Katika sehemu ya pili ya ripoti hii jana, kulikuwa na simulizi za wagonjwa wa kifua kikuu (TB) mgodini na hali ilivyo katika Hospitali ya Kibong’oto. Endelea na sehemu ya mwisho ya ripoti hii:
WATAALAMU wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wanasimulia namna TB ilivyo changamoto kwa vijana wa kiume, huku kundi kubwa la wanaoonwa zaidi hospitalini huko likiwa la wanaofanya kazi migodini.
Katika mazungumzo maalum na Nipashe, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani MNH, Verdiana Byemelwa, anasema takwimu za hospitali hiyo ya hadhi ya juu zaidi kitaifa zinaonesha wagonjwa wanaolazwa na wanaohudhuria kliniki, wengi wao ni wa jinsia ya kiume.
Anasema kuwa kwa mwezi Agosti mwaka huu, walikuwa na wagonjwa 21 wenye TB sugu. Kati yao, vijana ni 14 (wa kike saba).
Mtaalamu huyo anataja sababu ya vijana kuwa katika hatari ya maambukizi hayo ni mizunguko mingi waliyonayo kila siku na ni kundi ambalo halipendi kutibiwa.
Anasema vijana ni kundi ambalo hupenda kukaa wengi eneo moja; mfano chuoni, baa au migodini ambako ni miongoni mwa eneo hatarishi kwa ugonjwa huo.
Dk. Verdiana anasema kuwa kati ya waliowatibu mwaka huu, mmoja tu alirejea hospitalini huko baada ya kupata maambukizi, ambaye alikuwa katika tiba ya miezi tisa na hakuna kifo.
Akizungumzia TB kitaalamu, Dk. Verdiana anasema ni ugonjwa wa mapafu unaosababishwa na kimelea kinachoitwa Mycobacterium Tuberculosis (MTB), ambacho huathiri mapafu na sehemu nyingine za mwili kama mifupa, moyo, ubongo, tumbo na njia ya mkojo.
Anaeleza kuwa ugonjwa wa TB sugu uko wa aina mbili ukichangiwa na usugu wa dawa moja, dawa mbili au tatu.
Mtaalamu huyo anasema watu wanapata TB sugu kutokana na kushindwa kudhibiti maambukizi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine ambaye hajapata matibabu au hajagundulika kuwa na tatizo hilo.
"Mgonjwa kukaa miaka mitatu bila kutumia dawa yoyote inayostahili kutibu maradhi yake, huchangia kimelea hujibadilisha na kupata usugu," anasema.
Usugu mwingine, daktari huyo anasema huchangiwa na watu kutomaliza dozi ambapo kwa mgonjwa wa TB ya kawaida, hutakiwa kutibiwa kwa miezi sita au zaidi kwa aina nyingine ya TB, lakini baadhi ya watu hunywa dawa chini ya muda huo na kuacha na wengine hunywa kwa kuruka siku.
Pia anasema wagonjwa ambao hawatatibiwa vizuri, wanaporudi katika jamii huwa na vimelea sugu na huambukiza wengine.
"Sababu nyingine ya usugu huchangiwa na mtindo wa maisha na kufanya vimelea vibadilike kuwa sugu," anasema.
Dk. Verdiana pia anasema usugu mwingine husababishwa na mtu kutumia dawa anazonunua bila ushauri wowote wa daktari.
"Ukiwa na mgonjwa, mlete hospitalini na mwambie hatakiwi kutibiwa kwa dawa za kienyeji. Tuwaambie dawa zinachukua muda gani ili kusaidia matibabu kuwa rahisi," anashauri.
WALIO HATARINI
Kuhusu watu walio katika hatari ya kupata TB sugu, Dk. Verdiana anasema ni wenye upungufu wa kinga mwilini, wakiwamo wazee, wagonjwa wa kisukari na wenye Virusi vya Ukimwi (VVU) na wagonjwa wa saratani.
Kundi lingine lililoko hatarini kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa Muhimbili ni watoto chini ya miaka mitano kwa kuwa kinga za mwili hazijakomaa.
Dk. Verdiana anasema wagonjwa ambao wanaoonwa zaidi hospitalini huko wenye TB sugu ni walio na VVU na watu wanaofanya kazi migodini, kundi ambalo nalo wanalitaja lipo hatarini zaidi kupata maambukizi kutoka na shughuli mbalimbali zinazofanyika huko.
Mtaalamu anasema dawa zipo za kutosha na matibabu sahihi ya TB sugu huanzia miezi tisa hadi miezi 18 na huduma hizo hutolewa bila malipo.
Anasema dawa ya TB sugu inayotumika kwa sasa Tanzania yenye matumaini makubwa na kupunguza kutibu kutoka miezi 18 mpaka 24 na kurudi miezi tisa ni Bedaquiline, ambayo imeonesha matokeo makubwa kwa wagonjwa.
