Mwalimu adaiwa kumlewesha mwanafunzi kisha kumbaka

By Restuta Damian , Nipashe
Published at 01:20 PM Nov 08 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda.

MWALIMU wa taaluma katika Shule ya Msingi Rulanda, wilayani Muleba, mkoani Kagera, anatuhumiwa kumbaka na kumnywesha vitu vinavyodhaniwa kuwa dawa za kulevya, mhitimu wa darasa la saba aliyefika shuleni huko kufuatilia matokeo yake ya Mtihani wa Taifa mwaka huu kisha kumnajisi.

Akisimulia tukio hilo juzi nyumbani kwao, binti huyo mwenye umri wa miaka 13 (jina tunalo), alidai kuwa Oktoba 30 mwaka huu, saa tisa alasiri, alikwenda shuleni huko kufuatilia matokeo yake.

Alidai kuwa akiwa shuleni huko, alikutana na mwalimu huyo (jina tunalihifadhi) kwa lengo la kuangalia matokeo yake. Naye (mwalimu) alimweleza kuwa amepata Daraja "D".

Msichana huyo alidai kuwa baada ya kupewa matokeo yake, mwalimu huyo alimtaka arudi shuleni huko saa 10 jioni ili kumpatia ushauri kutokana na kuwa na matokeo yasiyoridhisha.

Alidai akiwa kwenye moja ya madarasa, alikokuwa anasoma baada ya kuitikia wito huo, mwalimu huyo alifika na kufunga mlango na madirisha na kumtaka avue nguo.

Mwanafunzi huyo alidai kuwa mwalimu huyo alimpaka vitu sehemu mbalimbali za mwili na baada ya hapo, akapoteza fahamu na alipozinduka, alimwona mwalimu akichungulia dirishani na kumtaka aondoke.

Mama wa mtoto huyo (jina tunalo) alidai kuwa ilipotimu saa 11 jioni siku hiyo pasi na kumwona mwanawe, alikwenda shuleni kumtafuta bila mafanikio.

Alidai kuwa ilitimu saa 1:30 jioni, mwanawe alirejea nyumbani na walipomhoji, alidai mwalimu wake alimfungia ndani na kumziba mdomo asipige kelele na kumpaka dawa.

Mama huyo alidai kuwa alipomchunguza mwanawe, alibaini alikuwa ameingiliwa kimwili kutokana na kuwa na michubuko sehemu za siri.

"Tulikwenda Kituo cha Polisi Muleba tukapewa PF3 (Fomu Na. 3 ya Polisi) kwa ajili ya kwenda hospitali kufanyiwa vipimo ndipo tulipompeleka Kituo cha Afya Kaigara kwa ajili ya huduma za kitabibu na baada ya hapo, tuliambiwa mtuhumiwa amekimbilia kusikojulikana," alidai.

Mama huyo aliendelea kueleza kuwa baada ya siku kadhaa, ndugu wa mwalimu huyo waliojitambulisha kama kaka na rafiki yake, walifika nyumbani kwake wakiomba suala hilo limalizwe kifamilia ili mtuhumiwa arejee kazini, lakini alikataa ombi hilo.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Lameck Jonas, alikiri kuwa na taarifa za tukio hilo, akieleza kuwa alipokea simu ya Ofisa Mtendaji wa Kata kuwa mzazi wa mtoto ameripoti kuhusu mtoto wake kufanyiwa ukatili huo.

"Kwa taarifa ambazo nilipokea ni kwamba, siku ya tukio hilo, pikipiki ya mwalimu ilionekana mazingira ya shuleni na siku hiyo hakukuwa na programu ya kufundisha jioni kwa sababu madarasa ya mitihani yamekwisha," alisema.

Diwani wa Rulanda, Evance Ernest, alisema alipokea taarifa hiyo kutoka kwa Ofisa Elimu Kata kwamba, amepokea hati kutoka Jeshi la Polisi iliyopelekwa kwake baada ya wazazi wa mtoto kupewa PF3 kwa ajili ya matibabu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Isaya Mbenja, alisema taarifa za ukatili huo amezipokea na katika maadili ya kazi, kuna tume ambayo husimamia nidhamu ya walimu.

Alisema halmashauri itaendelea na hatua ya kupelekwa taarifa za tuhuma hizo ili mamlaka zianze kufanya ufuatiliaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda, alitafutwa na Nipashe kwa njia ya simu kuzungumzia tukio hilo, akidai kuwa alikuwa nje ya ofisi kikazi. Aliahidi kuzungumzia suala hilo akiwa ofisini baada ya kupata taarifa kamili.