambaye alitarajia kuwa kidato cha nne mwaka huu, anasema alikatisha masomo akiwa kidato cha pili baada ya kupata ushawishi kutoka kwa marafiki kuwa Dar es Salaam kuna nafasi nyingi za kazi, lakini alivyokwenda alikutana na hali tofauti na alivyoelezwa awali.

SHERIA INASEMAJE

Wakati watoto wakisimulia madhira yanayowasibu, Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 kifungu cha 9(1) imeainisha wajibu wa mzazi ikiwamo kumopatia mtoto haki ya kuishi, utu, heshima, mapumziko, uhuru, huduma za afya, elimu na malazi.

Lakini bado wazazi wamejificha katika kifungu kidogo cha (2) cha sheria hiyo kisemacho, haki hiyo itazingatia mwongozo na uwezo wa mzazi, mlezi au ndugu.

Mkazi wa Kijiji cha Minkoto mkoani Geita, Veronica Yombo, anasema tatizo la watoto hao kuishia kutumikishwa ni baadhi ya watu wa mjini kutumia kigezo cha umaskini wa familia za watoto hao kwa kuwarubuni kwa fedha na kuchukua mabinti zao wenye umri wa kwenda shule kufanya kazi za ndani.

Mkazi wa Bukoba mjini ambaye ni mwajiri wa mtoto kutoka Ngara (jina tunalo), anasema: “Ili kupata wasaidizi wa ndani, kuna wakati hutumia madalali, ndugu au jamaa wa dada hao. Pia wako wanaopita mtaani kuomba kazi kwa malipo ya siku.”

Anasema wadada wanaowapenda ni wenye umri mdogo chini ya miaka 18 kwa sababu sio wasumbufu katika kazi na wakiagizwa wanafanya.

Omary Ibrahim, mkazi wa Nyamagana jijini Mwanza, anasema suala la ajira kwa watoto ni jambo ambalo halifuatiliwi na kuchangia watoto kutumikishwa.

“Ukihitaji mfanyakazi unapiga simu au kutoa tangazo  mtandao unaletewa. Mara nyingi ninamwona mke wangu anaagiza na analetewa tunaishi nao japokuwa si wadogo, lakini changamoto huwa hatupajui kwao zaidi tunawasiliana na wazazi na ndugu zake kwa njia ya simu ninajua ni hatari," anasema.

Ofisa Ustawi Jamii wa Manispaa ya Bukoba, Japhet Kanoni, anakiri kupokea kesi za namna hiyo mara kwa mara hasa kwa watoto wanaokuwa wamepishana na waajiri wao kisha kufukuzwa kazi.

Anasema wanapohojiwa baadhi husema katika familia wanazotoka hazina uwezo kuanzia makazi, chakula na huduma nyingine muhimu.

Kanoni anasema kutambua kama binti wameajiriwa katika familia ni vigumu, hivyo huwatambua na kuwasaidia pale wanaposhindwana na waajiri wao na baada ya manyanyaso.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Minkoto iliyoko Chato mkoani Geita, Gilbert Kayena, anakiri kuwapo kwa tatizo hilo. Anasema wengi wao hukimbilia mijini wengine kwenda kufanya vibarua kama kulima na kuchunga ng’ombe.

“Tatizo hili lipo lakini siyo kubwa. Wazazi wameanza kuelimika na kujitambua, wawakubali kuwatoa vijana wao kwenda kufanya kazi mijini, mashambani au kuchunga mifugo,” anasema Kayena.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mikonto, Jerome Nestory, anasema kijiji hicho kinakabiliwa na uhaba wa shule na madarasa, huku kikiwa na idadi ya wakazi 8373 kati ya hao nusu ni watoto.

Anasema watoto hushindwa kuendelea na masomo kutokana umbali wa shule uliko au kutumikishwa katika umri mdogo.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Majengo Kata ya Mkolani jijini Mwanza, Ramadhani Musabi, anataja mbinu ya kutokomeza tatizo hilo ni kuwadhibiti madalali katika vituo vya mabasi na stendi, ambako ndio njia kuu ya kuwasambaza kwa ajiri.

IMEANDALIWA na Vitus Audax, Rose Jacob, Neema Emmanuel (MWANZA), Restuta Damian (BUKOBA), Judith Julius (NGARA).