Ushiriki wa wadau waongeza ufanisi wa mahakama Kahama

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 07:14 PM Jan 13 2025
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama, Edmund Kente.
Picha: Shabani Njia
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama, Edmund Kente.

Ushiriki wa wadau wa Mahakama Wilayani Kahama, Shinyanga, umetajwa kuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha utendaji kazi wa mahakama hiyo kwa kuhakikisha kesi zinashughulikiwa kwa haraka na ufanisi zaidi. Hatua hii imepunguza muda wa kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi nyingi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama, Edmund Kente, alieleza hayo jana wakati wa kikao na wadau wa mahakama hiyo. Kikao hicho kilikuwa sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria, ambapo aliwahimiza wananchi kutembelea mahakama ili kujifunza zaidi kuhusu shughuli zake.

Kente alisema ushiriki wa wadau mahakamani, hasa wananchi, umeongeza kasi ya utatuzi wa mashauri kwa kutoa ushahidi wa kutosha, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo kesi nyingi ziliishia njiani kwa kukosa ushahidi.

“Wadau wetu wakuu ni wananchi. Wananchi wanapopata changamoto za kisheria, wanapaswa kujua mahali pa kukimbilia kupata haki. Kaulimbiu yetu mwaka huu inalenga maendeleo ya utatuzi wa mashauri ya madai, tukizingatia haki na maendeleo,” alisema Kente.

Kwa upande wake, mdau wa mahakama, Boke Matiko, alisema uoga wa wananchi kushiriki kwenye shughuli za mahakama na kutoa ushahidi unatokana na dhana potofu kwamba wakikosea watachukuliwa hatua za kisheria. Alisisitiza kuwa elimu ya sheria inahitajika ili kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu.

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu: “Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi Zinasimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.” Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuanza Januari 25 na kumalizika Februari 3, yakilenga kuashiria kuanza rasmi kwa shughuli za mahakama.