MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imeutaka upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi wa kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JATU Public Limited, Peter Gasaya.
Hakimu Mkazi Mwandamizi Godfrey Mhini aliyasema hayo jana wakati kesi hiyo ilipotajwa, kisha upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Roida Mwakamele ukadai haujakamilisha upelelezi.
Baada ya kudai hayo, Wakili wa Utetezi Nafikile Mwamboma alidai kuwa, mara ya mwisho upande wa jamhuri ulitakiwa kuja kueleza hatua ya upelelezi ulipofikia na si kueleza upelelezi haujakamilika.
Wakili huyo alidai kesi hiyo ilishafutwa na kufunguliwa upya, hivyo ilipaswa kuanza kusikilizwa na si kuwa hatua ya upelelezi.
"Mahakama hii ina wajibu wa kusimamia mwenendo wake wa kesi, kusema jalada halijawafikia si sawa, tunaomba mahakama ifute shtaka na imwachie mshtakiwa," alidai Wakili Mwamboma.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Roida alidai jalada la kesi hiyo halijawafikia; ndio maana hawajui hatua ilipofikia.
Ndipo hakimu aliutaka upande wa jamhuri kuharakisha upelelezi. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 2, mwaka huu.
Katika kesi hiyo, Gasaya anadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 hadi Desemba 31, 2021, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, alijipatia Sh. 5,139,865,733 kutoka Saccos ya JATU kwa njia ya udanganyifu.
Ilidaiwa kwamba, alijipatia kiasi hicho cha fedha kwa madai kwamba atakizalisha kwa kuwekeza katika mazao ya kilimo na kupata faida zaidi, jambo ambalo alijua si kweli.
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kwamba, Gasaya alitakatisha fedha hizo zilizokuwa katika akaunti ya JATU iliyoko benki ya NMB tawi la Temeke, kwa kujihusisha katika miamala.
Ilidaiwa kuwa alifanya hivyo huku akijua fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Mwongozo wa Utendaji wa Mahakama unaelekeza kesi za kawaida zisikilizwe na kutolewa uamuzi ndani ya miezi sita tangu kufunguliwa kwake na kesi kubwa zisikilizwe kwa muda usiozidi mwaka mmoja.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED