WAGOMBEA 30 wa nafasi Uenyekiti kupitia Chama cha Wananchi( CUF) katika Wilaya ya Kinondoni wameenguliwa kugombea nafasi hiyo kwa madai ya kushindwa kujaza anuani kwenye fomu za kugombea.
Nipashe Digital imeshuhudia hali hiyo katika ofisi mbalimbali za mitaa zilizopo Wilaya ya Kinondoni, ikiwamo Bwawani, Sindano, Kisiwani, Mpakani A na Mpakani B.
Majina yaliyobandikwa yanaonesha hakuna wagombea wa vyama vya upinzani waliopita katika ya nafasi ya Uenyekiti, wajumbe wa kamati ya mtaa katika kundi mchanganyiko na kundi la wanawake.
Nipashe Digital imezungumza na Katibu wa CUF Wilaya ya Kinondoni, Mbaruku Kombo Mhina, na ameeleza kusikitishwa wagombea wake kuenguliwa kwa kigezo cha kushindwa kujaza anuani kwenye fomu za kugombea nafasi hiyo.
Amesema Chama kilisimamisha wagombea 120 kugombea nafasi za uongozi ikiwemo ya Uenyekiti wa Mtaa, wajumbe wa kamati ya mtaa katika kundi mchanganyiko na kundi la wanawake.
Amebainisha kuwa CUF walishiriki nafasi ya Uenyekiti katika kata 13 kati ya 20 za Wilaya ya Kinondoni, na wajumbe katika Mitaa 106 ya wilaya hiyo ambapo kila mtaa walikuwa watano.
“Hii sio taswira nzuri, inatupa picha kwamba uchaguzi unaokuja hautakuwa huru wala wa haki,”amesema Mhina.
Miongoni mwa walioenguliwa kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Mtaa wa Kisiwani kwa chama cha Wananchi( CUF) Hussein Rashid Dimoso, amesema ameenguliwa kwa sababu ya kutojaza anuani.
Amesema ni mara ya tatu kugombea nafasi za uongozi wa Serikali za mitaa kuanzia mwaka 2014, 2019 na mara zote hizo hakujaza anuani lakini alifanikiwa kuwa kiongozi.
Hata hivyo wagombea wa Chama cha Mapinduzi wamechaguliwa kugombea nafasi mbalimbali za Uenyekiti, nafasi ya wajumbe wa kamati ya mtaa katika kundi mchanganyiko na kundi la wanawake wamepita majina yakibandikwa katika ofisi mbalimbali za Serikali za mitaa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED