SADC yaweka mikakati miundombinu ya nishati

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 08:00 PM Oct 15 2024
Naibu Katibu Mkuu Nishati, Khatibu Kazungu (kushoto) akipokea mfano wa picha wenye Ramani inayoonyesha mfumo wa umeme nchi za kusini ya Afrika, kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bwawa la Nguvu Kusini mwa Afrika (SAPP), Stephen Dihwa (kulia) wakati wa ufunguzi.
Picha: Mwandishi Wetu
Naibu Katibu Mkuu Nishati, Khatibu Kazungu (kushoto) akipokea mfano wa picha wenye Ramani inayoonyesha mfumo wa umeme nchi za kusini ya Afrika, kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bwawa la Nguvu Kusini mwa Afrika (SAPP), Stephen Dihwa (kulia) wakati wa ufunguzi.

KATIKA jitihada za kukuza ushirikiano na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa gharama nafuu, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imeweka mikakati mbalimbali ya kuimarisha miundombinu ya nishati katika kanda hiyo.

Mkutano wa 57 wa Kamati Kuu ya Bwawa la Umeme Kusini mwa Afrika (SAPP), umefanyika leo jijini Dar es Salaam, ulijadili namna nchi wanachama zinavyoweza kushirikiana kuzalisha, kusafirisha, na kusambaza umeme kwa tija lengo  ni kupunguza gharama za nishati na kuboresha biashara ya umeme ndani ya kanda nzima.

Nchi wanachama wa SADC ambazo zimeshiriki mkutano huo  zikiwemo Tanzania, Malawi,  Zambia, Angola na Zimbabwe,  zimeweka mikakati ya kuzalisha umeme wa kutosha, kuunganisha gridi za umeme za kikanda, na kutumia vyanzo mbadala kama vile nishati ya jua, upepo, na jotoardhi.

Mikakati hiyo inalenga kukabiliana na changamoto za upungufu wa umeme, gharama kubwa za usambazaji, na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoathiri uzalishaji wa nishati.

Akizungumza katika mkutano  huo wa Southern African Power Pool SAPP, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayesimamia Umeme na Nishati Jadidifu, Khatibu Kazungu amesema kuwa Tanzania imepiga hatua katika miradi ya uzalishaji umeme kama vile  Bwawa la Mwalimu Nyerere kwa sasa linazalisha megawati 700 na litafikia megawati 900 baada ya upanuzi kukamilika. Vilevile, serikali imejipanga kuzalisha megawati 600 kupitia nishati ya jua na megawati 5,000 kutoka jotoardhi.

Amesema Serikali ya Tanzania imejipanga vyema katika kutekeleza mikakati ya uzalishaji na usambazaji wa umeme kwa kuimarisha vyanzo vya nishati vilivyopo na kuanzisha miradi mipya ya umeme wa jua, maji, na jotoardhi.

Aidha, amesema hatua hizo zinalenga sio tu kukidhi mahitaji ya ndani, bali pia kutoa fursa ya kuuza umeme kwa nchi jirani kama Zambia, ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa umeme.

“Tanzania, ikiwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa miradi ya nishati mbadala na asilia, tunaahidi kuendelea kushirikiana na SADC katika kuimarisha miundombinu ya umeme, kuunganisha mikoa ya pembezoni kwenye Gridi ya Taifa, na kuwekeza katika miradi ya nishati safi kama vile jua na jotoardhi,”amesema  Kazungu.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),  Mhandisi Costa  Rubagunya, ameeleza wanajikita katika miradi ya kuimarisha uzalishaji wa umeme kwa kushirikiana na mitandao ya kikanda kama vile Southern African Power Pool (SAPP).

Amesema kuwa kujiunga kwa Tanzania na mitandao ya umeme ya kikanda kutaongeza uwezo wa nchi kuuza umeme kwa nchi nyingine za SADC, hasa zile zinazokabiliwa na upungufu wa nishati.

Rubagunya amefafanua kuwa Tanzania itaendelea kuwekeza katika miradi ya umeme ili kuhakikisha taifa lina umeme wa kutosha kwa matumizi ya ndani na biashara ya kikanda.

Aidha, amesema miradi hiyo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania na pia kwa kusaidia nchi jirani zinazoathirika na upungufu wa nishati.

Mwenyekiti wa Mkutano huo kutoka  nchi ya Malawi, Steven Dihwa amesisitiza kuwa ushirikiano wa kikanda katika masuala ya nishati ni muhimu ili nchi za SADC ziweze kupata umeme wa gharama nafuu na wa uhakika.

Amesema kuwa mikakati ya pamoja ya kuunganisha nchi wanachama kwenye gridi za umeme ni hatua kubwa kuelekea kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu kwa kanda nzima.