Dk. Verdiana anasema changamoto wanazokutana nazo katika kuwahudumia ni mapokeo ya wagongwa wengi, hawaamini kama kweli wana TB sugu na hawapendi kukaa hospitalini.
"Wapo wenye TB sugu na wana magonjwa mengine ambayo matibabu yake yanakwenda nje ya TB sugu, huitaji kulipia, sasa wagonjwa wanakuwa hawataki kulipia, wanafikiri matibabu yote ni bure.
"Kwa mfano mgonjwa anakuwa na TB sugu na ana kisukari, matibabu ya kisukari mfano dawa zake, sasa mgonjwa anataka vyote vilipwe na hospitali.
"Hivyo, baadhi ya ndugu huondoka na hutuachia wagonjwa. Serikali hulipa gharama za TB, lakini magonjwa mengine yaliyojitokeza kwa mgonjwa wa TB yanayopaswa kulipiwa na mgonjwa hajalipa, hospitali huingia gharama," anasema.
Kwa mwaka wa fedha 2021/22, kiasi cha fedha kilichotumika kwa wagonjwa wote wa msamaha waliotibiwa Muhimbili - Upanga ni Sh. bilioni 19, 2022/23 Sh. bilioni 18 na 2023/24 Sh. bilioni 13.
Dk. Verdiana anaendelea kusema wagonjwa wengi wa TB sugu hujificha kwa kuhofia unyanyapaa kwa kuona wakisema watakaa hospitalini miezi mitatu na nyumbani kutengwa kuanzia vyumba, vyombo mpaka vijiko.
Dk. Verdiana anasema Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia ripoti yake ya mwaka 2020 linaonesha Tanzania ni miongoni mwa nchi sita za Afrika zenye idadi kubwa ya wagonjwa wa TB. Nchi zingine ni pamoja na Ethiopia, Kenya, Namibia na Afrika Kusini.
"Kwa Tanzania, mwaka 2020 wagonjwa 26,800 waliripotiwa kufariki dunia kwa TB. Kwa dunia nzima, Tanzania ipo nafasi ya 15 kwa nchi ambazo zina maambukizi ya TB.
MTOTO AGUNDULIKA TB SUGU
Mratibu TB na Ukoma Muhimbili, Dk. Nuru Msanga, anasema kuwa mwaka 2021 walipokea mtoto wa miaka miwili mwenye TB sugu.
"Aliletwa Muhimbili akionekana kama ana dalili za shida ya kupumua, alikuwa na shida ya moyo, kinga zake ni ndogo na alikuwa na maambukizi ya VVU.
"Akalazwa na baadaye aliingizwa Chumba cha Uangalizi Maalum (ICU), alipopimwa ndipo ikabainika ana TB sugu," anasema.
Dk. Msanga anasema kwa sasa wagonjwa wenye TB sugu walioko Muhimbili wakijumlisha na wale wanaokuja kwa ajili ya matibabu wapo 21. Wenye TB ya kawaida idadi yao ni zaidi ya 200.
"Ukiongeza na kituo chetu cha IDC kwa wenye TB ya kawaida ni wagonjwa kati ya 400 mpaka 500, lakini kwa TB sugu wapo 21 kwa sasa," anafafanua.
Mei 13, mwaka huu, aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alisema wataendelea kusimamia utoaji huduma za TB na ukoma kwa mujibu wa Mpango Mkakati wa Sita (2020/21 - 2025/26) wa kupambana na magonjwa hayo.
Alisema serikali imetenga Sh. bilioni 84.864 ili kufanikisha mpango huo ikiwamo ununuzi wa vifaa tiba, vitendanishi na dawa za kutibu.
Alitaja malengo makuu ya mpango huo ni kupunguza maambukizi mapya ya TB kwa asilimia 50, kupunguza vifo kwa asilimia 75.
"Hadi kufikia mwezi Machi, mwaka huu, Tanzania imepunguza maambukizi mapya ya TB kwa asilimia 36, kutoka wagonjwa 306 kwa kila watu 100,000 mwaka 2015 hadi wagonjwa 195 kwa kila watu 100,000 mwaka 2023.
"Takwimu zinaonesha vifo vitokanavyo na TB vimepungua kwa asilimia 67 kutoka vifo 56,000 mwaka 2015 hadi vifo 18,000 mwaka 2023 na hivyo kuwa kwenye njia sahihi ya kufikia lengo la kupunguza maambukizi kwa asilimia 50 na vifo kwa asilimia 75 pindi ifikapo mwaka 2025," alisema.
Ummy alisema katika kipindi hicho jumla ya wagonjwa 194 wa TB sugu waligundulika na kuanzishiwa matibabu ambao ni sawa na asilimia 43 ya lengo la kugundua wagonjwa 453, kulinganishwa na wagonjwa 266 waliogundulika katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23 sawa na asilimia 40 ya lengo la kuibua wagonjwa 664 wa TB sugu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED