RAIS Samia Suluhu Hassan amemwahidi Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, kuendeleza ushirikiano na taifa hilo katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na wa kibiashara.
Kupitia ukurasa wa X, Rais Samia alimpongeza Trump kwa ushindi huo na kuahidi kuendeleza ushirikiano wa pamoja kati ya Tanzania na nchi hiyo kwa maendeleo ya wananchi wake.
“Kwa niaba ya serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatuma pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Donald Trump, Rais Mteule wa Marekani kwa ushindi wako katika uchaguzi.
Mheshimiwa Rais Mteule, ninakutakia kheri. Ninatumaini kushirikiana nawe kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Marekani,” alimwahidi Trump.
Rais wa Kenya, William Ruto, alisema jana kuwa nchi yake iko tayari kuimarisha ushirikiano kwenye biashara, uwekezaji, teknolojia na ubunifu, amani na usalama na maendeleo endelevu.
Alisema nchi hiyo inathamini ushirikiano wao wa muda mrefu uliodumu kwa miaka 60 na kujengwa misingi, demokrasia, maendeleo na kuheshimiana.
Rais Ruto alisema anatarajia kuimarisha ushirikiano huo kwa kufanya kazi kwa pamoja kukabiliana na changamoto za kimataifa, kukuza amani na usalama na kuendeleza ukuaji wa uchumi shirikishi kwa manufaa ya wananchi.
“Kenya iko tayari kuimarisha ushirikiano wetu katika masuala ya maslahi ya pamoja kama biashara, uwekezaji, teknolojia na ubunifu, amani na usalama, na maendeleo endelevu,” alisema.
Rais wa Rwanda, Paul Kagame, alisema anatarajia kushirikiana na Rais Trump kwa miaka ijayo kwa faida ya wananchi wa nchi hizo.
“Ujumbe wako umeweka wazi kuwa Marekani inapaswa kuwa mshirika wa uchaguzi unaovutia kwa mfano wake, badala ya kulazimisha mitazamo na njia zake za maisha kwa wengine,” alisema.
Katika kinyang’anyiro cha urais wa Marekani, Trump alimshinda Kamala Harris, mgombea wa Democrat kwa kupata kura za wajumbe maalum 294, ambao ni 24 ya wajumbe 270 wanaotakiwa kupata ushindi.
Alimshinda majimbo muhimu kama Pennsylvania, Georgia, North Carolina na Wisconsin.
Wafuasi wake wanamchukulia Rais huyo mteule kutoka Chama cha Republican kama mwokozi na shujaa, aliyekuwa tayari kutetea maadili yao dhidi ya wanamageuzi nchini Marekani.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED