MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeitaja Kampuni ya ‘Jubilee Health Insurance’ kama kiongozi kwa kupata mafanikio ya ukuaji kutoka asilimia moja 2023 hadi 22, mwaka huu.
Hayo yamebainisha na Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo katika kampuni hiyo, Wilbert Mweiro,wakati wa hafla ya uzinduzi wa mfumo mpya wa wateja, uliofanyika leo mkoani Dar es Salaam, akieleza kuwa malengo yao kwa mwaka ujao ni kukuwa angalau kwa asilimia 40 na kuwafikia watanzania wengi zaidi.
Pia amesema wamezindua mfumo ambao utawafanya watanzania kutokuwa na haja ya kufika katika matawi yao badala yake wataweza kupata huduma wakiwa eneo lolote nchini bila kuwa na haja ya kukutana na mtoa huduma wa kampuni hiyo.
“Mfumo huo utaondoa usumbufu kwa watu, ikiwemo mteja kumpa mtu asiemuamini fedha yake, kwa maana kwamba akishaingia kwenye mfumo atapatiwa maelezo ya kukamilisha usajili ikiwemo kuchagua huduma anayoitaka na kulipia moja kwa moja kupitia ‘control number’ bila fedha yake kupita kwa mtu,” amesema Mweiro.
Ameongeza kuwa mfumo huo utaongeza uaminifu kwa wateja wao ikiwemo kuwa na uhakika kwamba fedha anayoitoa inakwenda sehemu husika ambayo itamuwezesha kupata huduma stahiki bila kukutana na usumbufu.
Aidha, ameeleza kuwa mwaka jana walikuwa na mawakala 87, lakini mwaka huu mpaka Septemba wameongezeka hadi kufikia 140, na kwamba hispitali wanazofanya nazi hadi sasa ni 650.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED