USALAMA wa majengo yaliyoko Kariakoo, jijini Ilala umeibua jambo, wamiliki wake wako matumbo joto:
Rais Samia Suluhu Hassan amemwagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuongoza timu ya wakaguzi majengo kukagua majengo yote yaliyoko eneo hilo la kibiashara ili kujua hali ilivyo katika majengo hayo.
Alitoa maelekezo hayo jana wakati akizungumza na watanzania akiwa jijini Rio de Janeiro, Brazil ambako amekwenda kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Nchi Wanachama wa Kundi la G20.
Rais Samia pia ameliagiza Jeshi la Polisi kupata taarifa kamili kwa mmiliki wa jengo lililoporomoka jinsi ujenzi ulivyokuwa unafanyika.
"Baada ya zoezi la uokoaji kukamilika, ninamtaka Waziri Mkuu aongoze timu ya wakaguzi majengo waendelee na zoezi la kukagua majengo yote ya Kariakoo na kupata taarifa kamili ya hali ya majengo ya Kariakoo," Rais Samia aliagiza.
Alisema serikaki itahakikisha inatoa ushirikiano kuanzia mwanzo wa zoezi hili hadi mwisho na kwamba taarifa za uchunguzi zitakapopatikana, zitawekwa wazi na hatua zitakazochukuliwa na serikali zitawekwa wazi pia.
Mkuu wa Nchi alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa alizopewa, hadi kufikia saa 4:00 asubuhi watu waliokuwa wameokolewa ni 84 na kati yao, majeruhi 26 walikuwa wanaendelea na matibabu hospitalini na watu 13 wamefariki dunia kutokana na kuporomoka kwa ghorofa hilo.
Aliongeza kuwa serikali itagharamia matibabu na kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama, mashirika mbalimbali, wananchi na madaktari wanaowahudumia majeruhi.
MANUSURA ASIMULIA
Mmoja wa manusura wa tukio hilo, Hassan Yahya, ameelezea namna walivyotumia fimbo kuomba msaada wa kuokolewa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini, Yahya alisema kuwa katika eneo walikokuwa wamenasa, walibaini kuwapo upenyo wenye nafasi ndogo na hivyo wakawa wamebahatisha kupata fimbo ambayo waliitumia kuomba msaada.
“Mimi ni mfanyabiashara katika jengo lililoporomoka, na mpaka linadondoka, nilikuwa ghorofa ya katikati. Nikiwa humo, nilisikia mtikisitiko mkubwa, ghafla nikaona majirani zangu wanakimbia, ikabidi na mimi nikimbie kuwafuata, nikawaza kwamba kuna jambo haliko sawa.
"Wakati ninakimbia, wala sikufika mbali, tukawa tumekutana watu wengi kama 26, hivi kwenye hicho kieneo, kila mtu anataka kutoka, kila mtu analia, ikabidi tuteue viongozi wa kudhibiti hiyo hali, nikajiteua mwenyewe kuongoza.
"Tukaanza kuulizana kila mmoja na kuhangaika kutafuta sehemu hata kunakopatikana mwanga hata kidogo, tukafanikiwa kupata kiupenyo kidogo ambacho hata mkono hauwezi kupita, tukatumia kifimbo ambacho tulikiokota kukapenyeza hapo kuomba msaada kwa waokoaji, ndipo wakawa wametuona, wakaanza kuvunja ukuta.
"Tulikubaliana kwamba waanze watoto watolewe na mimi nilikuwa wa tatu mwishoni kutoka katika lile kundi letu, lakini wakati huo tulikuwa tunasikia na wenzetu upande mwingine wanaomba msaada," alisema Yahya.
Alisema kwamba alipopata uhakika wa kutolewa, yeye na wenzake wawili waliokuwa wa mwisho, walipiga picha na kisha kuituma kwa ndugu zao kuwataarifu kwamba wako hai.
Pia alisema kuwa baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini Muhimbili alikokuwa amepelekwa, alipokea simu nyingi za watu waliokuwa wamepata taharuki kwama amefariki dunia.
Akiwa eneo la tukio jana, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF), John Masunga, alisema waliwasiliana na baadhi ya watu ambao wako chini ya jengo hilo wakiwaambia kuwa wako salama.
Kamishna Masunga alisema kuwa baadhi yao walichukua hatua ya kugonga kuta kama ishara ya kuwaonesha mahali walipo ili wawapatie msaada.
"Pamoja na kufanikiwa kuwaokoa baadhi ya watu waliofukiwa na kuwapatia huduma ya Oksijeni, maji na glucose, tumekutana na changamoto nyingi, hivyo kulazimika kuvunja kuta mbilimbili hadi tatu ili kuwafikia walioko chini, tulitumia mbinu ya kutoboa mashimo kwa haraka ili tuwapatie huduma lakini pia kuwafikia," alisema Kamishna Masunga.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alitoa taarifa kuwa, watu 77 walikuwa wameokolewa huku watano wakifariki dunia.
Naibu Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Dar es Salaam, Renatus Mlelwa, alisema ameridhishwa na kazi kubwa inayoendelea kufanywa na timu ya wataalamu wa uokoaji.
Nipashe ilishuhudia ulinzi katika eneo hilo na maeneo mengi ya Kariakoo ukiwa umeimarishwa.
Vikosi vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Wananchi (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) vilikuwa vimetanda katika eneo hilo na eneo kubwa la Kariakoo kuimarisha ulinzi.
BALOZI NCHIMBI
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi alipongeza utayari na mshikamano uliooneshwa na watanzania baada ya tukio la kuanguka kwa jengo hilo, akisema kuwa hatua hizo zimeonesha uzalendo na moyo wa udugu uliojengwa ndani ya taifa.
Baada ya kutembelea eneo la tukio jana, Balozi Nchimbi alitoa pole kwa familia za waliopoteza maisha na kuwapa faraja waliojeruhiwa, huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano katika nyakati za dharura.
"Kwa namna ya pekee, ninapenda kutoa pole zangu za dhati kwa familia za wenzetu waliopoteza maisha. Maisha ya kila mtanzania yana thamani kubwa.
"Kwa walioumia, walioko hospitalini na hata waliotoka, tunawaombea uponaji wa haraka. Mwenyezi Mungu awajalie nguvu na afya njema ili mrejea katika shughuli zenu," alisema.
Katika hotuba yake, Balozi Nchimbi alipongeza serikali na vyombo vyake, hasa Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), pamoja na timu zake zikiongozwa na Waziri William Lukuvi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, na taasisi mbalimbali zilizoonesha mshikamano wa dhati katika kuhakikisha maisha yanaokolewa.
"Serikali inafanya kazi yake kwa ufanisi. Hiki ndicho tunachotarajia kutoka kwenye serikali za CCM—kuwa na uwapo wa karibu wakati wa matatizo. Ninawashukuru wote mnaoendelea kuwa hapa kushughulikia hali hii kwa ari kubwa," alisema.
Aliongeza kuwa juhudi za vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi binafsi na wadau wengine zinapaswa kupongezwa kwa moyo wa kujitolea.
"Uokoaji huu haupaswi kusimama. Kila maisha yanahesabika. Kama chama, tupo tayari kushirikiana ili kuhakikisha watu zaidi wanaokolewa," alisema Balozi Nchimbi.
*Imeandaliwa na Elizabeh Zaya na Thobias Mwanakatwe
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED