MIAKA nane sasa wazee wa Zanzibar waliofikisha miaka 70 na kuendelea wanapata pensheni ya kujikimu ambayo hutolewa kila mwisho wa mwezi, ikijulikana kama pensheni jamii.
Zanzibar ni ya kwanza Afrika Mashariki kutoa pensheni jamii kwa wazee na nchi mbalimbali za Afrika Mashariki zinafika visiwani humo kujifunza namna ilivyofanikiwa kutoa fedha kwa wazee.
Baadhi ya wanafunzi waliokuja kusoma ni kutoka Kenya, Uganda na Rwanda.
Uamuzi wa kutunza wazee ulianza miaka nane iliyopita na awamu ya Dk. Ali Muhamed Shein, akiwapa wazee Sh. 20,000 kwa kila aliyefikisha miaka 70 na kuendelea.
Katika uongozi wa miaka minne ya Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameendelea kuwajali wazee, akienda mbali zaidi kwa kuongeza kiwango cha pensheni jamii kutoka Shilingi 20,000 hadi 50,000.
Kiwango hicho cha fedha kwa sasa kinatolewa kwa wazee 30,552 kati ya hao Unguja 18,105 na Pemba 12,447 waliosajiliwa ndani ya mpango huo.
Maono ya viongozi hao yanatokana na matamanio ya mwasisi wa Zanzibar Mzee Abeid Amani Karume ambaye ni kielelezo cha kuwajali na kuwaenzi wazee ambao tangu mwaka 1964 baada ya Mapinduzi hadi sasa wanalelewa katika nyumba maalum za serikali Unguja na Pemba.
Serikali ya Dk. Mwinyi inaendeleza jitihada za kuwahudumia na kuwatunza wazee wasio na ndugu wala jamaa katika makao maalum yaliyopo Sebuleni, Welezo kwa Unguja na Limbani kwa upande wa Pemba na jumla ya wazee 68 wanatunzwa katika maeneo hayo yaliyoanzishwa na Mzee Karume.
Mchanganuo wa wazee hao kati ya 68, wazee 38 wapo Welezo wakiwamo wanawake 13 na wanaume 25, Sebuleni 21 wanawake 13 na wanaume wanane kwa Unguja na kwa Pemba Limbani wapo wazee tisa wanawake watatu na wanaume sita.
Wote wanaendelea kupatiwa huduma za kiustawi ikiwamo chakula, mavazi, malazi, matibabu na fedha za kujikimu.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Riziki Pembe Juma, anasema serikali kwa kuona umuhimu na mchango mkubwa wa wazee katika kuleta maendeleo ya nchi iliongeza kiwango hicho cha pensheni jamii kutoka 20,000 hadi 50,000 sawa na asilima 150.
Anasema hatua hiyo ni miongoni mwa utekelezaji wa sera ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2014 ambayo inaeleza changamoto kubwa inayowakabili wazee ni ukosefu wa usalama wa kipato.
“Pensheni hii inawasaidia wazee kuimarisha maisha yao, ikiwamo kuanzisha shughuli mbalimbali za kujipatia kipato. Kuumarisha zaidi mpango huu, serikali imeandaa sheria ya kusimamia masuala ya wazee namba mbili ya mwaka 2020,” anasema Waziri.
Anasema sheria hiyo imeweka miongozo imara inayohakikisha wazee wanapatiwa pensheni kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na serikali inafanya kila juhudi kwa kushirikiana na jumuiya na mabaraza ya wazee katika ngazi za mkoa, wilaya na shehia ili kusimamia maendeleo ya wazee nchini.
Anasema hadi kufikia Agosti mwaka huu, mabaraza tisa ya wazee yalianzishwa katika ngazi ya wilaya kote Unguja na Pemba hivyo wilaya na shehia zote zimeshakuwa na vyombo hivyo vinavyojadili mafanikio na changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee katika maeneo yao.
