Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile Albano, amewaasa wastaafu watarajiwa wanaochangia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), kutopokea ushauri kutoka kwa watu wasiowajua.
Ameyasema hayo Novemba 18, 2024, jijini Arusha, wakati wa ufunguzi wa semina kwa wastaafu watarajiwa wanaochangia PSSSF wa mkoa wa Arusha yenye lengo la kuwaandaa wanachama wa Mfuko huo ili waweze kumudu maisha mapya ya ustaafu na waweze kutumia pesa zao vyema katika maeneo mbalimbali.
“Matapeli wanawasubiri kwa hamu, washauri pia, epukeni kupokea maelekezo kutoka kwa watu msiowajua, badala yake chukueni elimu mnayopewa hapa ili ikawaongoze namna bora ya kuishi baada ya kustaafu.” amefafanua Musa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uendeshaji PSSSF, Mbaruku Magawa, ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, amesema, mpango huo wa mafunzo kwa Wastaafu watarajiwa wa Mfuko hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuwaanda wanachama wa PSSSF wanaokaribia kustaafu waweze kutumia pesa zao vyema katika uwekezaji wenye tija ili kumudu maisha mapya ya ustaafu.
“Mafunzo haya yatalenga maeneo ya uwekezaji katika viwanda vidogo vidogo na vya kati, uwekezaji katika masoko ya fedha, kilimo biashara na ujasiriamali kwa ujumla.” amebainisha.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED