RAIS Samia Suluhu Hassan amehutubia mkutano wa nchi tajiri zaidi duniani maarufu kama G20 na kuwaeleza kuwa Afrika bado inakabiliwa na viwango visivyo endelevu vya umaskini, njaa, magonjwa, utapiamlo na kuwa chini ya uzalishaji.
Akizunguma kwa mara ya kwanza kwenye mkutano huo jana, Rais Samia alisema vijana wengi wanakabiliwa na changamoto zinazochangiwa na migogoro na sera za kimataifa zinazoongeza uhaba wa chakula, kukandamiza ushindani na kupunguza ufikiaji wa masoko na teknolojia inayohitajika sana.
“Bado tuko kwenye dunia ambayo watu wengi wanangoja ahadi ya utandawazi ya mafanikio kutimizwa, huku wakibaki na matumaini kwamba mageuzi ya utawala wa kimataifa yataleta uwakilishi wa haki na upatikanaji wa rasilimali zinazohitajika kuondokana na umaskini,” alisema Rais Samia.
“Kama dunia itabaki kama ilivyo swali tutakalouliza mwaka 2030 halitakuwa 'tumeshindwa kwa kiasi gani kufikia malengo ya maendeleo ya milenia SDGs', bali 'ni watu wangapi zaidi dunia imewaacha nyuma kimaendeleo,” alisema
Alisema anaamini kuwa dunia yenye haki na endelevu itakuja wakati nchi zinazoendelea kama Tanzania zitapata usaidizi, rasilimali na uwakilishi unaohitajika ili kuendeleza maendeleo endelevu.
Rais Samia alisema pamoja na vikwazo vilivyopo Tanzania imeweza kufanya mageuzi makubwa ya kisera na kitaasisi pamoja na uwekezaji uliolengwa ili kubadilisha mifumo ya kilimo cha chakula.
Alisema asilimia 61.5 ya nguvu kazi ya Tanzania katika kilimo na juhudi zilizofanyika zilipandisha kiwango cha ukuaji wa sekta hadi asilimia 4.2.
Rais Samia alisema juhudi hizo zilileta viwango vya kujitosheleza kwa chakula hadi asilimia 128 na kupunguza viwango vya umaskini hadi asilimia 26.4 mwaka 2023.
“Licha ya hatua hizi, changamoto zinaendelea, ikiwa ni pamoja na uhaba wa mitambo na mbolea ila tunaamini kwamba kwa usaidizi unaolengwa, tunaweza kutumia uvumbuzi vyema zaidi, kujenga uthabiti na kuwezesha ukuaji wa maana na jumuishi,” alisema.
“Ombi langu mahususi kwa G20 hii ni kuhamishwa kwa SDR kwa Taasisi za Kifedha za Afrika kama vile AfDB,” alisema.
Alisema mbali na hitaji la mfumo wa upendeleo wa haki katika usanifu uliopo wa kimataifa wa fedha, Tanzania inataka mifumo zaidi ya msamaha wa madeni, misaada na mikopo yenye masharti nafuu ambayo inashughulikia mahitaji na udhaifu uliopo.
“Pia tunaunga mkono ushirikiano ulioimarishwa kama vile Muungano wa Kimataifa wa G20 dhidi ya njaa na umaskini ili kukuza uvumbuzi na ukuaji jumuishi,” alisema.
"Mkusanyiko wetu unazungumza juu ya dhamira yetu ya pamoja ya kutoondoka ulimwenguni kama ilivyo. Ni lazima tuongeze juhudi zetu maradufu, na turudishe ahadi zetu za kujenga ulimwengu wa haki, ustawi na haki,” alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED