Silaa aahidi ushirikiano na vyombo vya habari

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 10:39 AM Nov 19 2024
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa.
Picha:Mtandao
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa.

WIZARA ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeahidi ushirikiano na wadau mbalimbali wa sekta hiyo ikiwamo vyombo na wanahabari, ili kuhakikisha mazingira rafiki wakati wa utekelezaji wa majukumu kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Jerry Silaa, wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya habari, alisema anatarajia Novemba 21, mwaka huu, kukutana na Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa, ambao ndani kuna taasisi 16 kujadili masuala mbalimbali ya kisekta.

Alisema baadaye atakutana pia na taasisi moja kati ya 1,023 za nchini, akieleza kuwa sekta ya habari ni mtambuka na inasimamiwa na sera, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ambazo katika utekelezaji wake wanahabari wanafurahia haki na uhuru wa kupata na kupasha habari bila kuwa na woga wa kijinai.

"Kutokana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, Septemba 14, mwaka huu, nimeteua pia wajumbe sita wa bodi itakayosaidia masuala mbalimbali katika sekta hii, na hii itatufungulia safari ya kuanzisha meza huru na mfuko wa tathmini ya uchumi kwa wanahabari. 

"Pia wizara inaendelea kuratibu uendeshaji wa mchakato wa maboresho ya sera ya habari, haya ni kati ya masuala ya msingi yanayokwenda kuboresha sekta ya habari nchini, ili kukamilisha jukumu la wanahabari kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi na kwa wakati, na kuwa huru kwa mujibu wa sheria," alisema Silaa.

Aliongeza kuwa Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa katika suala la amani na kuimarisha mshikamano na umoja wa kitaifa kwa mchango wa vyombo vya habari.

"Niwaahidi sisi ni familia moja, niko karibu nanyi, milango yangu iko wazi karibuni tujenge sekta yetu," alisisitiza Silaa.

Aidha, alisema ni dhamira yake kuhakikisha wanafanya mapinduzi katika sekta ya habari, na kwamba wameanza na sera na sheria, pamoja na kuendelea kuvisikiliza vyombo mbalimbali kukaa kuzungumza na kubadilishana uzoefu ili kuifanya sekta hiyo kuwa bora zaidi.

Rais wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzani (UTPC), Kenneth Simbeye, alitoa mapendekezo ya umoja huo kuelekea uchaguzi wa Serikali ya Mitaa na Uchaguzi Mkuu, kwamba vyombo vya habari viwezeshwe kutekeleza wajibu wao kwa weledi bila kubugudhiwa, na waandishi kuachwa watimize majukumu yao kwa kuzingatia kanuni na miongozo ya kitaaluma.

Alishauri chombo cha habari kisibaguliwe kwa mtazamo wa kidini au siasa, waandishi waheshimiwe, pamoja na wasimamizi wa vyombo hivyo wasimamie kwa usawa bila kujali kwamba ni cha serikali au binafsi.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, alisema kuelekea uchaguzi watahakikisha wanatimiza wajibu wao wa kusimamia sheria na kutengeneza mazingira ya amani na kuzuia viashiria vya uhalifu kabla havijatokea.

Alisema lengo la Jeshi la Polisi sio kutekeleza majukumu hayo kwenye uchaguzi pekee bali hata baada ya uchaguzi na kwamba watahakikisha usalama wa wagombea wakati wa kampeni, wapiga kura na hata katika hatua ya kuhesabu kura.

"Wajibu wetu pia ni kuweka ushirikiano mzuri na vyombo vya habari wakiwamo waandishi wa habari. Pia tutawaandaa askari kwa nadharia na vitendo lengo ni kuwezesha uchaguzi kufanyika kwa amani na usalama," aliahidi Misime.