‘Tuondoe vikwazo vya rufani za tiba’

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:17 AM Aug 31 2024
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa
Picha: Mtandao
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ametaka watoa huduma za afya wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuondoa vikwazo vinavyozuia wagonjwa wanaotafuta matibabu ndani ya ukanda huo.

Amesema nchi wanachama ikiwamo Tanzania zimejitahidi kuwekeza katika sekta ya afya na kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje ya kanda kwa matibabu.  

Majaliwa alisema hayo jana alipokuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa 12 wa Shirikisho la Watoa Huduma za Afya Afrika Mashariki uliofanyika katika Kituo  cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Njerere (JNICC), Dar es Salaam.  

"Hatua hii ni kwa manufaa ya wananchi wetu na kwa uchumi wa kikanda na ukuaji wa utalii tiba. 

"Kwa sasa ni wagonjwa wachache sana wanaosafiri nje ya nchi zetu kwa ajili ya matibabu, kwani karibu magonjwa yote makubwa sasa yanaweza kutibiwa ndani ya Afrika Mashariki,” alisema. 

Katika hatua nyingine, Majaliwa alitoa wito kwa wawekezaji wa sekta ya afya kuwekeza nchini Tanzania. 

Alisema serikali imetengeneza sera rafiki za uwekezaji hususan katika Sekta ya Afya kutokana na uhitaji wa huduma hizo nchini. 

"Tunawakaribisha wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya afya, Sera nzuri tunazo, Sheria na kanuni nzuri tunazo, mahitaji ya uwekezaji kwenye sekta ya afya ni makubwa na tunataka tupate teknolojia mpya na huduma za kibingwa," alisema.  

Pia aliwataka wadau wa afya wa kanda kujadili mbinu mbalimbali za kuimarisha mifumo ya afya na kuwa na mikakati ya pamoja ya kukabiliana na magonjwa. 

"Tumieni jukwaa hili kuweka mikakati ya pamoja ya kupambana na magonjwa ya mlipuko, magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ambukiza pamoja na magonjwa mapya yanayotokana na mabadiliko ya hali ya tabia nchi," alisema.

 Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, alisema uwekezaji uliofanywa na serikali kuanzia ngazi ya chini  umewezesha ugunduaji wa magonjwa yakiwa katika hatua za awali. 

"Rufani kwenda nje ya nchi zimepungua kwa kiasi kikubwa kipindi cha nyuma watu waliokuwa wanafika Ocean road walikuwa kwenye hatua za mwisho za ugonjwa, lakini kutokana na uwekezaji sasa zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wanakuja wakiwa na magonjwa katika hatua za awali," alisema.