Waziri Riziki anasema wazee waliopo katika vituo hivyo serikali inaendelea kuwapatia huduma zote za msingi wanazostahiki ikiwamo kuwasimamia, chakula, malazi, mavazi matibabu pamoja na posho.
Rais Dk. Mwinyi pamoja na kuongeza kiwango cha pensheni jamii kwa wazee, ameongeza pia pensheni kwa wastaafu wote kutoka shilingi 90,000 hadi 180,000 kwenye kiwango cha chini.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Sada Mkuya, anasema maamuzi hayo ya kuwa na penshen jamii yanaifanya Zanzibar kuwa pekee katika Afrika Mashariki inayotoa huduma hiyo.
Dk. Sada anasema ongezeko la pensheni kutoka Sh. 2000 hadi 50,000 kulikofanywa na Dk. Mwinyi kunatokana na uchumi na maisha kubadilika, akiona kuna haja ya kuongeza kiwango hicho kwa asilimia 150.
“Wazee wametoa mchango mkubwa kustawisha maisha na serikali, na ndipo Dk. Mwinyi alipotoa ahadi ya kwamba kila hali ya uchumi itakapoimarika na kiwango cha pensheni jamii kitaimarika pia,” anasema Waziri Sada.
Aidha anasema wakati pensheni hiyo ilipoanza kutolewa, wazee wakipewa mkononi fedha taslimu lakini kwa sasa wanalipwa kupitia benki na kwamba hatua hiyo ya kulipwa kidijitali inatokana na nchi kwenda na mageuzi ya kiuchumi na kimifumo ya kielektroniki.
Anasema mabadiliko yoyote lazima yatakuja na changamoto na mara ya kwanza kutoa fedha hizo kwa mfumo wa kibenki baadhi ya wazee hawakukubali lakini baada ya kuwapa elimu waliridhia.
WAZEE WANENA
Wazee wanaopokea pensheni jamii wanaishukuru serikali kwa kuendeleza maono ya muasisi wa mapinduzi katika kuwaenzi na hawakutegemea kuwa watakuwa wanapewa fedha ya kujikimu.
Juma Muhammed mkazi wa Kisauni anasema, “tunampongeza rais wetu kwa kutoa ruzuku hii bila ya ubaguzi kila aliyefikia kigezo cha miaka 70 anapata ruzuku hii ambayo inatusaidia sana.”
Mpango wa pensheni jamii umewasiadia kiuchumi na wazee walio wengi huzitumia fedha hizo katika shughuli ndogo za uzalishaji mali na kujiongezea kipato, anasema Muhammed.
Sinajambo Ame mkaazi wa Makunduchi, anasema fedha anayoipata ya pensheni jamii inampatia huduma mbalimbali hasa ikizingatiwa kuwa wazee wanamahitaji mengi.
“Tunaipongeza serikali maana kupewa pensheni jamii imesaidia hata kupunguza wimbi la wazee wanaombaomba mitaani hivi sasa tuna uhakika wa kupata pesa kila mwisho wa mwezi tunaiomba serikali iendelee na mpango huu,” anasema.
Maulid Nafasi Juma anasema wazee wa Zanzibar wanampongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuendeleza jitihada zilizoanzishwa na serikali ya awamu ya kwanza na kuahidi kuendelea kumuunga mkono katika kupambana na vitendo viovu ikiwamo ubadhirifu wa mali za umma.
Anasema pamoja na mipango mizuri ya serikali lakini bado wazee wanakabiliwa na baaadhi ya changamoto ikiwamo kubebeshwa tuhuma za uchawi ndani ya jamii.
Aidha, anashauri serikali kushusha umri wa wazee katika kupokea pensheni jamii badala ya miaka 70 iwe miaka 60 ili iweze kutoa fursa kwa wazee wengi zaidi kupata fedha hizo pamoja na kuanzishwa kwa dirisha maalum katika vituo vya afya kuwahudumia wazee popote walipo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED