MBUNGE wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina amemaliza adhabu yake ya kutohudhuria vikao 15 bungeni, akiwa na hoja tano, ikiwamo kutaka mkataba kati ya serikali na kampuni ya DP World uwasilishwe bungeni.
Vilevile, mbunge huyo ameandaa maoni kuhusu masuala ya kodi yenye kurasa 50 ili kuyawasilisha kwa Tume ya Maboresho ya Mifumo ya Kikodi.
Hoja zingine zinazohusiana na utekelezaji mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia (LNG), kutokamilika kwa wakati Mradi wa Bwawa la Uzalishaji wa Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP) na utaratibu wa usafirishaji mizigo uliosababisha wafanyabiashara kukosa nyaraka.
Akichangia bungeni jana mjadala wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa na Maandalizi ya Bajeti kwa Mwaka 2025/26, Mpina alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunda tume hiyo na kwamba pamoja na kuwa alikuwa "mapumziko", ameandaa kurasa 50 atakazowasilisha kwa tume hiyo namna nchi inavyopoteza mapato.
"Kwa muda mrefu tumeongelea hili bungeni, ninaamini matokeo ya hiyo tume yataleta mageuzi makubwa sana katika ukusanyaji mapato nchini. Hongera sana Rais kwa kuliona hili.
"Na mimi kwa kulichukulia uzito jambo hili, pamoja na kuwa nilikuwa mapumzikoni, tayari nimeandaa kurasa 50, nitapeleka tume, kurasa zimezungumzia maeneo mbalimbali nchi inavyopoteza mapato," alisema.
Mpina, akizungumzia suala la mkataba wa DP World na serikali, alisema walikubaliana mikataba ya aina hiyo kupelekwa bungeni na kwamba ilielezwa mwekezaji atawekeza Dola milioni 250 kwa miaka mitano na kudai kuwa mwekezaji huo ameanza kukusanya kodi.
"Tulikubaliana hapa bungeni mikataba hii mikubwa, yote mitatu, italetwa kwenye hili Bunge ili tujue kilichokubalika ndani ya mikataba hiyo, lakini Sheria yetu ya Rasilimali za Asili inasema mikataba yote ya rasilimali iletwe bungeni, ninaendelea kuuliza hivi imeshindikana nini kuleta mikataba ya Bandari ya Dar es Salaam tuliyoingia na DP World bungeni?" Mpina alihoji.
Kuhusu Bwawa la Mwalimu Nyerere, Mbunge Mpina alisema mradi huo tayari uzalishaji umeanza na megawati 740, lakini haijulikani huo mradi unakamilika lini ili kupata megawati zote 2,115.
"Tuliwaahidi wananchi kwamba umeme huu ni umeme wa bei nafuu, hatujaambiwa kwenye mpango huu unafuu wa mradi, tuliahidi kushusha umeme kwa wananchi wetu, na hatujaambiwa ni nchi ngapi tumeingia nazo mkataba wa kuziuzia umeme, na umeme utashuka kwa gharama kiasi gani ili wapate wananchi na wawekezaji kwa bei nafuu," alisema.
Mpina alisema kuwa katika mradi wa LNG, mazungumzo yamekuwa ya muda mrefu na kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Ralisimali za Asili, mikataba ya aina hiyo inapaswa kupelekwa bungeni na kuhoji mazungumzo hayo yatakuwa ya muda gani kwa kuwa inatakiwa utekelezaji wa mradi uanze kwa haraka ili nchi inufaike.
Mbunge huyo alisema kuwa katika mkataba wa usafirishaji mizigo wa kuchangia makasha kwa wasafirishaji mizigo tofauti, sheria ya usafirishaji huo ilibadilishwa sambamba na kanuni zake.
"Ilifika mahali msafirishaji wa mizigo anasafirisha na majina ya nyaraka zote yanaandikwa kwa jina lake, lakini tukapata matatizo ya wafanyabiashara wengi kukosa nyaraka za ulipaji kodi kwa sababu majina yameandikwa ya msafirishaji, mwisho wa siku wananchi wakashindwa kuuza bidhaa kwa kutoa risiti na wakashindwa kutumia EFD na migomo ikatokea kule Kariakoo," alisema.
Alisema hali hiyo imesababisha fedha nyingi kupotea na kushauri kampuni (jina tunalo) ambayo kwa miaka mitano imefanya kazi hiyo na inapofika kwenye kutoa mizigo nyaraka hazionekani.
"Naomba ufanyike ukaguzi wa kiuchunguzi kuchunguza kampuni ya... (alitaja jina la kampuni) kwa miaka mitano ili kubaini kodi iliyopotea ili kampuni ilipe hasara hiyo kwa serikali," alisema.
Hapo Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, aliomba kuzungumzia mkataba wa bandari ambao Mpina anataka upelekwe bungeni, akidai hakuna kodi yoyote inaruhusiwa kukusanywa na taasisi yoyote isiyo ya serikali.
"Na kwa mantiki, alilokuwa analiongelea la DP World, hakuna kodi yoyote DP World wanakusanya. Kodi zote ambazo zinakusanywa bandarini, zikiwapo import duty, excise duty, VAT, kodi ya reli, zote... custom processing fee, zote zinakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
"Na kimsingi, baada ya DP World kuanza shughuli zile ambazo zimeongeza ufanisi bandarini, kodi inayokusanywa na TRA imeongezeka na kufikia Sh. trilioni 1.23, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa tangu TRA ianzishwe," alisema waziri huyo.
Waziri Mwiguli aliendelea kusema, "Kwa maana hiyo, kauli aliyotoa Mbunge wa Kisesa kwamba DP World wameanza kukusanya kodi ni ya uongo na imelenga kulipotosha Bunge na watanzania na kama hajafanya kwa makusudi, ninaomba afute kauli hiyo," alisema.
Akitoa majibu kuhusu hoja hiyo ya Waziri Mwigulu, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, alimwita Mpina, naye katika maelezo yake alisema: "Wakati ninachangia, kama nilitumia neno kodi, nilimaanisha tozo zinazokusanywa na DP World, sasa baada ya kuwa imekabidhiwa tangu Aprili 2024, kama nimetumia neno ‘kodi DP World imekusanya', ninalifuta kwenye kumbukumbu sahihi za Bunge na mimi nilimaanisha tozo ambazo sasa hivi wanakusanya DP World."
Naibu Spika alielekeza kufutwa kwa maneno yanayoleta upotoshaji kwenye kumbukumbu za Bunge na kuwataka mawaziri kutolea ufafanuzi papo kwa papo wanapoona kuna jambo litasababisha ukakasi kwa umma.
Naye Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Prof. Sospeter Muhongo alisema kuna fursa za ajira nje ya nchi na kuwataka Watanzania wasing’ang’anie kupata kazi nchini.
"Marekani wanataka wataalamu, Ulaya wameanzisha blue card, watahitaji watu, nchi kama Ujerumani inahitaji wataalamu wa sekta sita za masuala ya afya, uhandisi, ujenzi, kilimo, misitu na Ufaransa inahitaji wataalamu kwenye maeneo 23, sasa Watanzania tusing’ang'anie kazi nchini," alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED