Doris Mollel Foundation yazindua mtandao wa familia za watoto njiti

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 11:09 AM Nov 18 2024
Doris Mollel Foundation yazindua mtandao wa familia za watoto njiti

KATIKA kilele cha Siku ya Mtoto Njiti, kilichohitimishwa jana Novemba 17, 2024 Taasisi ya Doris Mollel Foundation imezindua Mtandao wa Familia za Watoto Njiti nchini ili kutoa elimu, msaada na kuhamasisha jamii kuhusu changamoto zinazowakumba watoto njiti ili kukuza uelewa.

Mtandao huo utawaleta wazazi na familia za watoto njiti kushirikiana, kubadilishana uzoefu na kupewa msaada wa kitaalamu katika huduma za afya, hasa katika muktadha wa huduma bora kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.

Akizundua mtandao huo jana Jijini Dar es Salaam, tukio lililotanguliwa na mafunzo kwa waandishi wa Habari juu ya kuandika habari za watoto njiti, Dk. Bingwa wa Watoto na Mjumbe wa Bodi ya taasisi ya Doris Mollel Foundation, Albert Chota alisema lengo lingine la mtandao huo ni kuisaidia serikali kupunguza vifo na kuielemisha jamii juu ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti).

Alisema ni wajibu wa serikali kuongeza idadi ya wahudumu wa afya, ambao wataisadia kuokoa maisha ya watoto njiti, akitolea mfano kuwa na uwiano wa ‘mtoto njiti mmoja, muuguzi mmoja.

"Kwa kupitia Mtandao huu, familia zitapata taarifa muhimu kuhusu jinsi ya kushughulikia afya na ustawi wa watoto wao njiti, ikiwemo huduma za mapema na uangalizi wa afya kwa watoto hao. Doris Mollel, ambaye pia alikulia kama mtoto njiti, alisisitiza umuhimu wa jamii kuwa na uelewa mkubwa kuhusu changamoto hizi na kuhamasisha serikali pamoja na wadau wa afya kutoa msaada wa kutosha" alisema.

Alisema kuwa mtandao huo pia utaongeza ufanisi wa kupunguza vifo vya watoto njiti kwa kutoa vifaa vya afya na msaada wa kiufundi kwa vituo vya afya na hospitali mbalimbali nchini.

"Juhudi hizi ni sehemu ya malengo ya taasisi ya Doris Mollel Foundation ya kuboresha huduma za afya na kusaidia familia za watoto njiti kuwa na ufahamu na msaada unaohitajika.

Dk.Chota pia aliiomba serikali kuingilia kati suala la gharama za kuwahudumia watoto njiti hospitalini, ambapo gharama hizo zimekuwa kikwazo kwenye mapambano ya kupunguza vifo vitokanavyo na uangalizi mfinyu wa watoto hao.

Awali, mwakilishi kutoka taasisi hiyo, Dk. Sylvia Ruambo akimuwakilisha muasisi wa taasisi hiyo, Doris Mollel, alisema katika mafanikio ya miaka tisa waliyoyapata tangu kuanzishwa kwake, tayari wamezifikia hospitali 85 nchi nzima katika kuchangia vifaa tiba kama mashine za kupumulia, vitanda n.k, vyenye thamani ya zaidi ya bilioni 1.5.