MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, anatarajiwa kuzindua kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji, kesho katika Wilaya ya Ikungi.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ameyasema hayo leo Novemba 19, 2024 jijini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari, kuhusu hatima ya chama hicho kushiriki uchaguzi huo, uliopangwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.
Amesema akishafungua kampeni Ikungi, Lissu ataenda kuzindua Tarime, mkoani Mara keshokutwa.
Mbowe ametoa maelezo hayo baada ya kuhojiwa na waandishi wa habari kuhusu kauli ya Lissu, aliyoitoa hivi karibuni kwamba chama hicho kinapaswa kujipanga upya na uchaguzi, kwa kuwa hivi sasa hakikujiandaa vizuri.
“Makamu Mwenyekiti wetu alisema uchaguzi umevurugwa, ni kweli umevurugwa na kila mtu anaona na kusema hivyo, kila mwenye akili timamu anajua uchaguzi umevurugwa. Makamu Mwenyekiti hajawahi kusema tujitoe kwenye uchaguzi, kwa sababu anajua tulikubaliana nini kwenye vikao,” amesema.
Amesema: “Ndiyo sababu kesho anazindua kampeni Ikungi na keshokutwa yuko Tarime anazindua kampeni. Hii taarifa kwamba alitoa kauli uchaguzi umevurugwa, wamesema Maaskofu, Masheikh, Wanazuoni, Wanasiasa na hata waandishi wa habari.”
“Hakumaanisha tujitoe, alisema uchaguzi umevurugwa. Kwani nani anasema uchaguzi haujavurugwa. Na anazindua huko na wengine tutatawanyika kuzindua maeneo mengine,” amesema.
Amesema viongozi wakuu wa chama hicho, wamepangiwa kanda na maeneo tofauti na kila mmoja atatakiwa kufanya kampeni hizo.
Mbowe amesema hoja ya Lissu kutaka CHADEMA ijipange upya, ni sahihi kwa kuwa mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa maandalizi wa uchaguzi mwingine.
“Uchaguzi mmoja ukiisha unazaa mwingine. Mchakato mmoja ukiisha hukati tamaa, unajipanga upya. Ndicho anachomaanisha, sasa shida iko wapi?” alihoji.
Amesema chama hicho kiko imara na kwamba tofauti za mawazo miongoni mwa viongozi, haimaanishi mpasuko bali ni kuimarika kwa wanasiasa hao.
“Ukishakuwa na chama cha siasa kisichokuwa na minyukano hicho ni chama mfu. Siasa ndiyo ilivyo. Mkiona kwenye siasa mnakubaliana kila kitu kwa asilimia 100, hiyo safari hamtoboi,” amesema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED