HATIMAYE Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amevunja ukimya kuhusu tuhuma zilizoibuliwa dhidi yake na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, akimtaja hadharani kwamba ndiye kiongozi wa umma aliyeongoza kikosi cha wasiojulikana waliomshambulia kwa nia ya kumuua miaka saba iliyopita.
Makonda kwa mara ya kwanza alitoa ufafanuzi hadharani jana, akijibu tuhuma hizo, huku akihoji Lissu ana uhakika gani kuwa shambulio hilo aliliongoza.
Ni wakati akiwajibu waandishi wa habari waliomwuliza maswali wakati wa utoaji ripoti ya miezi sita ya uongozi wake, hafla iliyohudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini na kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni vya kitaifa.
Makonda alisema amemshangaa Lissu kwa nini hadi jana alikuwa hajaenda mahakamani kwa kuwa ni zaidi ya miaka saba sasa tangu shambulio hilo kutokea (Septemba 2017).
"Lissu anavyonituhumu kuwa mimi nilihusika kumpiga risasi, si (tuhuma) za kweli hata kidogo, badala yake anatafuta huruma kwa wengine, yaani mimi Makonda hata mgambo sijaenda, ninaanzaje kufanya haya na sipendi kuhangaika kumjibu Lissu na mjue hakuna Rais anayeweza kuunda kikosi na kutenda mambo yasiyofaa, hakuna," alisema.
Makonda pia alizungumzia kwa mara ya kwanza hadharani tuhuma za kuvamia studio za Clouds Media, akisema anawashangaa waandishi wa habari hadi jana walikuwa hawajawahi kumhoji Dk. Harrison Mwakyembe kuhusu kilichomo katika ripoti yake ya uchunguzi wa tukio hilo.
Alisisitiza kuwa akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alikuwa na urafiki mkubwa na wamiliki na wafanyakazi wa chombo hicho cha habari, hata kuwanunulia magari na baadhi ya vifaa vya kazi, hivyo tuhuma dhidi yake kuvamia studio zao si za kweli.
Kuhusu utendaji kazi ndani ya miezi sita mkoani Arusha, Makonda alisema kuwa katika sekta ya utalii, mapato yameongezeka na kufika trilioni 2.7 huku magari ya utalii baada ya filamu ya Tanzania The Royal Tour yakiongezeka, yakiwamo yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufikia Sh. bilioni 336 tangu Rais Samia alipoingia madarakani.
Alisema hospitali nne mpya za wilaya zimejengwa na tatu kukarabatiwa huku idadi ya watoa huduma za afya ikiongezwa ili kuondoa changamoto kwa wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya huku vifo vya kinamama vikipungua sambamba na vya watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Alisema wameimarisha pia huduma za maji, ulinzi na usalama na kwamba Desemba Mosi mwaka huu, Rais Samia Hassan Suluhu anatarajia kukutana na viongozi wa kimila jamii ya Wamasai na viongozi wengine muhimu ili kujadili mustakabali wa wananchi wanaoishi wilayani Ngorongoro na kutoa majibu sahihi.
Akizungumzia kuhusu kuenguliwa kwake kwa nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Makonda alisema, "Nilipoenguliwa kutoka Katibu Siasa na Uenezi Taifa ulikuwa ni usiku mkubwa na wenye mawazo kuwa nikiwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha nitafanyaje, sababu nilianza kusahau, lakini nilipofika Arusha, nimekutana na watu wakarimu, wenye bidiii za kufanya kazi na kutafuta fedha."
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED