BAADA ya kupata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya KMC juzi, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema anafurahia namna wachezaji wake wanavyopambana huku akigusia walinyimwa penalti katika mechi waliyopoteza dhidi ya watani zao Yanga iliyochezwa Oktoba 19, mwaka huu.
Simba imefikisha pointi 25 baada ya kucheza michezo 10 ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, imeshinda mara nane, imetoka sare moja na imepoteza mechi moja.
Fadlu alisema kwa sasa kila mchezaji anayepewa nafasi ya kuanza katika kikosi chake anafanya kile anachokitaka na inasaidia kupata matokeo mazuri.
"Nimefurahi namna timu ilivyocheza, muhimu pointi tatu na namna timu inavyocheza… tulistahili ushindi huu," alisema Fadlu.
Kocha huyo alisema wamekuwa wakipambana kucheza vizuri katika kila mchezo lakini baadhi ya vitu vinawanyima ushindi kwenye baadhi ya mechi.
"Tulicheza vizuri dhidi ya Yanga, maoni yangu nadhani tulistahili kupata penalti mbili kwa Kibu, lakini huwezi kuhoji maamuzi yaliyotolewa, tunaendelea na mbio zetu, nafurahi kuona timu inazidi kuimarika na tunapata matokeo," alisema kocha huyo.
Aliongeza kwa sasa mawazo wanayaelekeza katika michezo iliyopo mbele huku wakizidi kukiimarisha kikosi chao.
"Tutakuwa na mapumziko mafupi kwa ajili ya kalenda ya mechi za kimataifa za timu za taifa, tutayatumia kujiimarisha zaidi kabla ya kurejea tena katika ligi," Fadlu aliongeza.
Kocha huyo aliongeza kama wachezaji wake wangekuwa na utulivu, wangepata mabao mengi zaidi katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye KMC Complex, hapa jijini.
Hata hivyo alisema bado kikosi chake hakichezi kwa kasi na ubora wa juu ndani ya dakika zote 90.
"Ninawapongeza vijana wangu kwa ushindi na kwa kuzingatia maelekezo yangu, lakini sijaridhika na idadi ndogo ya mabao kipindi cha kwanza. Tumepoteza mabao matatu kabla ya kupata goli la kwanza, nadhani ilitakiwa liwe la nne, kipindi cha pili wapinzani wakabadilika, baadaye tukauchukua mchezo na kufunga mawili mengine, dakika 10 za mwisho hatukuwa katika ubora wetu," kocha huyo raia wa Afrika Kusini, alisema.
Aliongeza kwa kushirikiana na wasaidizi wake wataendelea kuimarisha maeneo wanayofanya vizuri na kurekebisha pale ambapo bado wanaona hawachezi katika ubora anaoutaka.
"Bado kuna kitu nakitafuta na sijakipata, hili nalifanyia kazi kwa sababu kuna wakati tunakuwa katika ubora unaotakiwa, lakini baadaye tunashuka, mchezo mmoja tunakuwa na kasi tofauti, tunapanda na kushuka, hili ni tatizo, nadhani tukicheza kwa kasi kwa dakika zote 90, Simba itakuwa hatari sana," Fadlu aliongeza.
Kuhusu kutoa nafasi kwa wachezaji wote, Fadlu alisema kikosi chake kimekuwa na ushindani wa namba kwa sababu anatoa nafasi kwa kila mchezaji kuitumikia timu hiyo.
"Nataka kila mmoja acheze, timu ikishinda ishinde kama timu, sitaki kikosi chenye kutegemea mchezaji mmoja au wachache ambao kama wakikosekana inakuwa katika hatari ya kupoteza mchezo," alisema.
Naye Kocha Mkuu wa KMC, Abdihamid Moallin, alisema makosa ya kizembe yaliyofanya na wachezaji wake yamesababisha timu yake kupokea kichapo hicho.
Moallin alisema walianza vyema mchezo huo lakini walipokuwa nyuma kwa mabao mawili, hali ilibadilika na wachezaji walianza kupoteza hali ya kujiamini.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED